WAZIRI
wa Uchukuzi, Samuel Sitta, amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Madeni Kipande, kwa tuhuma
za utendaji mbovu, uliosababisha malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali.
Sitta amechukua
uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam wakati alipozungumza na waandishi
wa habari kuhusu uamuzi huo ambao umefikiwa baada ya kufanyika kwa kikao
cha dharura cha Bodi ya Mamlaka ya Bandari kilichofanyika hivi
karibuni.
Hatua hiyo ya Sitta imekwenda
kinyume na mtangulizi wake, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa
akimwona Kipande ni mtendaji aliye makini.
Sitta alisema tangu kuingia kwa
Kipande, kumekuwa na malalamiko mbalimbali ikiwamo kutokuwapo uwazi
katika utoaji wa zabuni zinazotangazwa na mamlaka hiyo.
Alisema kumekuwa na malalamiko
kuhusu utoaji wa zabuni ambazo zimekuwa zikitolewa katika mazingira
ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wadau mbalimbali, kwamba hazitolewi
kwa uwazi, huku kukiwa na ubababaishaji kwa kamati za zabuni kubadilika
mara kwa mara.
“Jamani bandari ni kituo muhimu kwa
uchumi wa nchi wala haina haja ya kuelezea kwa kirefu, Takwimu
zinaonyesha asilimia 43 ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato hutokana na
mfumo wa forodha, kati ya makusanyo hayo asilimia 87 yanakusanywa katika
Bandari ya Dar es Salaam,” alisema.
Alisema pamoja na Waziri Mwakyembe
kuyashughulikia malalamiko hayo, lakini bado bodi ya zabuni inapokuwa
imetoa uamuzi kumekuwa na ucheleweshwaji wa kutoa barua ya kuwaruhusu
wahusika kuanza kazi hali iliyokuwa ikizua taswira mbaya kwa Serikali na
nchi kwa ujumla.
“Kwa vile mhusika mkuu ni Kaimu
Mkurugezi Mtendaji, hivyo basi naamua kumsimamisha kazi hadi hapo tume
niliyoiteua itakapokamilisha kazi ndani ya wiki mbili kuhusu malalamiko
hayo,” alisema.
Sitta amemteua Meneja wa Bandari, Awadh Massawe, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wakati uchunguzi unapoendelea dhidi ya Kipande.
Pia ametangaza tume ya watu watano
ambayo itafanya uchunguzi kwa wiki mbili kuhusu Kipande, ambayo itakuwa
chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa ya Kodi, Augusta
Bubeshi.
Wajumbe wengine ni Mkurugenzi
mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dk. Ramadhan
Mringa, mtumishi wa Wizara ya Uchukuzi, Deogratias Kasinda pamoja na
Samson Luhigo, Happines Semkoro na Flavian Kinunda ambao wote ni
wastaafu kutoka idara mbalimbali za Bandari.
Sitta alisema sababu ya kuchukua
wastaafu imechangiwa na ukweli kwamba hawana mpango wa kutaka cheo na
watatenda kazi yao kwa kuzingatia haki.
KIPANDE AZUNGUMZA
Kwa upande wake, Mhandisi Kipande alipotakiwa kuzungumzia uamuzi huo
uliochukuliwa na Waziri Sitta, alisema alifanya kazi kwa juhudi kadiri
alivyoweza na Watanzania wataamua kuhusu hilo.
“Nimefanya kile ambacho kazi
imetaka nifanye na naamini Watanzania wataamua katika utendaji wangu,
hadi sasa bado mimi sijaona kosa nililofanya,” alisema.
Kipande alipata nafasi hiyo baada
ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Dk. Harisson Mwakyembe kumsimamisha kazi
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Ephrahim
Mgawe pamoja na wasaidizi wake wawili ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za
wizi.
Kutokana na kumsimamisha kazi
mkurugenzi huyo, Dk. Mwakyembe alimteua Mhandisi Kipande kukaimu nafasi
ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
MAKOSA YA KIPANDE
Taarifa
ya ndani ya Waziri Sitta imeeleza makosa ya Kipande ikisema Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania ipo katika kipindi cha misukusuko mikubwa
ya kiutawala jambo linaloashiria hatari ya anguko kubwa la uchumi wa
nchi yetu.
“Hatari hii itagusa kwa kiasi
kikubwa nchi jirani ambazo tegemeo lake ni bandari za Mamlaka. Nchi hizi
hupitisha wastani wa asilimia 30 ya jumla ya shehena yote inayohudumiwa
kupitia Bandari ya Dar es Salaam,”imesema taarifa ya Waziri Sitta na
kuongeza:
“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia
43 ya makusanyo yote ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatokana na
Kodi ya Ushuru wa Forodha (Customs and Excise Duty).
Kati ya makusanyo hayo asilimia 87
yanakusanywa kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Hii inaonyesha kuwa
Bandari ya Dar es Salaam ina mchango mkubwa katika makusanyo ya mapato
ya taifa.”
Katika taarifa hiyo, Sitta amesema
tangu ameingia wizarani hapo, amekuta matatizo makubwa ya kiutendaji
yanayomhusisha Mtendaji Mkuu Kipande moja kwa moja ikiwa pamoja na
uhusiano mbaya kati yake na wadau na wateja wa mamlaka, kukiuka kwa
makusudi kwa taratibu za manunuzi na mahusiano mabaya kati yake na
wafanyakazi wa mamlaka kwa ujumla wake.
Kuhusu uhusiano mbaya na wadau na
wateja wa mamlaka, Sitta alidai tuhuma hizo zimeendelea kujenga taswira
mbaya ya taasisi hiyo ambayo inafanya shughuli za kibiashara.
“Kwa ujumla vitendo hivi vina
madhara makubwa na vikiendelea kuachwa vitaathiri biashara ya bandari
ambayo kwa sasa inakabiliwa na ushindani mkubwa. “Nimepewa taarifa na
mdau anayemiliki bandari kavu (ICD) hapa Dar es Salaam aliyefika ofisini
kwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka tarehe 05/02/2015.
Katika mazungumzo na Mtendaji Mkuu
alitolewa maneno makali na vitisho vingi na hatimaye akaambiwa kuwa
‘siogopi mtu yeyote katika Serikali hii, nenda popote sitasaini contract
yako na nimeambiwa unataka kwenda mbele basi tutakutana huko’. Tuhuma
hii kama ni ya kweli ni aibu kwa taifa,” alisema Sitta.
Aliongeza kuwa amekuta taarifa ya
mtendaji huyo ya kumfukuza Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanga Cement
aliyekwenda ofisini kwake kufuatilia maombi yao ya kupewa unafuu wa
gharama katika bandari ya Tanga.
“Tanga Cement ndio watumiaji
wakubwa wa bandari ya Tanga na miaka yote wamekuwa wanapewa punguzo la
gharama kutokana na kuisaidia bandari ya Tanga ambapo hukodisha
matishari (Barges) kutoka Mombasa ili kusaidia shughuli za kupakua meli
zinazoleta shahena yao ya makaa ya mawe kupitia bandari hiyo,”alisema.
Alisema pia amekuta taarifa kuwa
mwezi Januari mwaka huu aliwafokea na kuwafukuza wateja waliokuwa
wamekuja kumwona kwa ajili ya mizigo yao iliyokaa muda mrefu bandarini.
Sitta alisema kuwa wateja hao wa Kampuni ya KRB Freight Ltd waliondoka kwa masikitiko makubwa.
Kwa upande mwingine, Sitta amezungumzia kukiuka kwa makusudi kwa taratibu za ununuzi.
Alisema mtendaji huyo alisitisha mchakato wa zabuni ya ujenzi wa gati Na. 4 katika bandari ya Mtwara.
“Usitishaji huo ameufanya baada ya kupata maelekezo ya wizara ya kuharakisha mchakato huo,”alisema Sitta na kuongeza:
“Mtendaji Mkuu amekuwa na kawaida
ya kupinga mapendekezo ya Kitengo cha Ununuzi (Procurement Management
Unit) kwa kuondoa baadhi ya majina yanayokuwa yamependekezwa katika timu
ya wachambuzi wa zabuni (Evaluation Team) na kuweka majina anayotaka
yeye kwa sababu anazozijua mwenyewe.”
Alisema amepata taarifa pia kwamba
Mtendaji huyo Mkuu aliingilia mchakato wa zabuni ya mradi wa “Integrated
Security System” kwa kuiondoa kampuni ambayo ilikuwa imeshinda zabuni
hiyo kitendo ambacho kilifanya Benki ya Dunia kusitisha msaada kwenye
mradi huo.
“Nimetaarifiwa pia kuwa sasa mradi
huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za mamlaka na unatekelezwa na kampuni
iliyokuwa imekataliwa na Benki ya Dunia,” alisema Sitta.
Aliongeza kuwa mtendaji huyo
alipotembelea Ubelgiji bila utaratibu, aliingia mkataba wa mradi mpya wa
‘Electronic Cargo Tracking Note’.
Alisema lengo la mradi huo ni
kufuatilia na kupata taarifa za shehena yote inayoagizwa toka nje ya
nchi na kusafirishwa kwa njia ya meli kupitia bandari za mamlaka.
“Kwa makusudi hakukuwa na ushirikishwaji wowote wa menejimenti wala wadau wa bandari na pia taratibu za zabuni hazikufuatwa.
“Mradi huu umekuwa na upinzani
mkubwa toka kwa SUMATRA na wadau wa bandari kwa kuwa utazifanya bandari
zetu kuwa ghali ikilinganishwa na bandari shindani.
“Hii inatokana na ukweli kuwa kila
mwagizaji wa bidhaa angetakiwa kuilipa kampuni hiyo ya Kibelgiji wastani
wa dola za Kimarekani 150 hadi 250 kwa kontena la futi ishirini,”
alisema.
Alisema kama mradi huo
utatekelezwa, wateja wengi wataikimbia bandari ya Dar es Salaam kutokana
na ongezeko la gharama kwani hakuna bandari yoyote shindani inayotumia
mfumo huo kwa sasa.
Kuhusu uhusiano mbaya kati yake na
wafanyakazi wa mamlaka kwa ujumla wake, Sitta alidai kupata taarifa
kwamba kauli na vitendo vya Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Bandari
vinakatisha tamaa katika kujenga ufanyakazi wa pamoja na morali kwa
wafanyakazi wakiwamo wafanyakazi wake.
“Ninayo taarifa pia kuwa kwa
maelekezo ya Mtendaji Mkuu kumekuwapo kwa uhamisho wa watendaji
mbalimbali ambao hauna tija kwa shirika.
Mara kadhaa baadhi ya wafanyakazi
wamekuwa wakihamishwa kituo kimoja hadi kingine bila kuzingatia uwepo wa
nafasi,” alisema katika taarifa hiyo.MTANZANIA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni