MKUU WA MKOA AZOMEWA NA WANANCHI WAKE WA WILAYA YA KITETO
MKUU wa Mkoa wa Manyara,
Mheshimiwa Elaston Mbwilo, amejikuta katika wakati mgumu baada ya wananchi wa wilaya ya
Kiteto, kumzomea na kumtaka aondoke na mkurugenzi wake wakati alipokutana nao
kuzungumzia mgogoro wa wakulima na wafugaji.
Hali hiyo
ilijitokeza wakati mkulima, Ramadhani Machaku, aliposimama kuuliza swali,
lakini Mkurugenzi wa Wilaya ya Kiteto, Jane Mutagurwa, kumnyang’anya kipaza
sauti na kumtaka aulize swali badala ya kutoa hotuba.
Katika swali lake Machaku, alishutumu uongozi wa
wilaya kuwa umechangisha mamilioni ya fedha kwa wafugaji ili kuhakikisha
wakulima wanaondoka na matokeo yake kule mashambani wanaishi kama maadui na
kuuana kinyama.
Aidha alisema kuwa
viongozi wamekuwa hawataki kuongea ukweli kuhusu jambo hilo na kudai kuwa
hawataondoka katika eneo hilo hadi hapo serikali itakapowahakiki wafugaji ambao
ndiyo waliowauzia maeneo.
Alimuomba
Rais Jakaya Kikwete au Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia kati kutatua mgogoro
huo kutokana na viongozi wa wilaya hiyo kuwagawa wananchi na kupindisha
ukweli.
Hatua ya mkurugenzi huyo
kumnyang’anya kipaza sauti, kiliwakasirisha wananchi hao, ambao walianza
kuzomea huku baadhi wakisusia na kuanza kuondoka kwenye mkutano huo, wakitaka
Mkuu wa mkoa aondoke na mkurugenzi wake.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kiteto, Foka Dinya,
aliingilia kati na kuwataka wananchi hao kuacha vurugu.
Awali Mhe. Mbwilo ambaye alitoa fursa kwa wananchi
kuuliza maswali, alikiri kuwa mgogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Wilaya
ya Kiteto unasababishwa na viongozi wa wilaya hiyo na kuiagiza kamati ya ulinzi
ya mkoa kukaa kuangalia tatizo ili wilaya hiyo iwe na amani.
“Mambo haya tangu mwanzo nayafahamu lakini bado
tunayafanyia kazi lakini ni kwa nini watu wanakubali kuchangishwa fedha bila ya
utaratibu wa serikali na bila kibali maalum sisi kama serikali tunalifuatilia
haiwezekani michango ichangishwe kikabila,”alisema.
Alisema kuwa serikali ya mkoa inatambua suala hilo
la viongozi kuhusika na mgogoro huo.
Alisema kuwa tangu juzi amefanya ziara na kupokea
malalamiko na taarifa kuwa viongozi wa wilaya walipokea rushwa ya madume ya
ng’ombe kutoka kwa wafugaji ili wakulima waondolewe katika Hifadhi hiyo.
“Wananchi kweli mmegawanywa katika makundi na
inawezekana ni sisi viongozi ndiyo tuliofanya hivi na matokeo yake wafugaji
wanaona wana haki ya kukaa ndani ya hifadhi huku wakulima nao wanaona
wamehujumiwa kwanini wafugaji wakubaliwe,” alisema Mbwilo.
Alisema kuwa mgogoro huo ulitokana na baadhi ya
wakulima kuingia katika eneo la hifadhi kinyume na sheria na kujichukulia ardhi
kubwa mpaka kumiliki hekari 6000.
Aliwataka wakulima na wafugaji kuondoka katika
hifadhi hiyo mpaka hapo watakapofanya utaratibu wa kugawa tena kulingana na
vielelezo watakavyowasilisha kuwa walipewa idhini na nani ya kumiliki maeneo
hayo.
Aliwaagiza viongozi wa wilaya
kuwaondoa katika eneo hilo wakulima na wafugaji wote kwa pamoja kwa kuwa
wameingia kinyume na sheria tofauti na agizo la awali ambalo liliwataka wakulima
kuondoka.
Awali mmoja wa wafugaji wa
jamii ya Kimasai, Kisioki Masiyai, alisema kuwa chanzo cha mgogoro na
kusababisha mapigano ni Mkurugenzi wa wilaya hiyo, ambaye aliwachangisha fedha
wafugaji ili kuwaondoa wakulima.
Alisema kuwa hawatakubali kuondoka katika hifadhi
hiyo mpaka hapo serikali ya wilaya hiyo itakapotoa mchanganuo wa matumizi ya
mamilioni ya fedha ambazo walichangishwa wafugaji. CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni