Jumatano, 3 Februari 2016

Basi linalotumia umeme wa jua lazinduliwa Uganda

Basi linalotumia umeme wa jua
Basi linalotumia umeme wa nguvu za jua ambalo limedaiwa na watengezaji wake nchini Uganda kuwa la kwanza barani Afrika limeendeshwa hadharani.
Basi hilo la kielektroniki aina ya Kayoola linalomilikiwa na kampuni ya Kiira Motors lilionyeshwa katika uwanja wa Uganda mjini Kampala.

Mojawapo ya betri zake zinaweza kuwekwa chaji na vibamba vya umeme wa jua katika paa la nyumba ambavyo huongeza kasi ya gari hilo hadi kilomita 80 kwa saa.
Watengezaji wake sasa wanalenga kuwavutia wateja watakanunua basi hilo ili kuvutia soko kubwa la magari duniani.
Mkurugenzi mkuu wa Kiira Motors Paul Isaac Musasizi ameiambia BBC kwamba amefurahishwa na jaribio la gari hilo lilipoendeshwa.
Raia wamefurahishwa na wazo kwamba Uganda ina uwezo wa kutengeza mfano kama huu na bw. Musasizi anasema kwamba angependelea kulisaidia taifa hilo kushindana na kampuni nyengine za magari katika eneo hili.
Pia anatumai kwamba hatua hiyo itabuni ajira zifikiazo 7000 kufikia mwaka 2018.Hatahivyo mradi huo hauwezi kuanza bila ya usaidizi wa kampuni zinazotengeza vifaa vya magari.
 
Basi linalotumia umeme wa jua
Lengo ni kwamba kufikia 2039,kampuni hiyo itakuwa na uwezo wa kutengeza vifaa vya magari na kuviunganisha nchini Uganda bila kutegemea kampuni nyengine .
Basi hilo lenye viti 35 linalenga kufanya kazi katika miji midogo badala ya mji mkuu kutokana na masharti ya umbali linakoweza kusafiri.
Iwapo mabasi hayo yatazalishwa kwa wingi,kila basi litagharimu kiasi cha dola 58,000 ambacho bw,Musaizi anasema ni bei nzuri katika soko lenye ushindani mkubwa.
Kampuni ya Kiira Motors ilianzishwa kutokana na mradi uliofanyika katika chuo kikuu cha Makerere,ambacho ni mmoja wa mmiliki wa hisa katika kampuni hiyo na pia kimenufaika na ufadhili kutoka kwa hazina ya fedha ya serikali

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni