Jumatano, 23 Aprili 2014

WAZIRI MKUU AONGOZA MAMIA KUMUAGA DC CHANG'A



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Moshi Chang'a, nyumbani kwa marehemu Mbagala Kibonde Maji jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni mkewe Tunu.Picha:Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewaongoza baadhi ya viongozi na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Moshi Chang’a.

Chang'a alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Shughuli za kuuga mwili wa marehemu Chang’a, zilifanyika nyumbani kwake Kibonde Maji Mbagala Wilaya ya Temeke jana na kusafirishwa kwenda Kihesa mkoani Iringa kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika leo.

Akizungumza kabla ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili huo, Pinda alielezea alivyomfahamu Chang’a kwa muda mrefu kwa sababu sehemu kubwa ya utumishi wake amefanya akiwa serikalini.
 
“Ninyi mlimfahamu Chang’a kivingine, lakini mimi nilimfahamu kwa namna ya tofauti kutokana na jinsi alivyokuwa msaada mkubwa kwa serikali kila tulipokuwa tukipata shida ama migogoro ya kiuongozi,” alisema Pinda na kuongeza:

“Kama Tamisemi (Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), tumemtumia sana kusawazisha mambo kwa sababu Mungu alimjalia kipaji cha pekee ambacho ni ucheshi... hata jambo lingekuwa gumu vipi, huyu bwana alijua kufikisha ujumbe bila kumuudhi mhusika kutokana na maneno yake.”

Pinda alifikisha salamu za rambirambi kwa wafiwa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye alisema yuko safarini kikazi.

Vile vile, aliwataka wanafamilia ambao wamebaki bila mama wala baba, wawe na umoja na mshikamano na kuahidi serikali itawasaidia watoto wake wakamilishe malengo ya elimu yao kama ambavyo baba yao alikuwa amepanga.

Marehemu Chang'a ameacha watoto watano, wa kike watatu na wa kiume wawili.

Katika maziko ya marehemu Chang'a, serikali itawasilishwa na Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Hawa Ghasia.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni