Jumatano, 27 Mei 2015
FOLENI YA IKULU INATISHA
Dar/Mbeya. Ni dhahiri sasa kuwa hatua ya vikao vya juu vya CCM kuwafungulia makada wake waliokuwa wamefungiwa kwa kuanza kampeni mapema na kutangaza tarehe za kuanza kuchukua fomu, vimechochea harakati za kusaka urais na kuongeza urefu wa foleni ya wanaotaka kuelekea Ikulu kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yamejitokeza ndani ya siku nne baada ya uamuzi huo wa CCM kutangazwa mjini Dodoma na kuwafanya makada wake, kuanza kujitokeza hadharani wakiweka bayana tarehe za kutangaza nia hiyo.
WanaCCM waliojitokeza ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo ambao kwa nyakati tofauti wamethibitisha kuwa wanatangaza nia hiyo wiki ijayo.
Wakati Makongoro akisema sasa anajisikia kuomba kazi ya urais na anatarajia kutangaza nia hiyo kabla ya Juni 3, Profesa Muhongo ameahidi kufanya hivyo kati ya Mei 31 na Juni 3, huku Profesa Mwandosya akisema ataweka wazi kila kitu Jumatatu ijayo. Tarehe ya kuanza kuchukua fomu kwa chama hicho ni Juni 3 na kurejesha ni Julai 2.
Kuingia ulingoni kwa makada hao ambao kwa muda mrefu hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, kunaongeza orodha ya makada waliokwishajipanga kwenye foleni hiyo akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anayetarajia kutangaza kile anachoita ‘safari ya matumaini’ Jumamosi mjini Arusha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliyetangaza nia hiyo juzi, akifafanua kuwa atafanya hivyo hivi karibuni huko Mtama, Lindi alikozaliwa.
Pia wamo, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira aliyekwishaeleza nia hiyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliyejiuzulu unaibu Katibu Mkuu wa CCM Jumapili ili aweze kuwania urais bila mgongano wa masilahi katika vikao vya chama hicho, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum Ali.
Katika mlolongo huo wapo makada waliokuwa wanatajwa muda mrefu ambao wanasubiriwa kuweka bayana azma yao ambao ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kauli ya Makongoro
Akiwa mjini Mbeya juzi, mbunge huyo wa Afrika Mashariki alisema: “Najisikia kuomba kazi ya kuwaongoza Watanzania katika ngazi ya juu ya uongozi, kwani uwezo ninao, afya na muda wa kufanya hivyo vinaniruhusu.”
Makongoro alisema hayo wakati akitoa shukrani kwa viongozi wa dini baada ya kumkabidhi Tuzo ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa niaba ya familia, ikiwa ni ishara ya kuenzi na kukumbuka kazi alizofanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake.
Awali, viongozi wa dini na machifu walioshiriki hafla hiyo, walimtaka Makongoro ‘kuvunja ukimya kuhusu tetesi’ zinazosambazwa kupitia vyombo vya habari juu yake kuhusu kuwania urais na kumtaka atamke wazi juzi hilo kwa kuwa wako tayari kumsaidia katika harakati zake.
Kiongozi wa machifu wa Busokelo, Prince Mwaihojo alisema wananchi wa Mbeya wana imani kubwa na familia ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa mwasisi huyo wa Taifa alikuwa akitangaza mambo mazito akiwa mkoani hapo.
Mwaihojo alisema wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alizungumza jinsi rushwa inavyoitafuna nchi na umuhimu wa michezo kwa nyakati tofauti.
“Wazee wanasema watakusaidia katika harakati zako za kisiasa na mambo mengine, lakini ni muda mrefu wamekuwa wakisikia tu kwenye vyombo vya habari, hivyo wanataka uweke wazi suala hili ukiwa mkoani Mbeya, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere kuzungumzia masuala nyeti akiwa hapa (Mbeya),” alisema Mwaihojo.
Askofu wa Makanisa ya Pentecostal Assemblies of God mkoani Mbeya, Damiano Kongoro alisema Taifa linatakiwa kuongozwa na mtu anayejua kwamba nchi ni maskini ndani ya utajiri uliotukuka ambaye atawaondoa Watanzania katika hali hiyo, mwenye kufuata maadili na misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere.
Hata hivyo, Makongoro aliwaambia viongozi hao kwamba asingeweza kutamka chochote juu ya minong’ono hiyo katika hafla inayomhusu baba yake, Mwalimu Nyerere.
“Nimewasikia wazee wangu waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere na viongozi wa dini hapa, mlichosema nimewaelewa ila hapa siyo mahala sahihi pa kuzungumzia suala hili, tumekuja kupokea nishani ya kumuenzi Mwalimu Nyerere.
“Ila najisikia kuomba kura za kazi za kuwaongoza wananchi kwani nina afya nzuri, uwezo ninao na ni muda mwafaka kabisa lakini siku mbili kabla ya tarehe 3 Juni nitakutana na wanahabari kulizungumzia jambo hili,” alisema Makongoro.
Alisema anakumbuka baba yake alivyokataa kumbeba mwaka 1995 wakati akitaka kugombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini na kwamba ndiyo maana anasita kutamka mambo makubwa kwenye hafla hiyo.
“Baada ya kuona ile ngoma kwenye CCM imedunda, nikasema ngoja nijaribu kumweleza baba nigombee kupitia chama cha upinzani, hapo nilitegemea kupata jibu tofauti, lakini akaniuliza nagombea kwa chama kipi, nikamwambia NCCR-Mageuzi, akasema hapo safi na kunisisitizia nikiingia huko nikamsaidie sana (Augustine) Mrema,” alisema Makongoro. Mrema, alikuwa mwenyekiti wa chama hicho wakati huo.
Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Sabina Gereja akizungumza katika hafla hiyo, alisema umefika wakati wa Watanzania kuienzi familia ya Nyerere ambayo iliishi katika maisha ya kawaida enzi za uongozi wake.
Alisema kuna haja kwa Serikali nayo kuhakikisha inaendelea kuwaenzi wanafamilia hiyo wanaoongozwa na Mama Maria Nyerere.
Profesa Mwandosya
Jana, Profesa Mwandosya alisema amepanga kuzungumza na vyombo vya habari, Juni Mosi jijini Mbeya, pamoja na mambo mengine, juu ya mbio zake za urais.
Pamoja na Profesa Mwandosya kutoingia kwa undani kuhusu suala hilo, alipoulizwa iwapo siku hiyo atatangaza nia, alisema mambo hayo na mengine yote yatajulikana siku hiyo.
Mmoja wa watu walio katika kamati ya maandalizi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema upo uwezekano waziri huyo akatamka suala la kuwania urais.
“Hadi sasa maandalizi ni mazuri, tunatarajia kufanya shughuli hii na Profesa Mwandosya atazungumza na wananchi, waandishi wa habari na wanachama wa CCM na kueleza mipango yake na vipaumbele iwapo atafanikiwa katika safari yake hiyo,” alisema.
Profesa Muhongo
Hatimaye minong’ono imekuwa kweli baada ya Profesa Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, kujitosa katika kinyang’anyiro hicho akipanga kutangaza nia kati ya Mei 31 na Juni, 3.
Profesa Muhongo aliliambia gazeti hili kwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kuwa atatoa tamko lake juu ya “Tanzania ijayo (2015 - 2025)” kabla ya kuchukua fomu na kuwaomba makada wa CCM kujitokeza kumdhamini muda ukiwadia.
Kabla ya uthibitisho huo, kulikuwa na taarifa zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii ya Whatsapp, Twitter na Facebook, kuwa mtaalamu huyo wa jiolojia ataweka bayana safari yake mpya ya kutafuta cheo cha juu zaidi nchini.
Alipotakiwa kuthibitisha ukweli wa ujumbe huo, alijibu kifupi: “Ndiyo. Ni kweli. SM.”
Hata hivyo, Profesa Muhongo hakuweka bayana eneo atakalotolea tamko
MWANANCHI
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni