Israel: Hatutaki kukoleza mzozo mpakani
Afisa wa Serikali ya Israel amesema nchi hiyo haitaki kuendeleza mvutano
kwenye mpaka wake na Lebanon, baada ya mapambano kati ya jeshi la nchi
hiyo na wanamgambo wa Hezbollah, ambamo wanajeshi wawili wa Israel
waliuawa.
Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, ametoa kauli hiyo katika
mahojiano na Radio ya Israel, baada ya mkutano wa dharura wa maafisa wa
usalama uliofanyika usiku mjini Tel Aviv. Mkutano huo uliodumu kwa saa
kadhaa uliwahusisha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, waziri wa ulinzi
Moshe Yaalon na kamanda mkuu wa jeshi la Israel Benny Gantz.Ulifuatia shambulizi lililofanywa na kundi la Hezbollah la nchini Lebanon dhidi ya msafara wa jeshi la Israel, ndani ya eneo la mpaka ambalo Lebanon inasema Israel inalikalia kimabavu. Shambulizi hilo la Hezbollah liliwauwa wanajeshi wawili wa Israel wenye vyeo vya Kapteni na Sajenti, na kuwajeruhi wengine saba, hii ikiwa ni kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Israel Peter Lerner.
Hezbollah ilikiri kufanya shambulizi, ambalo lilijibiwa na Israel kwa mizinga na mashambulizi ya anga.
Netanyahu aonya kuhusu adhabu chungu
Awali, Netanyahu alikuwa amesema waliolishambulia jeshi la nchi yake watalipa kwa gharama kubwa.
'Kwa wakati huu ljeshi letu linashughulikia matukio kwenye mpaka wa kaskazini. Yeyote anayefikiria kutuchokoza kwenye mpaka huo, namshauri azingatie kilichotokea Gaza. Hamas ilipata kipigo kikubwa zaidi tangu kuundwa kwake, na jeshi letu liko tayari kujibu kwa nguvu kwenye mipaka yote''. Amesema Netanyahu.
Makabiliano haya yamekuja siku kumi baada ya mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na Israel kuwauwa wapiganaji sita wa Hezbollah katika milima ya Golan siku kumi zilizopita.
Mwanajeshi wa kulinda amani auawa
Mbali na wanajeshi wa Israel waliouawa au kujeruhiwa, mwanajeshi raia wa Uhispania ambaye alikuwa katika ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo, pia alipigwa risasi na kuuawa.
Balozi wa Uhispania kwenye Umoja wa Mataifa Roman Oyarzun Marchesi, amewaambia waandishi wa habri mjini New York, kuwa risasi iliyomuuwa mhispania huyo ilitoka upande wa Israel.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha dharura kuujadili mzozo huo, na rais wake wa sasa Cristian Barros Melet ambaye ni balozi wa Chile, amesema baraza hilo linalaani vikali shambulizi hilo lililomuuwa mwanajeshi wa kulinda amani.
Hata hivyo, licha ya karipio hilo kutoka baraza la usalama na katibu mkuu wa umoja wa mataifa mwenyewe, Ban Ki-moon, hakuna aliyethibitisha upande uliomuuwa mwanajeshi huyo.
Stephane Dujarric ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema katibu mkuu huyo amesononeshwa na kuzorota kwa usalama kwenye mpaka baina ya Israel na Lebanon, na kuzitaka pande zote zinazohusika kuendeleza utulivu, na kuonyesha stahamala.
Hali hiyo ya mvutano imezifanya nchi hizo mbili kuzifunga shule zilizo karibu na mpaka, huku wakazi wa maeneo ya karibu na mpaka huo wakisema wamesikia milio milio ya silaha nzito
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni