Tembo wakijitafutia
chakula mwituni, Serikali imesisitiza kurejesha Operesheni Tokomeza Ujangili,
ikitangaza kuwa tembo 13,000 tu ndio waliosalia katika Mbuga za Wanyama za
Selous na Mikumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu, alitoa msisitizo wa kurejea kwa operesheni hiyo itakayoanza hivi karibuni, huku akibainisha kuundwa kwa Tume ya Kimahakama kuwashughulikia wote waliohusika kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya wananchi wakati wa utekelezaji wa operesheni ya awali.
Mbele ya mabalozi kadhaa wanaoziwakilisha nchi zao nchini na wadau mbalimbali wa Maliasili na Utalii, Nyalandu alitangaza rasmi matokeo ya sensa hiyo iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba mwaka jana kupitia mfumo wa ekolojia wa Mbuga za Selous, Mikumi, Ruaha na Tungwa.
“Matokeo ya sensa hii yanaonyesha kwamba mfumo wa ikolojia wa Selous na Mikumi kwa sasa una tembo 13,084 na Ruaha-Rungwa una tembo wanaokadiriwa kuwa 20,090, takwimu ambazo zinaonyesha kupungua kwa idadi ya wanyama hao, hasa Mikumi ikilinganishwa na sensa ya awali,” alisema Nyalandu.
Alisema kuwa takwimu za mwaka 1976 za Selous-Mikumi zinaonyesha kuwa kulikuwa na tembo 109,419 idadi ambayo ilipungua na kufikia 22,208 mwaka 1991 kutokana na wimbi la ujangili, kabla ya kuongezeka tena na kufikia 70,406 mwaka 2006 baada ya Operesheni Uhai iliyofanyika kati ya mwaka 1989 hadi 1990.
“Kwa matokeo haya, inaonyesha kuwa mfumo wa Ikolojia ya Selous- Mkumi idadi ya tembo imepungua kwa asilimia 66 ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2009 ambapo kulikuwa na jumla ya tembo 38,975, wakati kwa upande wa Ruaha –Tungwa tembo wamepungua kwa asilimia 36.5 ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2009, ambapo walikuwa 31,625,” alisema.
Katika hatua nyingine Waziri Nyalandu alimtembelea askari wa wanyamapori katika Pori la Akiba Ugalla mkoani Tabora, Richard Temu aliyelazwa katika Hospitali ya Tiba ya Mifupa(Moi), ambaye alivunjika mguu wa kushoto wakati yeye na wenzake wakiwa katika harakati za kukabiliana na majangili.
“Wizara inatambua umeumia ukiwa katika harakati za kupambana na majangili na itakuhudumia. Inawasiliana kwa karibu na madaktari wanaokuhudumia ili kujua maendeleo yako,” alisema Nyarandu,
Kwa upande wake askari huyo alisema kuwa anaendelea na matibabu na kwamba Jumatano ya wiki ijayo anatarajia kufanyiwa upasuaji wa mguu wake huo uliovunjika mara mbili, wakati akiwa kwenye harakati ya kuwakabili majangili waliokuwa na bunduki.
“Mimi ndiyo nilikuwa kiongozi wa msafara wa kupambana na majangili wale. Tuliwaona wakiwa kama mita 150, wakati najipanga vyema ili kuwakabili mguu unaingia kwenye shimo dogo ndipo nikavunjika, hapo tena wenzangu wakaanza kunihudumia wale wahalifu wakapata fursa ya kutokomea,” alisimulia BwanaTemu. MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni