Tanzania ni moja ya nchi zinaoongoza kwa mimba na ndoa za utotoni, kwa mujibu wa ripoti inayotarajiwa kuzinduliwa hii leo jijini Dar es Salaam na Shirika la Haki za Binadamu duniani.
Hata hivyo nchi hiyo imepiga marufuku ndoa hizo, ambapo mtoto wa kike anaruhusiwa kuolewa anapofikisha umri wa miaka kumi na nane.Mkoa wa Shinyanga ulio kaskazini magharibi mwa Tanzania ndio unaotajwa kuongoza kwa mimba na ndoa za utotoni, ikilinganishwa na mikoa mingine nchini humo.
Takwimu kutoka mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF zinaonyesha kuwa, kwa siku, watoto 16 wanapachikwa mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa wataalamu, hali hii imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa imezorotesha maendeleo ya mtoto wa kike katika eneo hilo.
Ili kumwokoa mtoto wa kike kutokana na janga hili, kumekuwa na jitihada mbalimbali kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali za kuwaokoa hasa wale ambao tayari wameshatumbukia katika dimbwi hilo.
Shirika lisilo la kiserikali la Agape limeweza kuwaokoa wanafunzi wa kike wapatao mia mbili, wakiwa wamepitia ndoa za utotoni. Wengine tayari wamezalishwa wakiwa na umri chini ya miaka 13. Hivi sasa wanaanza maisha mapya ya kusoma.
Mmoja wa watoto waliokolewa akiwa amejitambulisha kwa jina la Pili Omar, ana miaka 14 na ni mama wa mtoto mmoja. na amekubali kueleza kilichomsibu."Niliolewa kwa sababu wazazi wangu waliniambia sitaendelea kuwa mzigo kwao, hivyo niolewe ili nianzishe mji wangu."anasema Pili.
Wazazi na walezi wa watoto hawa wanalaumiwa kwa kuwalazimisha watoto wao kuingia katika ndoa za utotoni. Licha ya kukithiri kwa ndoa hizo, pia imebainika kwamba asilimia 99 ya ndoa hizo hazidumu. Harieth Kulwa ni mmoja wa waathirika wa ndoa hizi ambaye ndoa yake imevunjika."Nilidhai kuolewa ndio kutatatua matatizo yangu, kumbe nilijiongezea matatizo. Mwanamume aliyenioa kwanza alikuwa mkubwa kwangu, pili alikuwa mlevi…" Anabainisha Harieth.
Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu wanaulalamikia mfumo mzima wa kusimamia sheria kwa kutowachukulia hatua kali za kisheria watu wanaobainika kuwasababishia mimba watoto, wakidai kuwa ni kutokana na vitendo vya rushwa vilivyogubika vyombo vya sheria
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni