Shambulio
la kigaidi lililofanyika katika mji wa Sousse ulio katika pwani ya
Tunisia Ijumaa iliyopita lilisababisha vifo vya watu 39 ambao walikuwa
watalii nchini humo. Imethibitika kuwa raia thelathini wa Uingereza ni
miongoni mwa watu waliouawa na mtu mwenye silaha katika eneo la watalii
nchini Tunisia.
Waathirika wa shambulio hilo ni pamoja na watu wa vizazi vitatu vya familia moja. Uchunguzi wa kimataifa umeanza katika shambulio la Sousse, ambalo lilitekelezwa na mhitimu wa chuo kikuu akihusishwa na kundi la wapiganaji wa Islamic State. Zaidi ya maafisa wa polisi na wafanyakazi wengine mia sita wa Uingereza wanashiriki katika uchunguzi huo-- moja ya operesheni kubwa kuliko zote za kukabiliana na ugaidi tangu mashambulio ya London ya mwaka 2005. Serikali ya Tunisia imesema kwa sasa wanaelewa kuwa mtu huyo mwenye silaha, Seifeddine Rezgui alikuwa na wenzake waliompatia bunduki ya Kalashnikov na kumpeleka katika eneo hilo la watali.
Ijumaa, siku kumi kabla ya kuadhimisha miaka kumi kukumbuka shambulio katika mfumo wa usafiri wa London, ambapo watu 52 waliuawa, mwanafunzi Seifeddine Rezgui akiwa amebeba bunduki aina ya Andre Kalashnikov (AK 47) alianza kuwafyatulia risasi ovyo watalii waliokuwa wakiotea jua.
Baba yake amezungumzia kitendo hicho kuwa ni cha aibu na ameomba radhi kutokana na kitendo cha mwanaye mwenye umri wa miaka 23, akisema habari ya tukio hilo ni ngumu kwake kueleweka. Hakim Rezgui baba wa mtu mwenye silaha amenukuliwa akisema kwa uchungu "Mungu wangu, nimeshtushwa. Sifahamu ni nani waliwasiliana, kumshawishi au mtu aliyepandikiza mawazo haya ndani ya kichwa chake. Alikuwa na marafiki wapya ambao wamemwingiza katika uhalifu huu.Ameongeza kusema: "Mtoto wangu hakuwa na tatizo na mtu yeyote. Lakini sifahamu aliyembadilisha akili yake, kumshawishi na ambaye amempandikiza akili ya mauaji."Bwana Rezgui ameendelea kuomboleza kwa kusema: "Natamani kusingekuwa na waathirika wa shambulio hili, asidhurike mtu yeyote. Natamani lisingetokea hili. Kwa sababu ninapowaangalia waathirika nafikiria wangelikuwa watoto wangu mwenyewe. Sina wazo lolote na kwa kweli nasikitika sana. Nimesononeka kuwaona waathirika hao. Naelewa uchungu mkubwa wa kupoteza familia. Nahisi kama nimekufa pamoja na waathirika wa kitendo hicho."Ni aibu kubwa kwangu, mama yake na kwa familia yote."
Tangu shambulio hilo video zimeibuka na picha ya Rezgui - akiwa miguu peku na akiwa amevalia fulana nyeusi na kaptula akifyatua bunduki na kukimbia ufukweni mwa pwani ya Sousse. Picha nyingine za video zinamwonyesha Rezgui akicheza dansi na ameripotiwa kuwa anafahamika kwa kushiriki mashindano ya uchezaji dansi katika mji mkuu wa Tunis.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni