Wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba wakimpongeza mjumbe mwenzao, David Kafulila (katikati) baada ya
kuwasilisha maoni ya walio wachache katika Kamati Namba Tano ya bunge hilo mjini
Dodoma jana. Picha na Silvan Kiwale.
DODOMA.
MJUMBE wa Bunge la Katiba, David Kafulila jana aligeuka
shujaa bungeni na kubebwa juujuu na wajumbe wenzake kutoka kundi la walio
wachache baada ya ‘kusambaratisha’ hoja za wajumbe wanaopinga Serikali tatu.
Kafulila ambaye pia
ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), alifanya hivyo alipokuwa akifafanua
hoja kutoka kundi la walio wachache katika Kamati Namba Tano.
Miongoni mwa hoja ambazo alizijibu na kushangiliwa na wajumbe, ni
juu ya gharama za Serikali tatu, kuwa zitavunja Muungano, kwamba Serikali ya
Muungano itakosa mapato, hoja ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere na uhalali wa
takwimu za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema hoja kuwa Serikali
tatu ni kuvunja Muungano si za kweli, akisema ni propaganda zilezile ambazo CCM
ilizitumia mwaka 1992 kutembea nchi nzima kupinga mfumo wa vyama vingi.
“Wakati ule CCM ilitembea nchi nzima huku wakionyesha video kuwa
vyama vya upinzani vitaleta vita, lakini leo miaka 20 baada ya kukubali mfumo wa
vyama vingi hakuna vita vilivyoletwa na upinzani,” alisema Kafulila. Alisema
haiwezekani tume zote ambazo zinaundwa na Serikali zipendekeze serikali tatu na
kila wakati serikali iliyopo madarakani ikatae.
“Hoja ya serikali
tatu siyo hoja ya Warioba, tume zote zilizowahi kuchunguza muundo ya Muungano
zote zilipendekeza serikali tatu,” alisema na kuongeza: “Ofisi ya Rais
ilipendekeza serikali tatu, ofisi ya Waziri Mkuu ilipendekeza serikali tatu,
inatuwia vigumu ndani ya muda mfupi, vyombo hivi vibadilike na kutaka serikali
mbili.”
Alisema wanaotaka serikali tatu wanataka kwa namna ambayo
inaimarisha Muungano, tofauti na maoni ya walio wengi kuwa serikali ya Muungano
itakuwa legelege kwa kuwa itakosa nguvu za kiuchumi.
“Ni kweli
inawezekana vyanzo vya mapato vilivyopendekezwa havitoshi kuendesha Bunge,
lakini ndiyo sababu tupo hapa, haiwezekani ripoti ya Tume iwe imekamilika pande
zote,” alisema na kuongeza:
“Wamependekeza badala ya kutegemea
vyanzo vya washirika, tumependekeza kodi ya bandari ambayo ni karibu Sh3.6
trilioni inaweza kuwa ni kodi ya Serikali ya Muungano. Kodi hiyo pekee inatosha
kuendesha wizara zote ambazo gharama yake si zaidi ya Sh3 trilioni.”
“Kuna hoja hapa, haiwezekani kuwa fedha za bandari zote ziwe
zinachangia Muungano kwani ni fedha za Tanganyika, lakini Muungano wowote ni
lazima kukubali nchi kubwa kuchangia zaidi.”
Kafulila ambaye hata
baada ya kumaliza muda wake wajumbe walipiga kelele wakitaka aendelee, alisema
kwa Serikali ya Muungano kupata mapato hayo tu, itakuwa haina haja ya kusubiri
fedha za nchi washirika na pia itakuwa na uwezo wa kuchangia fedha kwa nchi
washirika.
“Haiwezekani Watanganyika wakubali kubeba gharama kubwa
ya serikali mbili badala ya gharama ndogo za serikali tatu na hii ndiyo inawapa
hofu Wazanzibari kudhani kuna kitu kinachofichwa,” alisema. Kuhusu hoja ya
kutumia maneno ya Nyerere kupinga Muungano wa serikali tatu, alisema Mwalimu
hakuwa nabii, alitazama mambo kwa wakati ule na alikuwa akibadilika kutokana na
wakati.MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni