MKAZI wa Shinyanga Julius John [30] ameuawa na wananchi wilayani Kahama, kwa kupigwa na kisha kuchomwa moto baada ya kutuhumiwa kuiba baiskeli na karanga zenye ujazo wa gunia moja.
Tukio hilo limetokea baada ya Julius kwenda nyumbani kwa shangazi yake Justina John [48] katika kijiji cha Kasomela Kata ya Kinamapura wilayani Kahama na kisha kufanya uhalifu huo.
Mlinzi wa amani kwenye Kata hiyo Clement Bilike ameeleza kuwa baada ya Julius kuwa ugenini, shangazi yake alisafari huku akimuacha nyumbani kwake na watoto.
Hata hivyo Julius alichukua baiskeli pamoja na gunia moja la Karanga na kuanza kutoroka mnamo mida ya saa moja jioni hadi kijiji cha jirani cha Ilemve ambapo baiskeli ilipata pancha.
Akiwa katika harakati za kutafuta namna za kuziba tairi ya baiskeli hiyo alikamatwa na wananchi na kuanza kupigwa hadi kupoteza maisha na baadaye kuchomwa moto na wananchi hao waliokusanyika baada ya kupigwa yowe.
Polisi wilayani Kahama walifika kwenye tukio na kuruhusu mabaki ya mwili wa marehemu Julius kuzikwa na kwamba uchunguzi juu ya tukio hilo bado unaendelea.
Hata hivyo wananchi wanashauriwa kuacha kuchukua sheria mikononi mwao badala yake wawapeleke watuhumiwa wa uhalifu kwenye vyombo vya dola (TK).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni