Tatizo la kunyonyoka kwa nywele na kuwa na kipara limekuwa likiwatatiza wanaume wengi kwa muda.
Shida hii mara nyingi huanza wanaume wakiwa wana miaka 30 hivi, na kufikia umri wa miaka 50 ambapo nusu ya wanaume huwa wanakabiliwa na tatizo hili.
Tatizo hili hutokana na vinyweleo vya nywele, ambavyo huwa kina cha ukuaji wa nywele, kunywea. Shughuli hii huendelea pole pole kwa muda mrefu.
Kuna wengi wanaodai kuwa na tiba ya tatizo hili, baadhi wakitumia dawa za kisasa na wengine za kiasili lakini ufanisi wake huwa tofauti.
Ni njia gani hufanikiwa?
Kwa mujibu wa Idara ya Taifa ya Afya Uingereza (NHS) kupandikizwa kwa nywele ni moja ya njia zinazofanikiwa sana.
Lakini gharama yake huwa ya juu mno.
Kupandikizwa nywele kunaweza kugharimu kuanzia £1000 hadi £30,000 [sawa na shilingi za kitanzania milioni 3 hadi 90].
Wakati mwingine, daktari wako anaweza kupendekeza utumie dawa yenye kiungo fulani ambacho hujulikana kama Finasteride. Kiungo hiki hubadilisha viwango vya homoni fulani zinazodhibiti mfumo wa uzazi katika binadamu.
Utafiti unadokeza kwamba tiba hii inaweza kusisimua ukuaji wa nywele tena katika theluthi mbili ya wanaume wenye upara.
Dawa nyingine kwa jina Minoxidil iligunduliwa kibahati miaka ya 1950 watafiti waliokuwa wanatafuta tiba ya shinikizo la damu. Inaaminika kwamba hufanya kazi kwa kwa kuongeza mtiririko wa damu kwenye ngozi ya kichwa maeneo yenye nywele na kufungua vinyweleo vya nywele.
Ikitumiwa vyema, inaweza kufanikiwa kwa asilimia 80 ya wanaoitumia, lakini huhitaji kutumiwa kwa muda mrefu.
Kutumia dawa hizi mbili kunaweza kukugharimu maelfu ya pesa kila mwaka.
Kuna ushahidi pia kwamba aina fulani ya vyakula vina uwezo wa kuzuia upara. Kuna utafiti ulioonyesha kwamba ulaji wa vyakula vyenye Omega 3 kwa wingi ulipunguza kunyonyoka kwa nywele pole pile.
Upara huhusishwa pia na upungufu wa madini ya chuma mwilini, hivyo kula mboga zenye rangi ya kijani (mfano spinachi) kunaweza pia kumfaa mtu.
Kando na kula vyakula vifaavyo, utafiti unadokeza pia kwamba kufanya mazoezi zaidi na kupunguza mfadhaiko ni mambo yanayoweza kupunguza kunyonyoka kwa nywele pia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni