Ugiriki imesema kama taifa hilo litakuwa kwenye hatua ya kuondoka katika
kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro, basi mataifa ya Uhispania
na Italia yanaweza kufuata mkondo huo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ulinzi wa Ugiriki, Panos Kammenos,
wakati akizungumza na gazeti la Ujerumani la Bild, katika mahojiano
ambayo yatachapishwa leo Jumamosi (14.03.2015). Kammenos amesema kama
Ugiriki ikiondoka kwenye kanda inayotumia sarafu ya Euro, basi Uhispania
na Italia zitafuata, na hata ikiwezekana Ujerumani pia.Amesema hivyo wanahitaji kutafuta njia ndani ya kanda inayotumia sarafu ya Euro, lakini njia iliyopo sasa haiwezi kuwalazimisha Wagiriki kuendelea kulipa deni lao. Aidha, amesema Ugiriki haiitaji mkopo mwingine wa tatu zaidi ya kupewa punguzo kama lile walilopewa Ujerumani katika mkutano wa madeni uliiofanyika mjini London mwaka 1953.
Kauli hiyo ameitoa siku chache baada ya Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble kutamka hadharani kwamba Ugiriki huenda ikatoka kweye kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya, kwa sababu viongozi wake wameshindwa kufikia maafikiano juu ya mikopo mpya.
Ujerumani na Ugiriki zimejiingiza katika vita vya maneno na Ugiriki ilishafanya mgomo rasmi kwa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani, ikimshutumu Waziri Schaeuble kwa mtukana waziri mwenzake wa Ugiriki, Yanis Varoufakis kama mtu ''mshamba na asiyejua chochote'', kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya Ugiriki. Hata hivyo, Schaeuble amekanusha shutuma hizo.
Juncker azitahadharisha nchi za Umoja wa Ulaya
Ama kwa upande mwingine, Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker ametoa kauli ya tahadhari kwa serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, huku akitaka mshikamano na Ugiriki kuinusuru isifilisike na kuhatarisha kutolewa katika kanda ya sarafu ya euro.
Uhusiano kati ya Ujerumani na Ugiriki tayari ulishaingia dosari kutokana na msimamo wa Ujerumani kuhusu mzozo wa deni la Ugiriki. Kammenos ameishutumu Ujerumani kwa kuingilia mambo ya ndani ya Ugiriki, akisema kuwa anahisi Ujerumani inataka kuiondoa nchi yake katika kanda inayotumia sarafu ya Euro.
Aidha, wakati Juncker amekutana na Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras, Schaeuble ameionya Ugiriki isitegemee kupokea hundi iliyowazi. Matamshi hayo ameyatoa wakati ambapo mazungumzo kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake ambao ni Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, yanaendelea mjini Brussels, kwa lengo la kuendelea kuibakiza Ugiriki katika kanda ya mataifa yanayotumia sarafu ya Euro.
Msemaji wa wizara ya fedha ya Ujerumani, Friederike von Tiesenhausen, amesema nchi yake haitaki kuona Ugiriki inaondoka kwenye kanda inayotumia sarafu ya Euro, lakini pia ni muhimu kutambua kuwa nchi hiyo haitapatiwa hundi iliyowazi.
Wakopeshaji wa kimataifa wanaitaka Ugiriki ifanye mageuzi kadhaa ya kiuchumi ili nchi hiyo iweze kupatiwa msaada wa Euro bilioni 7.2 ambazo bado zimebakia katika madeni ya kimataifa. Ili kuepuka makosa yasitokee, Ugiriki imepokea awamu mbili za mkopo huo wa dharura, huku kila mmoja ukiwa na jumla ya Euro bilioni 240, tangu mwaka 2010
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni