Jumanne, 3 Juni 2014

HATIMAYE MTOTO NASRA AZIKWA KISHUJAA

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera wakati wa maziko ya mtoto Nasra makaburi ya Kola
RASHID Mvungi, baba mzazi wa mtoto Nasra (4), aliyefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili , Dar es Salaam, alikolazwa kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimkabili yanayosadikiwa kuchochewa na mateso aliyoyapata alipokuwa akiishi kwenye boksi kwa takribani miaka minne, ameshindwa kumzika mwanae katika makaburi ya Kola, Manispaa ya Morogoro.
Kushindwa kwake kuhudhuria kuweka undogo katika kaburi la mwanae ni baada ya kuzuiwa na Polisi kwenda makaburini kwa madai ya kumwepusha na hatari ya hasira za wananchi kwa unyama waliomfanyia Narsa na walezi wake wawili.
Baba mzazi huyo , licha ya awali kushiriki kwenda Jijini Dar es Salaaam kuuchukua mwili wa mwanae pamoja na viongozi wa Idara ya Ustawi wa Jamii Mkoa na Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia , pia alikuwepo uwanja wa Jamhuri wa Mjini hapa kushiriki shughuli za kuangwa kwa mwili wa mtoto huyo.
Mvungi alikuwa ameketi mstari wa mbele ya jeneza la mwanae wakati wote wa kutolewa nasaha mbalimbali za viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa , Joel Bendera na wale wa dini wakiendesha sala ya kabla ya mwili kuondolewa kwenda msikitini kusaliwa.
Hata hivyo mara baada ya kumalizika shughuli hiyo Mvungi alichukuliwa na Askari Polisi wa kitengo cha Upelelezi Mkoa.
Akihojiwa na Mwandishi wa Habarileo, eneo la Makaburi ya Kola, juu ya kutoonekana kwa baba mzazi wa marehemu , Narsa, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa , Kibona, alisema kuwa, isingekuwa jambo la busara kuruhusu Mvungi ashiriki mazishi makaburini kutokana na kuhofia hasira za wananchi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa , kuwa Mvungi aliondolewa uwanjani hapo kwa ajili ya kulinda usalama wale mara baada ya kumalizika kwa shughuli za kuangwa kwa mwanae.
John nditi wa habarileo Morogoro

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni