WAZIRI 
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitasita kuwaondoa katika 
nyadhifa zao Wakurugenzi wote watakaoshiriki katika kutoa taarifa za 
uongo kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo
 yao. 
“Serikali
 inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kuna 
baadhi ya viongozi wamekuwa wakiandika taarifa za uongo kuwa mradi 
umekamilika wakati haujajengwa, hivyo wakurugenzi watakaoshiriki kutoa 
taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa,” alisema. Waziri
 Mkuu ameyasema hayo jana jioni (Jumapili, Julai 31, 2016) wakati 
akipokea taarifa ya mkoa wa Morogoro mara baada ya kuwasili mkoani hapa 
kwa ziara ya kikazi ya siku tatu. 
Alisema alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakurugenzi katika 
halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatembelea miradi yote inayojengwa
 katika maeneo yao ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama thamani yake
 inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa. 
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Serikali haihitaji Halmashauri 
kutoa ajira za mikataba kwenye kada zilizopo katika muundo wa ajira 
hivyo ameziagiza halmashauri zote nchini kufanya mapitio ya watumishi wa
 mikataba. 
“Tumeruhusu kuajiri kwa mikataba walimu wa masomo ya sayansi kwa kipindi
 cha miaka miwili tena kwa waliostaafu. Kuna kada zilizoko katika muundo
 wa ajira hizo hatuhitaji watumishi wa mikataba wakiwemo madereva 
msiwatumikishe kwa mikataba watakosa stahili zao,” alisema. 
Akizungumzia suala la watumishi hewa mkoani Morogoro Waziri Mkuu alisema
 ni vema wakaendelea kufanya uchunguzi na ifikapo mwisho wa mwezi huu 
wawe wamekamilisha taarifa na kuanza kuchukua hatua kwa waliohusika kwa 
waliohusika. 
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk. Stephen Kebwe katika 
taarifa yake aliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu alisema mkoa unaendelea 
kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuzitaka taasisi zote za 
Serikali kufanya uhakiki wa mishahara hewa na malipo batili ya 
watumishi. 
Alisema mkoa umebaini watumishi hewa 315 ambao wameisababishia Serikali 
hasara ya sh. bilioni 2.132 ambapo timu ya uhakiki bado inaendelea na 
zoezi hilo na taarifa kamili itatolewa mara kazi hiyo itakapo kamilika. 
IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATATU, AGOSTI 01, 2016.