Jumatano, 18 Februari 2015

BAADA YA SINEMA YA AMBONI: WANANCHI WAHOJI UWEZO WA JESHI LA POLISI


Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu

Magu. Matukio ya ujambazi na mauaji ya kutumia silaha, yameanza kuibuka kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini.

Hali hiyo imekuwa ikihojiwa na wananchi na wapenda amani na zaidi ni kuhusu intelijensia ya polisi kushindwa kugundua mipango ya uhalifu.




Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa kushamiri kwa matukio hayo kunaleta hofu katika jamii huku jamii yenyewe ikilaumiwa kwa kukaa kimya kwa watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na hutumia isivyo halali.


Hali hiyo imetokea mjini Magu, mkoani Mwanza kwa watu wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto usiku wa kuamkia jana walifunga Mtaa wa Kisesa Kata ya Kisesa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza na kumuua mfanyabiashara Nestory Andrew umbali wa mita 50 kilipo Kituo cha Polisi.


Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku, majambazi hayo yalifunga Barabara ya Mwanza-Musoma kwa muda na kusababisha taharuki kwa wakazi wa Kisesa huku milio ya bunduki ikitawala anga.


Wakizungumza na Mwananchi eneo la tukio jana, mashuhuda walisema walianza kusikia milio mizito ya vitu kama bomu na kwamba baada ya muda wakaona watu wakivamia duka la mfanyabiashara huyo na kupiga risasi hewani.


Mmoja ya mashuhuda hao, Daud Mwalimu alisema “Mimi ni fundi baiskeli hapa stendi jana (juzi) muda kama wa saa mbili usiku nilisikia sauti ya vishindo kama bomu, lakini baada ya muda nikasikia sauti za bunduki hewani,”


Aliongeza: “Kwa kweli tulitawanyika watu wote hapa mtaani na kuacha mali zetu. Baada ya kutulia tulikuja kushuhudia nini kilitokea, lakini tulikuta mtu mmoja ambaye ni mfanyabiashara hapa Kisesa anavuja damu tulimuangalia tukamkuta amefariki.”


Shuhuda mwingine, Emmanuel Juke alisema watu hao walifunga Barabara ya Mwanza-Musoma na kwamba, walikuwa wakipiga risasi ovyo hewani.


Juke alisema hali ilikuwa mbaya, kwani hawakuwahi kushuhudia tukio kama hilo na mtu aliyefariki alikuwa mfanyabiashara maarufu Kisesa.


Mwandishi wa habari hizi jana alifika Kituo cha Polisi Kisesa ambako askari wa kituo hicho walikiri kuwapo kwa tukio hilo huku wakitaka atafutwe Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Magu.


Kamanda w Polisi Magu, Charles Mkapa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini akadai msemaji mkuu ni Kamanda wa Polisi Mwanza.


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Robert Mnyandwa alimtaja mfanyabiashara aliyefariki baada ya kupigwa risasi na majambazi hao kuwa ni Nestory Andrew mkazi wa Igoma.


Mnyandwa alisema hivi sasa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba, hata thamani ya mali na fedha zilizoporwa haijajulikana kwani mhusika alifariki dunia.


“Ni kweli tukio limetokea jana saa mbili usiku na mtu mmoja ambaye ni mfanyabiashara wa Kisesa alipigwa risasi na kupoteza maisha. Bado hatujamkamata mtu na tunaendelea na uchunguzi,” alisema Mnyandwa.


Kufungwa kwa mitaa na majambazi, kumesababisha wafanyabiashara hasa wanaojihusisha na biashara ya fedha kwa mitandao kufunga maduka yao mapema.


Wafanyabiashara kadhaa wamekwishauawa ama kuporwa fedha zao kutokana na majambazi hayo kuvamia maduka yao.MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni