Ndege aina ya Super Bat DA-50
Na Daniel Mbega, Mkomazi
NI majira
ya saa tatu asubuhi Jumatano, Septemba 16, 2015 wakati tunawasili kwenye uwanja
mdogo wa ndege (air strip) katika eneo la Kisima ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Mkomazi inayotenganisha mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Uwanja unaonekana
mweupe, hakuna ndege! Nikashangaa kwa sababu wenyeji wetu kampuni ya Bathawk
Recon wametuambia tunakuja kushuhudia uzinduzi wa ndege maalum zinazopambana na
ujangili.
Kilichoonekana
mbele yetu ni hema kubwa ambalo mbele yake kulionekana minara midogo
iliyosimikwa kama fimbo. Kwenye banda kubwa ikaonekana ndege ndogo aina ya Twin
otter. Nikadhani ndiyo inayozinduliwa, lakini Idrisa Jaffary, mwenyei wetu
tuliyekuwa naye kwenye gari akasema, hapa siyo hiyo.
Mshangao ukanipata
baada ya gari kusimama wakati nilipokiona kifaa mfano wa ndege kikiwa
kimeegeshwa kwenye bomba maalum kana kwamba ndege inataka kupaa.
Kwa siku
za karibuni zimekuwa maarufu kwani zinatumika kupeleka misaada mbalimbali hata
katika maeneo hatari ya vita ambako hakufikiki kirahisi.
“Hii ndiyo
ndege yenyewe,” Idrisa akatueleza. “Hee! Ndiyo hii?” tukajiuliza kwa mshangao. Kwamba
Tanzania tumeanza kuitumia teknoloia hii yanaweza kuwa maendeleo mengine mapya.
Mshangao
wetu ulimalizika wakati Phil Jones, ofisa mwendeshaji wa mitambo hiyo kutoka
kampuni ya MartinUAV ya Marekani iliyotengeneza ndege hiyo aina ya Super Bat DA-50 UAV, alipoanza kutuelezea namna ‘ndege’hiyo (drone)
inavyofanya kazi huku akituonyesha kila sehemu na kazi yake.
“Hii ni ndege ambayo haihitaji kuwa na
rubani, inaongozwa kwa kompyuta maalum, ina antenna mbili, ina kamera maalum
ambazo zinaweza kupiga picha usiku na hata mchana,” akatueleza.
Akasema ndege hiyo ina uwezo wa kuruka
urefu wa futi 20,000 kutoka usawa wa bahari na kwenda katika nusu kipenyo cha
kilometa 35 kutoka ilipo mitambo ya kuiongoza.
Jones, ambaye baadaye alinieleza kwamba
yeye rubani wa zamani wa ndege za kijeshi katika Jeshi la Uingereza aliyestaafu
mwaka 2014 ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, akasema ndege hiyo
inayorushwa kwa mtindo wa manati (catapult
launch system), inaweza kuruka mfululizo kwa muda wa saa 10 ikiwa angani
kabla ya kutua na kujazwa mafuta tena.
“Ina mfumo maalum wa kamera ambazo zina
uwezo wa kupiga picha hata usiku wa manane na kutambua mienendo ya viumbe wenye
damu ya moto kama hayawani na binadamu, hivyo ni rahisi kubaini kama kuna
majangili,” akafafanua.
Baada ya maelezo ya takriban nusu saa, hatimaye yeye na wasaidizi wake
wakaamua kuirusha ndege hiyo baada ya kuiwasha. Ilichomoka kwa kasi ya ajabu na
kuelekea angani ikaanza kuzunguka.
Hapo ndipo tukasogezwa kwenye hema kubwa ambako tuliwakuta wasaidizi
wake – Austin Howard na Kory Ferguson – wakiendesha kompyuta hizo na
tukashuhudia mazingira halisi ya hifadhi katika eneo husika pamoja na kuona
wanyama mbalimbali.
“Sasa hapa unaweza kuona kama kuna wavamizi (majangili) na inakuwa
rahisi kuwasiliana na askari wa wanyama pori na kwenda kwenye eneo husika
kuwakamata,” anasema Jones.
Hata ilipotua, ilikuja kama ndege za kawaida zinavyokuja, tofauti yake
tu yenyewe haina magurudumu. Naam, unaweza kuwa ufumbuzi mwingine wa kupambana
na ujangili nchini, tatizo ambalo haliko Tanzania tu, bali katika nchi nyingi
barani Afrika.
Taasisi mbalimbali za ndani na nje zikiwemo serikali za mataifa makubwa zimekuwa
zikijitahidi kusaidia mapambano hayo kama alivyofanya Rais Barack Obama wa
Marekani alipoahidi kutoa Dola milioni 10 (sawa za Shs. 20 bilioni) ili
kuimarisha mapambano hayo nchini.
Takwimu zinaonyesha kuwa Bara la Afrika
mwaka 1930 lilikuwa na tembo 50 milioni na kwamba hadi kufikia mwaka 2013 tembo
waliobakia katika bara zima ni 500,000.
Aidha, takwimu hizo zinaonyesha kwamba
katika miaka ya 1960 Tanzania kulikuwa na tembo kati ya 250,000 hadi 300,000 na
kwamba wanyama hao walipungua hadi kufikia 130,000 mwaka 2002 na idadi ya tembo
hapa nchini imeendelea kupungua kwa kasi ambapo hivi sasa takwimu zinaonyesha
kuwa inakadiriwa kuna tembo wasiozidi 55,000.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wastani wa tembo 30 huuawa kijangili
kila siku ikiwa ni sawa na tembo 850 kwa mwezina zaidi ya tembo 10,000 wanauawa
kila mwaka,hali ambayo inatishia uwepo wa wanyama hao wakubwa zaidi duniani kwa
sasa.
Kwenye Hifadhi ya Tarangire, jumla ya tembo 104 waliouawa katika kipindi
cha miaka mitatu tu kutoka mwaka 2007 hadi 2009 na katika Hifadhi ya Serengeti
idadi ya tembo imepongua kutoka 2,500 mwaka 1985 hadi kufikia 500 mwaka 2012
huku nyati wakipungua kutoka 70,000 hadi 40,000 ujangili huo ukiua faru wengi
kutoka 1,000 waliokuwepo mwaka 1985 hadi 20 tu.
Kwenye Pori la Akiba la
akiba la Selous inaelezwa kwamba hadi kufikia mwaka 2007 kulikuwa na tembo
zaidi ya 70,000 lakini idadi hiyo imeshuka hadi tembo 30,000 tu kufikia mwaka
2012.
Kasi ya ujangili inayoongezeka kila mwaka
inachangiwa na mambo mbalimbali yakiwemo kukua kwa uchumi wa nchi ya China na
nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa Asia kama Hong Kong, Vietnam na Philippines.
Juhudi mbalimbali
zimefanywa na wadau wa sekta ya utalii na maliasili, lakini inaoenakana tatizo
hilo linazidi kuota mizizi huku taasisi za kimataifa zikiendelea kulipigia
kelele bila mafanikio.
Kampuni ya Bathawk Recon Limited ya Tanzania
imeitikia kwa vitendo mapambano ya vita dhidi ya ujangili nchini, ambapo leo
hii Septemba 16, 2015 ikaamua kuzindua ndege hizo maalum zinazoweza kupambana
na ujangili.
“Haya
ni majaribio ya tatu, tulifanya majaribio mara ya kwanza katika Hifadhi ya
Taifa ya Tarangire kwa kutumia ndege maalum aina ya DT 16, lakini hayakuonyesha
matokeo mazuri,” anasema Michael Chambers, Mkurugenzi wa Mikakati na
Mawasiliano wa Bathawk.
Chambers, ambaye amekuwepo nchini Tanzania
kwa takriban miaka 20 sasa, anasema jaribio la pili lilifanyika katika Pori la
Selous mwezi Mei 2015 kwa kutumia ndege aina ya DT 26 iliyotengenezwa Ufaransa,
lakini iliharibika na haikuweza kutoa matokeo mazuri.
Anaibainisha kwamba, katika kipindi cha
siku tano cha majaribio tangu Septemba 11, 2015, ndege hiyo mpya aina ya Super
Bat DA-50 UAV iliyotengenezwa na kampuni ya MartinUAV ya Marekani, imeonyesha
mafanikio makubwa.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi na muasisi
wa kampuni hiyo, Tom Lithgow, anasema baada ya majaribio yao kuonyesha
mafanikio, sasa wataandaa ripoti yao na kuiwasilisha kwenye taasisi ya Tanzania
Private Sector Foundation (TPSF) pamoja na kwenye Shirika la Hifadhi za Taifa
(Tanapa) ili kama wataridhia, basi waweze kuona namna gani yakuanza utekelezaji
kuhakikisha tembo na wanyama wengine wanalindwa.
“Tumefanya kazi kwa ushirikiano na Serikali
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, hususan Tanapa na Idara ya Wanyamapori,
tunaamini baada ya mafanikio haya, nao wataangalia ni kwa namna gani tunaweza
kuanza kuitumia,” anasema Tom, Mtanzania ambaye ana uzoefu mkubwa wa mazingira
ya porini na utalii kwa ujumla.
Hata hivyo, Mike Chambers anasema,
teknolojia hiyo itakuwa ya kwanza kutumia nchini Tanzania katika suala zima la
kubaini na kudhibiti ujangili na ni ya gharama nafuu zaidi kwani ndege hizo
hazitumii rubani ndani yake, zinatumia mafuta kidogo na kuruka kwa muda mrefu.
“Mbali ya kupambana na ujangili, lakini pia
teknolojia hii itasaidia suala zima la uhifadhi kwa kutambua hata idadi ya
wanyama waliopo (scouting),” anafafanua Chambers.
Herman van Rooyen na Johnson Makere ni
vijana waliohitimu stashahada ya Uhifadhi Wanyamapori katika Chuo cha
Wanyamapori cha Mweka mkoani Kilimanjaro, ambao kwa sasa wameelekezwa namna ya
kurusha na kuongoza ndege hizo kwa ustadi mkubwa.
Ingawa wanatakiwa kupatiwa mafunzo maalum
na muhimu, lakini wanaielezea teknolojia hiyo kwamba inafaa sana katika suala
zima la uhifadhi wanyamapori.
Wanasema, kutokana na tatizo la uhaba wa
watumishi na vitendea kazi pamoja na miundombinu duni ndani ya hifadhi na
mapori ya akiba, teknolojia hiyo inaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa ikiwa
serikali itaikubali na kuitumia.
“Teknolojia hii inasaidia kuwakamata
majangili wakiwa wanafanya uharamia wao ndani ya hifadhi na hivyo kuondoa
malalamiko yaliyopo sasa kwamba majangili wanaokamatwa wanakuwa wanasingiziwa,”
anasema Makere.
Makere anaongeza: “Hivi sasa utaratibu
unaotumiwa ni kama wa mbwa kufuata nyayo na harufu kwani majangili mara nyingi
wanakuwa wanakamatwa wakiwa majumbani mwao, lakini hapa watakamatwa humo ndani
na hivyo kuukazia ushahidi kwani picha zipo na watakuwa na vidhibiti.”
Kampuni ya Bathawk Recon inajipambanua
kwamba kwa kuja na teknolojia hiyo ya utambuzi inaweza kuwa suluhu ya janga la
ujangili kwa kuwa inao uwezo wa kutambua majangili hata kama wakijificha, labda
kama watachimbia ardhini.
“Na kama watajichimbia basi itakuwa faida
zaidi, kwa sababu hawawezi kufanya lolote bila kuonekana,” anaongeza Jones,
ambaye kwa zaidi ya miaka 10 amekuwa rubani wa ndege za kivita kwenye Jeshi la
Kifalme (Royal Armed Forces).
Ofisa uhifadhi kutoka Hifadhi ya Tarangire,
Marandu, ambaye alimwakilisha Mhifadhi katika uzinduzi huo, anasema anaamini
teknolojia hiyo ni nzuri na inaweza kusaidia kuwahifadhi wanyama.
“Katika mapambano dhidi ya ujangili na
ustawi wa maliasili, mbinu yoyote yenye kuleta matokeo chanya ni vizuri
ikapokelewa na kujaribiwa, kama inafaa basi itakuwa msaada mkubwa kwa taifa,”
anasema.
Sera ya Taifa ya Wanyamapori ya mwaka
1998 inaelekeza kuwa aina zote za viumbe hai zihifadhiwe, wanyamapori wasitumiwe
kiasi cha kuifanya idadi yao ipungue na kuwa katika hatari ya kutoweka na kuhakikisha
Taifa linaendelea kumiliki wanyamapori na kusimamia kwa niaba ya wananchi.
Ndege zilizojaribiwa
DT-18 ilijaribiwa Tarangire
Hii ilitengenezwa Ufaransa. Ni ndogo sana,
inaweza kuruka kwa saa mbili tu katika nusu kipenyo cha kilometa 15 kutoka
ilipo mitambo.
DT-26 ilijaribiwa Selous
Imetengenezwa Ufaransa na kampuni ya Delair
Tech. Hii ni kubwa kidogo, ina uwezo mkubwa na inatumia viwango vya satelaiti
za kijeshi vya mawasiliano kutumana kupokeataarifa pamoja na namna ya kuongozwa
kwake.
Superbat DA 50 – Imejaribiwa Mkomazi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni