Jumamosi, 25 Januari 2014

BASI LA TAQWA LAGONGANA USO KWA USO NA LORI NZEGA...


Basi la Taqwa.

Dereva wa basi la kampuni ya Taqwa, Adam Ibrahim (50) amekufa papo hapo huku abiria kumi wakijeruhiwa baada ya basi alilokuwa anaendesha kutoka Dar es Salaam kwenda Bujumbura, Burundi kugongana na lori katika kitongoji cha Ngonho, Kata ya Miguwa wilayani Nzega.
Ajali hiyo imethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Bitun Msangi aliyesema ilitokea juzi saa 2 usiku. Amelitaja basi hilo kuwa ni lenye namba T 532 BYJ lililogongana na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 984 AGK.
Alisema dereva wa Taqwa alikuwa katika mwendo kasi akitaka kulipita gari aina ya Mitsubishi Fuso lililolokuwa mbele yake na aliongeza mwenda ili alipite, alikutana na lori hilo lililokuwa linaendeshwa na Khalfani Hussein aliyejeruhiwa vibaya na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga wilayani Igunga.
Msangi aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Aziza Nassoro na Tatu Shabani ambao ni raia wa Burundi, Marieta Petro, mkazi wa Singida, Mwanakaombo Tau Mkazi wa Nzega, Tau Omary mwanafunzi wa chekechea mkazi wa Nzega, Khadija Rashidi mkazi wa Dar es Salaam, Hamad Ally ambaye ni fundi wa basi la Taqwa na Richard Mtaru, mkazi wa Moshi ambaye ni dereva msaidizi wa basi hilo.
Kutokana na ajali hiyo, Msangi amewataka madereva kuzingatia na kutii sheria barabarani ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.
Majeruhi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti katika hospitali ya wilaya ya Nzega walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi hilo.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa wilaya, Emmanuel Mihayo alisema afya za majeruhi hao zinaendelea vizuri huku wengine wakitarajiwa kupewa ruhusa tayari kwa kuendelea na safari zao.
Ajali hiyo ni moja ya ajali za barabarani ziliripotiwa wiki hii, zikiwemo mbili zilizoua watu 26 huko Singida na Lindi siku ya Jumatatu.
Ajali ya kwanza iliyoua watu 13 papo hapo na mmoja kujeruhiwa, ilitokea baada ya gari dogo la abiria aina ya Toyota Noah walilokuwa wakisafiria, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo eneo la Isuna, barabara kuu ya Singida-Dodoma.
Ya pili ni iliyoua watu 13 na kujeruhi wengine 25 baada ya basi la Al Hamdullilah walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara, kuacha njia na kupinduka mtaroni saa 7.30 mchana

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni