Uchunguzi unaohusisha vitengo vitatu vya serikali ya Kenya
umeanzishwa kufuatia madai ya mtoro wa ugaidi anayesakwa duniani Samantha
Lewthwaite, maarufu kama 'White Widow' , anayedaiwa kuonekana katika eneo la
Lamu pwani ya Kenya.
Maafisa wa uchunguzi wa jeshi la Kenya kwa ushirikiano na maafisa wengine
kutoka idara ya polisi na wizara ya usalama wa ndani wanachunguza madai kuwa
maafisa wa polisi mjini Lamu walimpa ulinzi mama mmoja mzungu, ambaye alitoweka
baada ya maafisa wa forodha na uhamiaji kumzuia kuondoka Kenya na kuingia nchini
Somalia.
Ripoti zinasema kuwa polisi walimpa ulinzi mama huyo aliyedai kufanya kazi na
shirika moja la kimataifa na alitaka kutembelea kambi ya wanajeshi wa Kenya
nchini Somalia.
Alipofika eneo la mpakani la Kiunga maafisa wa uhamiaji walihoji uhalali wa
stakabadhi zake na hivyo kumzuia kuondoka.
Mara tu baada ya tukio hilo, mama huyo alitoweka hadi sasa hajulikani
aliko.
Msemaji wa majeshi ya Kenya, Willy Wesonga amethibitisha kuwa kundi la
makachero wamekabidhiwa jukumu la kuchunguza ikiwa kweli mwanamke huyo ni
Samantha Lewthwaite na ikiwa ndiye, ni kwa nini alitaka kuzuru kambi ya
wanajeshi wa Kenya.
Kamanda wa polisi katika kaunti ya Lamu, Leonard Omollo, amethibitisha kuwa
maafisa wake walimpa ulinzi mama mmoja mzungu. Amesema wao hawakuwa na wasi wasi
kwa kuwa aliwapa stakabadhi za kujitambulisha ila wao hawakuwa na hofu kuwa ni
za kugushi.
Polisi pia wanalitafuta gari ambalo alikuwa amelikodisha baada ya
kuthibitisha kuwa gari lilo hilo ndilo lililotumika majuma mawili yaliyopita
katika shambulio dhidi ya wanajeshi wa Kenya ambapo wanajeshi wawili waliuawa na wengine
kujeruhiwa.
Samantha aliwahi kudaiwa kuhusika na mashambulizi ya kigaidi yaliyokumba
jengo la kifahari la Kenya Westgate mwaka jana
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni