Alhamisi, 30 Januari 2014

ZABUNI ZA VITALU KUFUNGWA MEI-WAZIRI

muhongo 7fc90
Serikali imesema zabuni ya vitalu vya utafiti wa mafuta na gesi asilia vilivyo bahari kuu na ziwa Tanganyika Kaskazini, itafungwa Mei 15, mwaka huu.
Waziri wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo alisema hayo alipofanya mazungumzo na Waziri Mstaafu wa Nishati na Viwanda kutoka Ufaransa, Erick Besson aliyemtembelea ili kufahamu fursa za uwekezaji zilizo katika Sekta za Nishati na Madini akiiwakilisha Kampuni ya GDF Suez ya Ufaransa.
"Kampuni unayoiwakilisha ni kubwa, yenye teknolojia ya kisasa na inafanya uwekezaji mkubwa duniani,"alisema Profesa Muhongo.
Waziri Muhongo alimweleza Besson kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), linamiliki vitalu viwili vya gesi karibu na mpaka wa Msumbiji lakini linahitaji mbia mwenye nia ya dhati watakayeshirikiana naye katika hatua zote za uendelezaji wa vitalu, kwa sababu TPDC bado inakua, alitoa changamoto kwa kampuni hiyo ya GDF Suez kuingia katika ushindani huo.

Katika suala la usimamizi wa bomba la gesi asilia, Profesa Muhongo alimweleza Besson kuwa TPDC pia itahitaji kupata uzoefu na pengine mbia aliyebobea katika usimamizi wa bomba hilo atakayeshirikiana na TPDC katika usimamizi wa bomba la gesi nchini.
Profesa Muhongo alisema Serikali itasambaza gesi katika makazi ya watu ili kupunguza uharibifu wa mazingira huku akitoa mfano kuwa Dar es Salaam pekee inatumia si chini ya magunia 50 ya mkaa kwa siku hivyo gesi itapunguza uharibifu wa mazingira.
Naye Waziri huyo mstaafu kutoka Ufaransa,Besson alimshukuru Profesa Muhongo kwa taarifa nzuri kuhusu fursa za uwekezaji nchini na ameahidi kupata taarifa zaidi za uwekezaji katika mashirika ya TPDC,Stamico na Tanesco ili kuona jinsi kampuni yake itakavyoshirikiana na mashirika hayo katika kuendeleza sekta za Nishati na Madini.
Ugunduzi wa mafuta na gesi umeleta habari njema kwa taifa na wawekezaji. Chanzo: mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni