Ijumaa, 2 Mei 2014

POLISI MACHINGA WACHAPANA KARIAKOO

Jeshi la Polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) katika Soko Kuu la Kariakoo.
Hamisha hamisha hiyo yenye baraka za uongozi wa mkoa zilianza mapema mwezi uliopita kwa lengo la kuondoa biashara zisizo rasmi katikati ya jiji la Dar es Salaam, pamoja na bodaboda, bidhaa zimwagwazo chini, mama ntilie na vibanda vya vocha.
Majira ya saa tisa alasiri magari ya polisi yaliwasili sokoni hapo huku yakiwa na askari polisi na mgambo waliokuwa wamevaa fulana na kofia za Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), zenye rangi ya njano, na kuanza kuwakamata wamachinga hao.
Askari hao waliokuwa katika magari aina ya Land Rover Defender na Toyota LandCruiser waliuvamia mitaa ya Kongo na Mchikichini kufanya oparesheni hiyo kabla hawajalazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwaondoa walengwa katika eneo hilo.
Hali hiyo ilizua tafrani kwa wateja waliokuwa wakinunua bidhaa kwenye maduka hayo walioenda kwa ajili ya kupata mahitaji yao walikimbia hovyo ili kujiokoa kutokana na vurugu hizo.

Maduka mengi ya mtaa huo, kuanzia kituo cha daladala hadi sokoni, yalilazimika kufungwa kwa hofu ya kupoteza mali kutokana na vibaka wanaotumia nafasi kama hizo kuiba vitu.

Kazi haikuwa rahisi kwa askari hao kwani wamachinga kadhaa hawakuwa tayari kuona wakikamatwa au kupoteza mali zao hivyo kulazimika kupambana kwa kile kilichoonekana kama kuwa radhi ‘kufia mali’ zao. Wamachinga hao waliokaidi amri halali ya jeshi hilo, walikamatwa na kuingizwa kwenye gari la polisi .

Watu walionekana wakikimbia hovyo na wengine wakipanda gari lolote bila kujali linaelekea wapi ili mradi waondoke eneo la tukio kabla hawajapatwa na lolote na kuumia au kuibiwa. “Sisi tutaenda wapi bwana. Acha wafanye mambo yao wakiondoka tunarudi tena kuendelea na biashara zetu,” alisema Hamis Jumanne, anayefanya biashara ya kuuza maji.

Kamanda wa Polisi Mkoa kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa zoezi la kuondoa wamachinga jijini ni endelevu (TK)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni