Kesi inayomkabili aliyekuwa rais wa Chad, Hissène Habré dhidi ya uhalifu wa binadamu, kivita na mateso, inaanza kusikilizwa leo
Jaji wa mahakama ya Burkinabe, Gberdao Gustave Kam ataamua iwapo kesi hiyo itaendelea bila upande wa utetezi wa Hissene Habre.
Tangu mwanzo wa utaratibu wa kesi hiyo, Hissene Habre, mwenye umri wa miaka 72, amekuwa akikataa kutambua uhalali wa mahakama maalum ya Afrika, ambayo iliundwa na Umoja wa Afrika mwaka 2013, ili kushugulikia kesi yake nchini Senegal. Rais huyo wa zamani wa Chad hajawahi kujibu maswali ya jaji.
Afisa wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Reed Brody amesema kwa kukataa kushirikiana na mahakama, Habre anajaribu kuchelewesha utaratibu wa mahakama, ambayo ina bajeti ya Dola milioni 9.5.
Kucheleweshwa kwa kesi hiyo kwa siku 45 kutaongeza bajeti kwa asilimia tisini.
Kesi hiyo ilikadiriwa kuchukua muda wa siku 90 pekee. Waathirika ambao walifanya kampeni ya miaka 25 kuhakikisha ameshtakiwa wanatarajia kuwa mahakama hiyo itatenda haki.
Hii ni mara ya kwanza rais wa nchi kushtakiwa katika nchi nyingine ya Afrika kwa shutma za unyanyasaji, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo maalum atajaribu kuwasilisha ushahidi kuonyesha kuwa Habre aliamuru mauaji na unyanyasaji wa maelfu ya watu waliompinga kisiasa.
Tume ya ukweli iliyoundwa kuchunguza madai hayo ilipata ushahidi wa mauaji ya takriban watu 4,000 na ikakadiria kuwa huenda idadi hiyo ikawa mara 10 zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni