Libya yaomba msaada wa kimataifa kuzima moto unaochoma mafuta
Tripoli
Serikali ya Libya imeomba msaada wa kimataifa ili kuzima moto mkubwa unaoendelea kuchoma hifadhi ya mafuta mjini Tripoli baada ya makombora ya wapiganaji wa Kiislamu kulipua hifadhi ya takriban lita milioni 6 ya mafuta yaliyosafishwa.
Serikali hiyo changa inayoyumbishwa na mapigano baina ya makundi yanayopinga utawala uliomrithi Kiongozi wa miaka mingi Maummar Gaddaffi aliyeuawa katika mapinduzi ya 2011.
Pipa hilo ni moja ya maghala yanayomilikiwa na kampuni ya kitaifa ya mafuta nchini Libya - Brega
Msemaji wa kampuni hiyo Mohamed Al- Hariri anasema kuwa ikiwa moto huo utasambaa hadi kwenye mapipa mengine yaliyoko karibu basi itakuwa ni janga.
Serikali ya mpito nchini Libya imetaka kusitishwa mapigano ili kuruhusu wazima moto kuendelea na shughuli zao.
Makundi 2 ya wapiganaji yanazozania udhibiti wa uwanja wa ndege mjini Tripoli
Takriban watu 97 wamekufa kufuatia mapigano baina ya makundi hayo hasimu ya waasi wanaotaka kumiliki uwanja wa kimataifa wa ndege wa Tripoli.
Katika mji wa Benghazi mapigano yamechachamaa na kusababisha vifo vya watu 38 siku ya jumapili.
Mataifa kadhaa yameelezea nia yao ya kutuma msaada wa kuzima moto huo lakini wanazongwa na tahadhari iliyotolewa na mataifa ya Magharibi yaliyopelekea kuondoshwa mara moja kwa Wafanyi kazi wao na raia wao nchini Libya wakiongozwa na Marekani iliyofunga Ubalozi wake.
Mwandishi wa BBC mjini Tripoli Rana Jawad amesema kuwa wakaazi wa Tripoli wametahadharishwa kuhama makwao kabla makao yao hayajaghubikwa na moto unaotarajiwa kusambaa iwapo hautadhibitiwa haraka.
Ufaransa ilifuata mkondo wa Marekani ilipoagiza raia wake wote waondoke nchini humo.
Wapiganaji wa LROR wanapigana na Zintan
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni