Jumamosi, 25 Januari 2014

BARABARA YA MOROGORO-DODOMA YAFUNGULIWA


Magari ya mizigo kutoka pande zote barabara ya Morogoro- Dodoma, yakipita kwenye daraja la Mkundi - Magole, wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, baada ya jana asubuhi kukamilishwa na kuruhusiwa kupita kwa zamu kila upande.
Magari yaliyokuwa yamekwama kwa siku tatu kuanzia Januari 22, kwenye barabara kuu ya Morogoro - Dodoma, baada ya daraja la Mkundi eneo la Magole, wilayani hapa kuharibiwa na mafuriko, yalianza kupita jana asubuhi baada ya matengenezo ya muda kukamilika.

Mbali na malori, pia mabasi yaliyokuwa yakitoka Dodoma nayo yalipita eneo hilo, baada ya gari la kwanza kuruhusiwa saa 4:30 asubuhi, siku mbili baada ya kuanza matengenezo yaliyopangwa kuchukua siku nne hadi kesho, kazi iliyozinduliwa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana eneo la Magole, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alimpongeza Waziri Magufuli kwa kusimamia kazi hiyo usiku na mchana hadi kukamilika ndani ya siku mbili tofauti na makadirio ya awali ya siku nne.
Mkuu wa Mkoa pia alishukuru wahandisi wa Kichina kutoka kampuni ya ujenzi ya CCECC kwa kutoa msaada wa magari ya kusomba mawe na kujaza eneo la meta 40 la tuta lililobomolewa na mafuriko kwa upande wa Morogoro na meta 10 upande wa Dodoma wa daraja hilo, hali iliyosababisha kukwama kwa usafiri hasa wa malori.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni