Kufuatia mvua kubwa zilizonyesha usiku wa
tarehe 04 Machi, 2015 Wilayani Kahama mafuriko makubwa yalitokea na
kuathiri wakazi wa kata ya Mwakata katika vijiji vya Mwakata, Numbi na
Mwaguguma. Kutokana na mafuriko yaliyotokea tathmini ya awali inaonesha
kuwa watu 42 wamepoteza maisha, watu 82 wamejeruhiwa na watu
wanaokadiriwa kufikia 574 wameathirika. Jumla ya nyumba 137 zimeathirika
kwa viwango mbalimbali.
Serikali imechukua hatua za haraka kwa
kushirikiana na wananchi kuwafikia na kuwanusuru waathirika wa mafuriko
hayo waliokuwa wamezingirwa na mafuriko. Aidha vimeanzishwa vituo vya
muda kuwahifadhi wananchi hao kwenye Shule.
Serikali imepeleka misaada ya kibinadamu kama ifuatavyo;
i. Chakula tani 20. Maharage tani 5, Mafuta ya kupikia lita 1,126 na Sukari tani 1.3
ii. Vifaa vya matumizi ya ndani ambayo
vinajumuisha blanketi 650, ndoo 82 za lita 20, ndoo 82 za lita 10 ;
Vifaa vya kupikia seti 82 na madumu 82
Kwa kuwa bado Serikali inalo jukumu kubwa
la kuwawezesha waathirika kurejea katika maisha yao ya kawaida;
inapenda kuwatangazia wale wote wanaoguswa na maafa haya kuwa Serikali
inaendelea kupokea misaada mbalimbali ambayo inahitajika kwa waathirika.
Mahitaji haya ni pamoja na sare za shule;
daftari za wanafunzi; mavazi ya kike na kiume; na chakula. Aidha kwa
kuzingatia kuwa waathirika hawa wamepoteza mali na fedha katika maafa
haya; misaada ya vifaa vya ujenzi (sementi, mabati, mbao, n.k.)
inahitajika sana.
Utaratibu wa kupokea misaada hiyo kwa
walio Dar es Salaam wanaweza kuiwasilisha misaada hiyo Idara ya Kuratibu
Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu au kuwasiliana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga.
Serikali itaendelea kuwasaidia Waathirika
dhidi ya Changamoto zinazoweza kujitokeza hususani za kiafya
zinazosababishwa na uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira. Elimu juu
ya ujenzi wa nyumba bora na makazi maeneo salama itaendelea kutolewa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni