Beki wa Nigeria, William Ekong akibinuka tik tak dhidi ya mshambuliaji wa Tanzania, John Bocco katika mchezo wa leo
TANZANIA
imejiweka njia panda katika mbio za Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka
2017, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Nigeria, jioni ya
leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taifa
Stars sasa inakamilisha mechi mbili za Kundi G bila ushindi, baada ya
awali kufungwa mabao 3-0 na Misri mjini Alexandria Juni mwaka huu,
wakati Nigeria inafikisha pointi nne baada ya awali kushinda 2-0 dhidi
ya Chad.Kocha Charles Boniface Mkwasa aliwaanzisha wote washambuliaji wa
TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, lakini hii leo
waliishia kuisumbua tu ngome ya Eagles.
Mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta akimhadaa beki wa Nigeria, Solomon Kwambe
Mshambuliaji wa Tanzania, Mrisho Ngassa akimtoka winga wa Nigeria, Simon Moses
Kikosi cha Taifa Stars kilichotoa sare na Nigeria leo
Mshambuliaji wa Tanzania, Emmanuel Ulimwengu akipambana na beki wa Nigeria, Kenneth Emeruo
Mshambuliaji
wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mrisho Khalfan Ngassa alifanikiwa
kuwapenya mabeki wa Nigeria na kubaki na kipa Ikeme Onora lakini mara
zote dakika ya 13, 22 na 58 akakosa mabao ya wazi, kabla ya kutolewa
dakika ya 67 kumpisha John Raphael Bocco.
Mbwana Samatta naye dakika ya 15 aliwapangua mabeki wa Nigeria, lakini shuti lake likaenda nje.
Super
Eagles walipata nafasi moja tu nzuri dakika ya 24 baada ya shuti la
mpira wa adhabu wa Nahodha Ahmed Musa kupanguliwa na kipa Ally Mustafa
‘Barthez’.
Baada ya
mchezo huo, kocha wa Tanzania, Mkwasa aliwasifu vijana wake kwa kucheza
vizuri, lakini akasema bahati haikuwa yao kwani walitengeneza nafasi
wakashindwa kutumia.
Kwa
upande wake, Sunday Oliseh wa Nigeria alisema kipindi cha kwanza
walicheza kwa kuwahofia wenyeji, na hata kipindi cha pili walipotaka
kubadilika kucheza, lakini mechi ikawa ngumu.
Kikosi
cha Tanzania kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shomary Kapombe, Mwinyi
Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Himid Mao, Thomas
Ulimwengu, Mudathir Yahya/Said Ndemla dk61, Mbwana Samatta, Mrisho
Ngassa/John Bocco dk67 na Farid Mussa/Simon Msuva dk81.
Nigeria;
Ikeme Onora, Solomon Kwambe, Kingsley Madu, Kenneth Omeruo, William
Ekong, Nwankwo Obiora, Ahmed Musa, Haruna Lukman/Igboun Emeneka dk35,
Emmanuel Emenike/Ujah Anthony dk61, Uzochukwu Izunna na Moses
Simon/Eduok Samuel dk69.
CREDIT: BIN ZUBEIRY
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni