Majaji wa mahakama ya jinai ya ICC wameamua kuwa rais wa Kenya hana budi kufika mahakamani binafsi Oktoba tarehe 8.
Majaji hao wamekatalia mbali ombi la mawakili wa rais Uhuru Kenyatta la kutaka aruhusiwe kuhudhuria kikao hicho kupitia kwa njia ya Video ama kikao hicho cha ana kwa ana kiahirishwe hadi siku nyingine kwani alikuwa amekabiliwa na kazi nyingi katika majukumuyake kama rais wa Kenya.
Majaji hao wanasema kuwa Rais Uhuru Kenyatta hakutoa sababu madhubuti ya kukosa kuhudhuria kikao hicho maalum.
Majaji hao aidha wanasema kuwa Bwana Kenyatta lazima awepo ili kujibu maswali muhumu kuhusu ushirikiano wa serikali yake na kujadili maswala muhimu yatakayowasilishwa katika kikao hicho.
Kenyatta alikuwa ameiambia mahakama kuwa amepangiwa kuhudhuria sherehe za kuadhimisha uhuru wa Uganda katika kipindi hicho.
Kauli hiyo inatolewa wakati ambapo mwendesha mashataka wa mahakama hiyo Fatou Bensouda alikuwa amepinga ombi la rais Kenyatta la kuahirisha kikao hicho ama kuruhusiwa kushiriki kikao hicho kwa njia ya video.
Bi Bensouda alikuwa ameilalamikia mahakama hiyo akidai kukosa ushahidi wa kutosha baada ya serikali ya Bw Kenyatta kumnyima stakabadhi alizotaka ili kuimarisha kesi dhidi ya kiongozi huyo wa Kenya.
Bw Kenyatta kwa upande wake naye alikuwa amewasilisha ombi mahakamani ya kutaka kesi dhidi yake itupiliwe mbali baada ya bi Bensouda kukiri kuwa hakuwa na ushahidi wa kutosha dhidi yake
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni