JAJI Mkuu Mohamed Othman Chande ameitaka Tume ya
Kurekebisha Sheria Tanzania kuharakisha mchakato wake wa kuandaa ripoti
inayohusu migogoro ya ardhi nchini ili kutoa nafasi ya kufanyiwa marekebisho
Sheria ya Ardhi.
Jaji Chande ametoa kauli hiyo wakati ambao
maeneo mbalimbali nchini yamekumbwa na migogoro mikubwa ya ardhi na kusababisha
wananchi kupoteza mali,mifugo,makazi na wengine
kuuawa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
kuhusu sherehe ya Siku ya Sheria Nchini itakayofanyika Februari 3, mwaka huu,
Jaji Chande amesema, “Ukiondoa idadi kubwa ya kesi za jinai, zinazofuata wa
wingi ni kesi za migogoro ya ardhi, hasa za madai, mfano Mahakama Kuu ya
Tanzania pekee kuna kesi za ardhi zaidi ya 6,000.”
Alisema asilimia 60 ya kesi hizo zinatoka kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya.“Mfumo wa kutatua kesi za ardhi uko chini ya mamlaka tatu. Ngazi ya chini kabisa ni Baraza la Ardhi la Kijiji ambalo lipo chini ya Serikali za Mitaa na Halmashauri. Pili, ni Baraza la Kata,” alisema na kuongeza.
“Na tatu ni Baraza la Ardhi na Nyumba la
wilaya ambalo mamlaka yake ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Baada ya hapo ndiyo kinafuata Kitengo cha Ardhi cha Mahakama Kuu”
alisema.
Alisema tatizo lililopo sasa ni kwamba ili
uweze kutatua migogoro ya ardhi ni lazima uangalie kesi husika ipo katika ngazi
gani na kusisitiza kuwa migogoro mingi ipo katika ngazi za chini ambazo zipo
katika mamlaka nyingine.
“Hivi sasa mfumo wa migogoro ya ardhi na
mashauri ya ardhi unaangaliwa upya na Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo
imetembelea mikoa yote nchini na kukutana na wadau wote ikiwamo, mahakama,
Wizara ya Ardhi, wananchi na wanasheria hivyo ripoti hiyo ikitolewa itasaidia
kuboresha sheria,” alisema.
Mahakama za mwanzo
Akizungumzia mahakama za mwanzo, Jaji Chande
alisema, “Tanzania tuna mahakama za mwanzo 960 lakini zinazofanya kazi ni 803,
kati ya hizo zinazofanya kazi mahakama 487 ndiyo zina mahakimu wa kudumu na
nyingine 316 hutoa huduma kwa kutembelewa na mahakimu mara moja au mbili kwa
wiki kutokana na mahakimu kutoishi maeneo hayo.”
Alisema kwa sasa kuna uhaba wa majengo zaidi
ya 296 ya mahakama za mwanzo, kwamba kuna majengo 157 ya mahakama za mwanzo
ambayo hayafanyi kazi kwa sababu ya uchakavu.
Alisema mahakama hizo zinakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kuwapo katika majengo chakavu na nyingine
zikiwa ndani ya majengo yanayomilikiwa na taasisi mbalimbali na Serikali, jambo
ambalo alisema linazifanya mahakama hizo kuonekana kutokuwa huru
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni