Takriban wabunge 50 walikurupuka kutoka bunge la waakilishi la Nigeria baada ya mpango wa kujadili mswada unaohusiana na kuagizwa kwa silaha kutoka Afrika Kusini Kupingwa.
Wiki iliyopita, iliripotiwa kuwa maafisa wa serikali walibeba takriban dola 9.3 millioni pesa taslimu wakaenda nazo Afrika Kusini kununua silaha.Naibu spika wa Baraza la waakilishi alisema kwa suala hilo linahusu usalama wa taifa na hivyo haliwezi kujadiliwa hadharani.
Bunge la juu pia liliwaita wakuu wa usalama nchini ili kujadili suala hilo.
Waandishi wa habari nchini Nigeria wanasema kuwa habari hizo zimewashangaza wananchi huku wengi wao wakitoa wito uchunguzi kufanywa ili kuzuia ubadhirifu wa mali ya umma.
Kashfa hiyo iligunduliwa Polisi nchini Afrika Kusini walipowakamata raiya wawili wa Nigeria na Muisraeli mmoja wakiwa na kitita hicho cha pesa zikiwwa kwenye mabegi matatu .
Hata hivyo watatu hao waliowasili Afrika Kusini kwa ndege ya kibinafsi hawakushtakiwa.
Mwandishi wa habari wa BBC ambaye yuko mjini Abuja, Haruna Shehu-Tangaza alisema kuwa wengi wa wabunge waliondoka kwa hasira walikuwa kutoka vyama vya upinzani.
Wabunge hawa walidai kuwa chama tawala cha People's Democratic Party (PDP) ndicho kilipinga mpango huu kupitia naibu wa spika,Emeka Ihiodioha.
Wachambuzi wanasema kuwa huenda Nigeria ikakabiliwa na vikwazo vya ununuzi wa silaha kutoka baadhi ya nchi, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa, kwa sababu ya rekodi yake mbaya ya haki za binadamu.
Kwa muda mrefu wanajeshi wa Nigeria wanaokabiliana na wapiganaji wa kundi la kiislamu la Boko Haram kaskazini mwa taifa hilo wamekuwa wakidai kuwa wapiganaji hao wamejihami kuwazidi wanajeshi.
Aidha kumekuwa na visa kadha vya wanajeshi kutoroka kazi na kukaidi amri kwa sababu hawakuwa wamejihami ipasavyo wakilinganishwa na kundi hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni