Jumanne, 23 Septemba 2014

MKURUGENZI WA ZAMANI WA USALAMA WA TAIFA AFUNGUKA KUHUSU UMUHIMU WA VIJANA KWENYE UASALA WA NCHI


Balozi wa Umoja wa Mataifa, Augustine Maiga, akitoa mada wakati maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani yaliyojadili Nafasi ya Vijana katika Kudumisha Amani yaliyofanyika mkoani Dodoma jana. Kulia ni mtoa mada mwenzake kutoka Baraza la Dini la Kudumisha Amani, Shekh Mohammed Khamis Said. Picha na Silvan Kiwale

NA MAREGESI PAUL, DODOMA

BALOZI wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa, Augustine Mahiga, amesema vijana wa Tanzania ni kati ya wapiganaji wanaounda kundi la kigaidi la Al-Shabaab lililoko nchini Somalia.

Amesema kwamba, yeye binafsi amewahi kuwaona vijana hao nchini humo na kwamba aliwahi kuzungumza nao ili kujua sababu zilizowapeleka katika kundi hilo.

Balozi Mahiga ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini, alitoa taarifa hiyo jana alipokuwa akizungumza na vijana mjini hapa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani.

“Nyinyi vijana ndiyo mtakaoweza kuleta amani na nyie ndiyo wenye jukumu kubwa la kulinda amani yetu.

“Kwa hiyo nawaombeni mlinde amani yetu kwa sababu kama ikitoweka itakuwa vigumu sana kuirejesha na mifano halisi ya maeneo yaliyopoteza amani mnayajua.

“Siku hizi vijana wamekuwa wakijiunga na vikundi vya kigaidi vikiwamo Al-Shabaab kwani wakati nikiwa nchini Somalia, nilishuhudia vijana wa Kitanzania wakishiriki katika kundi hilo.

“Wapo niliozungumza nao nikawauliza wamejiunga huko kwa sababu gani nao wakaniambia wanatafuta maisha. Tena Watanzania wengine niliwashuhudia wakiwa wameuawa, yaani inaumiza sana kuona wenzako wameuawa.

“Siyo kwamba vijana hao wako Al-Shabaab peke yake, wengine wako kule Yemen na tatizo hili si la Tanzania peke yake, ni tatizo la dunia kwani katika makundi ya kigaidi wako pia Wakenya na hata Waganda.

“Hili tatizo la vijana wetu kujiunga huko, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinajua kwamba kuna uandikishaji wa vijana wetu unaendelea ila hapa nilichokifanya ni kuwatonya tu,” alisema Balozi Mahiga.

Katika mazungumzo yake, alizungumzia jinsi hali ilivyo mbaya nchini Somalia na kusema kuwa wakati akifanya kazi za Umoja wa Mataifa nchini humo, alisaidia kuziunganisha pande zilizokuwa zikipingana na pia alisaidia kuundwa kwa Bunge la pamoja na uwepo wa Serikali ya kidemokrasia.

“Vijana msiombe nchi ikakosa amani, wanaopigana vita hawana ubinadamu kabisa, wao hawana muda wa kula, yaani mwenzao mmoja akianguka chini, mwingine anachukua bunduki yake na kusonga mbele.

“Kwa maana hiyo, nawaomba sana muilinde amani yetu, msikubali kutumika kwa namna yoyote kwa sababu amani ikitoweka ni gharama sana kuirudisha,” alisema.

Balozi Mahiga alizitolea mfano nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Liberia na Sieraleone ambazo alisema wananchi wa nchi hizo wanaishi maisha ya shida kwa sababu hakuna amani.

Nyerere na mapinduzi
Pamoja na hayo, alizungumzia jinsi Hayati Mwalimu Nyerere alivyonusurika kupinduliwa kijeshi katika miaka ya 80.

Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, mapinduzi hayo hayakufanikiwa baada ya vijana wawili waliokuwa wakifanya kazi mbili tofauti kutoboa siri ya mkakati huo.

“Kuna jambo sijawahi kulisema popote, lakini sasa ni zaidi ya miaka 30 ngoja leo niliseme.

“Wakati nikiwa Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, kuna kijana mmoja mwenye miaka 25 alikuwa dereva taksi alipata taarifa za watu waliokuwa wakitaka kuipindua Serikali.

“Yule kijana alipopata taarifa hizo, akamwambia mwandishi wa habari wa Daily News ambaye naye alikuwa kijana wa miaka 27. Yule kijana wa Daily News alipopata taraifa hizo, akaniambia, aliponiambia nikaanza kuchunguza ili kujua ukweli wake.

“Kwa bahati nzuri tukafanikiwa kujua ukweli na mwishowe tukawakamata hao waliotaka kupindua Serikali tukawaweka ndani ingawa baadaye walikuja kuachiwa na Rais Mwinyi.

“Kwa kweli hao vijana nitaendelea kuwashukuru na nimeamua kuwaambia hayo kwa sababu nataka mjue umuhimu wa vijana katika ulinzi wa amani nchini,” alisema.

Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), Gustavus Babile, aliwataka vijana kutokuwa tayari kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa kuwa wanahatarisha maisha yao.

Alisema kwamba, kitendo cha vijana kujihusisha na biashara hiyo, kinachafua taswira ya nchi kwa kuwa ripoti za kimataifa zinaonyesha kati ya makosa 50 ya biashara za dawa za kulevya, makosa 30 yanahusisha Watanzania.

Wakati huo huo, Mwakilishi wa Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mohamed Said, aliwataka vijana wajitokeze kwa wingi wakati wa uchaguzi mkuu ujao ili wawachague viongozi bora na kuwakataa viongozi wasiofaa.MTANZANIA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni