Mkurugenzi
wa Serikali za Mitaa Bwn. Khalist Luanda akizungumuza na waandishi
habari juu ya kukamilika kwa maandalizi ua uchaguzi wa Serikali za Mitaa
miji Dodoma leo. Bwn. Khalist Luanda alitangaza rasmi tarehe ya
kujiandikisha na kupiga kura.(Picha na habari kutoka Oya Waziri Mkuu
TAMISEMI)
Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa katika
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa Bwana Kharist
Michael Luanda amesema wananchi wanapaswa kujiandikisha katika daftari
maalum la kupigia kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za
Mitaa kuanzia tarehe 23/11/2014 hadi tarehe 29/11/2014.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa wananchi
wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi za vijiji,
vitongoji na mitaa wanapaswa kuchukua fomu za kugombea kuanzia tarehe
16/11/2014 hadi tarehe 22/11/2014. Akizungumza na waandishi wa habari
mjini Dodoma, Bwana Luanda aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi
katika zoezi la kujiandikisha ili waweze kupata fursa ya kushiriki
katika kupiga kura ili kuwachagua viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa
wanaowataka.
Alisema sifa za mtu anayestahili
kujiandikisha kushiriki uchaguzi huo ni lazima awe raia wa Tanzania,
mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, mkazi wa eneo hilo na mwenye akili
timamu.
Pia alisisitiza kuwa uandikishaji huo
utafanyika katika vituo maalum vilivyoandaliwa ambavyo vipo katika
majengo ya umma, isipokuwa sehemu ambazo hazina majengo hayo,
uandikishaji utafanyika katika vituo maalum kutokana na makubaliano ya
Msaidizi wa Uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa.Bwana Luanda
amesisitiza kuwa vituo hivyo vitafunguliwa saa 1:30 asubuhi na kufungwa
saa 10:30 jioni.
Aidha alisema kuwa vyama vya Siasa
vitaruhusiwa kuweka mawakala wao wakati wa uandikishaji wa wa wapiga
kura lakini gharama za kuwalipa zitakuwa juu ya chama husika. Kuhusu
sifa za mtu anayetaka kugombea nafasi mbalimbali katika ngazi ya
vitongoji, vijiji na mtaa Mkurugenzi huyo alisema kuwa ni lazima awe
mtanzania mwenye umri wa miaka 21 au zaidi na awe mkazi wa kudumu wa
eneo husika.
Vile vile alisema kuwa wasimamizi
wasaidizi wa kila kituo wanapaswa kubandika orodha ya wapiga kura tarehe
30/11/2014, endapo mkazi yeyote au chama cha siasa kitakuwa na
pingamizi au maoni juu ya orodha hiyo basi awasiliane na msimamizi
msaidizi wa uchaguzi ili kuweza kufanyia marekebisho na orodha ya mwisho
itabandikwa siku tatu kabla ya uchaguzi.
Uchaguzi wa serikali za Mitaa
Tanzania Bara umepangwa kufanyika disemba 14, 2014, ambapo wananchi
watawachagua wenyeviti wa vijiji, vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa
Halmashauri za vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa.
Viongozi watakaochaguliwa katika
uchaguzi wa serikali za mitaa ni pamoja na wajumbe wa Halmashauri ya
Kijiji wasiopungua 15 na wasiozidi 25, wenyeviti wa Mitaa na wajumbe wa
kamati za Mitaa wasioziidi 6 na wenyeviti wa vitongoji wa kila
kitongoji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni