NA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM
MAISHA ya
vijana wengi wa Kitanzania yapo hatarini kutokana na unywaji pombe na uvutaji
sigara kupita kiasi, unaotajwa kuwa miongoni mwa sababu za kupatwa na ugonjwa wa
moyo.
Kauli hiyo
ilitolewa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Robert Mvungi, alipozungumza na waandishi wa
habari katika Siku ya Moyo Duniani iliyoadhimishwa kidunia jana.
Dk.
Mvungi alisema wagonjwa wa moyo wanaofika kupata tiba katika hospitali hiyo ni
wastani wa watu 20,000 kwa mwaka na asilimia kubwa kati yao ni vijana.
Hospitali ya Muhimbili
Alisema hali hiyo inachangiwa na mtindo wa maisha ambao
wengi wao wamekuwa wakiishi kwa kunywa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara,
kula vyakula vyenye mafuta ya wanyama kwa wingi pamoja na kutokufanya mazoezi.
“Tumekuwa tukipokea watu 20,000 kwa mwaka hapa Muhimbili ambao
wanasumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kati yao idadi kubwa huwa ni vijana,”
alisema Dk. Mvungi.
Kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa, Dk. Mvungi
kupitia Kitengo cha Moyo wameamua kuhamasisha jamii kula vyakula ambavyo havina
athari kwao na kuepukana na tabia ya kutokufanya mazoezi ili kuondoa uwezekano
wa kupata ugonjwa huo.
“Huu ni ugonjwa hatari iwapo watu hatutachukua
tahadhari, kwa sababu kila mwaka takribani watu milioni 17.3 duniani wamekuwa
wakifariki dunia kutokana na kuugua ugonjwa huo,” alisema.
Septemba 29
kila mwaka, dunia nzima huadhimisha Siku ya Ugonjwa wa Moyo ambayo huambatana na
kaulimbiu mbalimbali kwa lengo la kuielimisha jamii kujua na kufuatilia undani
wake.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Muhimbili,
Dk. Delila Kimambo, alisema maadhimisho kwa mwaka huu yamepewa kaulimbiu isemayo
‘Jenga afya ya moyo, kazini, majumbani na michezoni’, ikilenga kuhamasisha jamii
kujenga mazingira mazuri katika kila eneo kwa kukwepa mambo ambayo yanaweza
kusababisha kuugua ugonjwa huo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani
(WHO), zinaonyesha kuwa ugonjwa wa moyo husababisha vifo vya watu milioni 17.3
kila mwaka.
Ugonjwa huo ni wa pili duniani baada ya malaria unaongoza
kwa kusababisha vifo vya watu.
SABABU ZA UGONJWA WA MOYO
Mienendo mibovu ya maisha ikiwamo uvutaji sigara, ulevi, ukosefu wa
mazoezi ya mwili na chakula bora kwa kiasi kubwa vinachangia ongezeko la vifo
vitokanavyo na ugonjwa huo nchini.
Wataalamu wa afya wanataja sababu
nyingine kuwa ni umri, jinsia, historia ya familia, shinikizo la damu, kisukari,
msongo wa mawazo na uchafu.
Takribani asilimia 80 ya vifo vya mapema
vitokanavyo na ugonjwa wa moyo vinaweza kuzuilika kwa kuepuka sababu hizo
hatarishi.
TAFITI
Utafiti uliofanyika mwaka 2012 na Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii na WHO, unaonyesha kuwa asilimia 26 ya Watanzania
wanakabiliwa na ugonjwa wa moyo huku asilimia 20 kati yao wakiwa wanawake.
Taarifa za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa asilimia 92.6 ya Watanzania
wenye ugonjwa huo hawapo kwenye matibabu licha ya kutambua kuwa wanaugua.
WHO inaeleza kuwa takriban asilimia 40 ya watu wazima katika Bara la
Afrika wanaugua ugonjwa huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni