Jumanne, 23 Septemba 2014

MHE KESSY ASIPIGWE ILA KIKUBWA APEWE MAJIBU YA HOJA ZAKE


Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Kessy akisisitiza jambo.
Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Kessy wiki iliyopita alilazimika kusindikizwa na askari wa Bunge la Jamhuri kuondoka katika viwanja vya eneo hilo kumnusuru na hasira za wajumbe kutoka Zanzibar waliokerwa na mchango wake kuhusu masuala ya Muungano.
Kessy alisimama bungeni hapo kutoa mchango wake kuhusu Katiba ya Jamhuri akijikita zaidi katika suala la muundo wa Muungano na kusema kwamba Zanzibar inabebwa na Tanganyika.
Nimnukuu: “Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanganyika inabeba mzigo mkubwa ambao haubebeki, hapa tunahudumia wabunge 83 kutoka Zanzibar ambao wanatibiwa wao na wake zao na watoto kwa gharama za Tanganyika wakati hawachangii.”
Aliongeza kuwa haiwezekani kwa Tanganyika kubeba mzigo mkubwa kama huo wakati katika Jimbo lake la Nkasi wananchi wanalia na shida ya maji. Akaendelea kusema kuwa katika kamati yao Namba Moja, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu alitoa semina iliyoonesha kuwa Zanzibar haichangii chochote kwenye Serikali ya Muungano na kuwa hata mishahara wakati mwingine wanategemea Tanganyika.
Kessy alisema wananchi wakilijua jambo hilo, wataikataa katiba inayopendekezwa na kuitupilia mbali kwa kuwa inatoa upendeleo kwa Wazanzibari na kuikandamiza Tanganyika.GPL (P.T)
“Mimi naweza kuwa na wanawake sita, nikazaa nao lakini kila mtoto akawa anaendelea kutunzwa na baba yangu, jambo kama hili halivumiliki hata kidogo japo najua kuwa ukweli unauma,” alisema huku baadhi ya wajumbe wakipaza sauti wengine kumpinga na wengine kuomba mwongozo wa mwenyekiti.
Lakini ninachotaka kusema hapa ni kwamba wananchi wengi wa Tanganyika niliozungumza nao katika utafiti wangu usio rasmi wanaungana na mbunge huyo.
Hapa Dar es Salaam baadhi ya wakazi wanasema iweje Zanzibar yenye watu milioni moja na ushee wawe na wabunge 83 wakati jiji lao lina wakazi zaidi ya milioni nne na lina wabunge wasiozidi kumi?
Alipinga suala la Rais wa Zanzibar kuwa makamu wa rais wa Muungano kwa maelezo kuwa katika mfumo wa vyama vingi jambo kama hilo haliwezekani na kuhoji itakuwaje awe makamu wa kwanza wa rais wakati hajachaguliwa na wananchi wa Tanzania Bara?
Baada ya kauli hiyo, kelele za wajumbe kutoka Zanzibar ziliongezeka baadhi wakisimama na kuwasha vipaza sauti kumshambulia Kessy hivi: “Huyu ni Chizi nini, chizi huyo, hafai kwanza ni Mwarabu,” zilisikika sauti huku nyingine zikimtaka aombe radhi.
Ukweli ni kwamba alichokizungumza Kessy ndizo kero za muungano kwa upande wa Tanganyika. Kati ya watu 50 niliowauliza jijini Dar kuhusiana na kauli hizo, ni wawili tu waliopingana naye, hivyo ni dhahiri kwamba kauli yake inapaswa kutazamwa.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba wachache wakitokea na kutoa wazo ambalo baadaye linaweza kuleta vurugu, ni bora likakubaliwa kama halina madhara. Hivyo hayo ya Kessy yatazamwe na yasipelekwe kisiasa.
Sikuona sababu za wajumbe kutoka Zanzibar kumshambulia Kessy wakati aliyesema hayo ni Gavana wa Benki Kuu, Bwana Ndulu yeye alikuwa akirudia na ndiyo maana akasema hayupo tayari kuomba radhi.
Alidai Ndulu alikuja katika kamati na akasema kwamba tangu kifo cha Abeid Karume (rais wa kwanza wa Zanzibar), Zanzibar hawajawahi kuchangia muungano, hili lilikuwa ndilo la msingi la kulijadili kama ni kweli au ni uzushi na siyo kuzomea na kutaka kumpiga mtoa hoja.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni