WAZIRI
wa zamani wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo, ametangaza nia rasmi
ya kuwaomba Wana CCM kumteua kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mwezi Oktoba, huku akisema ni yeye pekee mwenye uwezo wa
kuikwamua nchi katika hali mbaya ya umasikini na ukosefu wa wataalamu,
hali inayoifanya nchi ishindwe kupiga hatua.
Pamoja
na mambo mengine, Muhongo alitumia muda mwingi kutoa takwimu hali ya
umasikini na utajiri kwa wananchi wa Tanzania, bila kusahau baadhi ya
nchi ambazo zimeweza kupiga hatua kubwa kwa kujikita kwenye kuzalisha
wataalamu na watafiti, akiwamo yeye, ambaye si tu ni Profesa, bali pia
amebobea kwenye nishati kwa miaka mingi.
Akizungumza
kwa kujiamini mbele ya wanachama wa CCM na Watanzania katika Ukumbi wa
Chuo Kikuu Huria, Musoma Mjini, Profesa Muhongo alisema kwamba anayo
tiba ya umasikini wa Watanzania kwa kuhakikisha kwamba anatumia utaalamu
wake kwa kusimamia mambo ya gesi, mafuta, umeme, bila kusahau elimu kwa
ajili ya kuwakwamua wananchi wake.
“Nchi
ina upungufu mkubwa wa takwimu hali inayowafanya viongozi washindwe
kujua namna gani wanaweza kuondoa umasikini na kero zinazowakumba
wananchi wake, hivyo hata wale wanaosema wanataka uongozi, hawajui
wangapi wenye uhitaji.
“Ukiacha
takwimu ambayo kwa Dunia ya sasa ni lazima, nchi yetu lazima ijiamini,
kuongeza ushindani, kuongeza upendo, bila kusahau rushwa ambayo kwa
uhakika inapaswa kupigwa vita kwa vitendo ili nchi yetu isonge mbele,”
alisema Muhongo.
Kuhusu
uchumi, Profesa Muhongo alisema kwamba ni aibu Tanzania kupitwa
kiuchumi na Mataifa waliyokuwa nayo sawa, akitolea mfano wan chi za
Brazil, China, India na Kenya ambao wao wamewekeza kwa kiasi kikubwa
kwenye elimu na utafiti.
Alisema
nchi ikiwa na watafiti, wananchi wao hawataishi kwa mashaka, huku
akisema endapo atapitishwa kuwania nafasi hiyo na kuwa rais wa Tanzania,
atahakikisha kwamba anakuza uchumi wan chi kutoka asilimia 7.5 hadi
asilimia 10 na 15 kwa kipindi cha miaka mitano hadi 10 ya urais wake.
“Nimeweza
kufanya kazi ya gesi na mafuta kwa miaka kadhaa kwenye nchi mbalimbali,
hivyo hakika kama chaguo ni wataalamu, basi mimi nastahili kwa sababu
sioni mwingine mwenye uwezo wa kutangaza kuondoa kero za Watanzania na
jinsi atakavyoziondoa.
“Ndio
unaweza kusema utaondoa umasikini kwa wananchi au kuongeza mishahara,
lakini ili hilo liweze kufanikiwa kwa vitendo, ni lazima pia katika
kipindi cha uongozi wako uweze kukuza uchumi wako kwa kiasi kikubwa,
bila hivyo hakuna kitu,” alisema Muhongo.
Aidha
Profesa Muhongo alisema kwamba Duniani kote nchi zimepiga hatua kwa
kuwekeza kwenye wataalamu na viwanda, hivyo Tanzania inapaswa kuangalia
namna ya kuwekeza kwenye sekta hizo, bila kusahau sekta ya elimu yenye
umuhimu mkubwa.
Katika
hatua nyingine, Profesa Muhongo alisema kwamba akiwa Waziri wa Nishati
na Madini, ndio mtu ambaye alifanikiwa kwa vitendo kutekeleza ilani ya
CCM kwa kuhakikisha kwamba vijiji vingi vinapata umeme kwa kuongeza
bajeti na kusimamia kwa vitendo wakala wa umeme vijijini (REA).
Alisema
kusudio la kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaendelea kupata umeme
kwa bei nafuu ni kati ya mambo anayoona yanafaa kuongezewa chapuo na
usimamizi wa aina yake, hivyo mwenye uwezo wa kulitatua hilo ni yeye.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni