Na Walter Mguluchuma-Katavi
MKAZI wa Kijiji cha Uzega Tarafa ya Inyonga wilayani Mlele mkoani Katavi, Mashaka Kianga, amejeruhiwa vibaya mguu wake wa kushoto hadi kuvunjika, baada ya kupigwa na rungu na mke wake mkubwa wakati alipokuwa akiamua ugomvi wa wake zake, mkubwa na mdogo waliokuwa wakigombea mifuko mitupu ya mbolea ya tumbaku.
Tukio hilo la mume kupigwa rungu na mke wake mkubwa, lilitokea juzi saa nne asubuhi katika Kijiji cha Uzega.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Abel Kalifumu, alisema kabla ya Mashaka kujeruhiwa, aliwakuta wake zake wakiwa wanapigana kugombania mifuko mitupu ya mbolea ya tumbaku aina ya NPK.
Alisema ugomvi wa wanawake hao ulianza baada ya mke mkubwa kumtaka mke mdogo ampatie mifuko hiyo, hata hivyo mke mdogo alimkatalia ndipo ugomvi ulipoanza.
Kalifumu alisema wakati wanaendelea na ugomvi, mume wao aliwakuta wanaendelea kupigana, jambo lililoonekana kumkasirisha.
Mashaka alichukua fimbo na kuanza kuwacharaza viboko kwa lengo la kuwaamua, ndipo mke mdogo alivyoona viboko vimemzidia aliamua kukimbia na kumwacha mwezake eneo hilo. Ndipo mke mkubwa alifanya kweli kwa kumtandika mumewe kwa rungu na kumvunja mguu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni