Deo Filikunjombe (1972 -2015)
Taifa limekumbwa na msiba mzito
baada ya kuthibitika kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe (43) na watu wengine watatu kufariki dunia
baada ya helikopta (chopa) waliyokuwa wakisafiria kutoka jijini Dar es Salaam
kuelekea Ludewa mkoani Njombe kuanguka na kuwaka moto katika Mbuga ya Selous.
Miongoni mwa waliopoteza maisha
katika ajali hiyo ni rubani wa chopa hiyo, Kapteni William Silaa ambaye pia ni
baba wa mgombea Ubunge wa Jimbo la Ukonga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Jerry
Silaa.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa
Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alisema jana kuwa Filikunjombe na watu wengine
watatu waliokuwamo kwenye chopa hiyo wamepoteza maisha baada ya chopa
waliyokuwa wakisafiria kuanguka na kuwaka moto.
Kamishna Chagonja alisema tukio hilo
lilitokea jioni (juzi) katika mbuga ya Selous, eneo la Msolwa. Alisema muda
kamili wa kutokea kwa tukio hilo bado haujafahamika kwakuwa iliangukia porini
na eneo hilo halina mawasiliano, lakini watu walioshuhudia walisema ni jioni.
Chagonja alisema timu ya upelelezi
ya polisi kwa kushirikiana na mamlaka ya anga inafuatilia tukio hilo pamoja na
kubaini majina kamili ya watu wawili. Alisema bado wanafuatilia zaidi kujua
mmiliki wa chopa hiyo.
Taarifa nyingine zilizothibitishwa
na Zitto Kabwe ambaye ni rafiki wa karibu wa marehemu Filikunjombe zilieleza
kuwa miili ya marehemu iliwasili saa 12:00 jioni jana na kwamba, yote
imepelekwa na kuhifadhiwa kwenye Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
Ilelezwa zaidi kuwa miili hiyo
ilikuwa imeungua vibaya na hivyo haikuwa rahisi kuitambua, ingawa Filikunjombe
alitambuliwa mapema kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni saa aliyokuwa
ameivaa.
Kamishna Chagonja alisema taarifa
zaidi kuhusiana na ajali hiyo zitatolewa leo baada ya kupokea ripoti kamili
kutoka kwa wataalamu waliokwenda katika eneo la ajali.
NDUGU WAZUNGUMZA
Kadhalika, akizungumza na Nipashe
jana, Msaidizi wa Jerry Silaa, alisema walipata taarifa za kutokea kwa kifo
hicho jana majira ya saa 7:00 mchana.
“Jerry Silaa hawezi kuzungumza na
simu kutokana na hali iliyotokea. Taarifa ya kifo tumeipata kutoka kwa Kamishna
Chagonja,” alisema msaidizi huyo wa Jerry Silaa.
Kaka wa Filikunjombe, Dominic Haule,
aliiambia Nipashe jana kuwa taarifa za vifo hivyo, walizipata kutoka kwa
Jerry Silaa.
“Taarifa tulizonazo hadi sasa ni za
Jerry Silaa ambazo zimeenea mitandaoni. Walipata ajali wakiwa wanne na wote
wamepoteza maisha.
Dominic aliongeza kuwa yeye alikuwa
ni miongoni mwa abiria waliokuwa wasafiri na marehemu lakini alibanwa na
kazi nyingine na hivyo akanusurika.
“Naomba uwaeleze watu kuwa mimi
sijafariki dunia kwa sababu ni miongoni watu niliotakiwa kuwamo kwenye safari
hiyo lakini nilibanwa na kazi nyingine mkoani Mwanza,” alisema Haule.
Alisema wanaodhaniwa kufa ni
waliokuwa kwenye chopa hiyo ambao ni pamoja na kaka yao mkubwa, Casablanca
Haule Filikunjombe, ambaye alisafiri badala yake. Alisema abiria mwingine
alikuwa ni rafiki yao, Egid Mkwera, ambaye alikuwa ni Ofisa Mipango wa Musoma.
“Huyu rafiki yetu alitoka Musoma
jana (juzi), akanifuata Mwanza nikamkatia tiketi ya ndege ili amuwahi
Filikunjombe uwanja wa ndege na kweli alimkuta na kuanza kusafiri wote...naye
amepoteza maisha,” alisema Haule.
Alimtaja abiria mwingine aliyetakiwa
kusafiri na Filikunjombe kuwa ni Tonny Kebeda, ambaye alichelewa helikopta na
hivyo kuachwa.
“Filikunjombe na kaka yetu pamoja na
huyu rafiki yetu, walimsubiri kwa nusu saa huyu Kebeda na walipoona anachelewa,
wakaamua kuruka na kumuacha. Ilibidi wawahi kwenda Ludewa kwa sababu leo (jana)
walikuwa wafanye mkutano wa kampeni kwenye Kijiji cha Lupingu” alisema
Dominic.
Akizungumza muda waliosafiri,
alisema waliruka kutoka uwanja wa ndege majira ya saa 10:00 jioni wakielekea
Ludewa na kwamba, ilipofika saa 12:00 jioni, Katibu Mwenezi wa CCM ludewa,
alimpigia simu kumuuliza sababu za chopa hiyo kuchelewa kutua. Alisema aliamua
kuwasiliana na watu mbalimbali kuulizia chopa hiyo imekwama wapi bila ya
mafanikio.
“Taarifa tuliyopata ni kuwa helkopta
hiyo ilianguka mida ya saa 12:00 jioni, lakini taarifa ya kutokea vifo hivyo
tumeipata leo,” alisema Dominic.
Akizungumzia taratibu za msiba,
alisema marehemu alikuwa na nyumba Kijichi jijini Dar es Salaam na ndipo msiba
huo utakuwapo kabla ya kusafirishwa kupelekwa jimboni mwake, Ludewa mkoani
Njombe.
“Niko njiani natokea Mwanza kuelekea
nyumbani Kijichi. Taratibu zote zitakuwa nyumbani hapo Dar es Salaam na baadaye
kwenda Ludewa,” alisema.
MENEJA MBUGA YA SELOUS
Meneja wa Pori la Akiba la Selous,
Benson Kibonde, akizungumza na Nipashe, alisema taarifa za kutokea kwa ajali
hiyo saa 11:00 juzi alizipata kutoka kwa Deogratius Sanga, ambaye ni mmoja wa
wafanyakazi wa kampuni ya Forward Venture inayomiliki kitalu cha uwindaji cha
R2.
Alisema wakati Sanga na wenzake
wakiendelea na shughuli za uwindaji katika kitalu hicho, ghafla waliona
helikopta hiyo ikianguka na muda mfupi kutoa kishindo kikubwa katika eneo la
kitalu cha R3.
Kibonde alisema baada ya kupata
taarifa hizo, jitihada za kujulisha ofisi ya Bunge na uwanja wa ndege zilifanyika
lakini kufika eneo la tukio ilikuwa si kazi rahisi kwani ni ndani kabisa ya
msitu.
MAGUFULI AMLILIA
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Dk. John Magufuli, amesema amepokea kwa mshtuko na na kupatawa na huzuni
kubwa kutokana na taarifa ya kifo cha Filikunjombe pamoja na watu wengine
watatu akiwamo Kapteni Silaa.
Dk. Magufuli alituma salamu za
rambirambi kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga, Meya wa Manispaa ya
Ilala, Mstahiki Jerry Silaa na familia za wafiwa.
“Kwa hakika, nimeshtushwa na
kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya Filikunjombe na Silaa ambavyo
nimetaarifiwa kuwa vimetokea kwa ajali ya helkopta aliyokuwa akiitumia Ndugu
Filikunjombe kwa kampeni zake za ubunge katika jimbo hilo la Ludewa,” ilisema
sehemu ya taarifa ya Magufuli.
Aliongezea kuwa, “Kama unavyojua,
namfahamu vizuri Filikunjombe. Alikuwa mbunge mwenzangu katika Bunge
lililomaliza muda wake mwaka huu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa miaka
mitano ndani ya bunge letu. Alikuwa mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na
mwadilifu kwa wananchi wa Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Ludewa, ambao
aliwawakilisha vyema,”
Katika taarifa hiyo, Dk. Magufuli
alieleza kuwa alivyofanya ziara katika Jimbo la Ludewa mwezi uliopita alikuwa
akilala nyumbani kwake, na hiyo inadhihirisha namna alivyokuwa karibu
naye.
Pia alituma salamu zake za
rambirambi kwa Mstahiki Meya Silaa kwa kufiwa na baba yake kwani ni tukio
lisilozoeleka, na pia wafiwa wengine.
“Nawapa pole kwa wanandugu wengine
waliopoteza ndugu zao katika tukio hilo... wawe na subira katika kipindi hiki
kigumu,” ilisema taarifa hiyo ya Magufuli.
Kadhalika alituma salumu nyingine za
rambi rambi kwa Spika wa Anna Makinda na Wabunge wote kwa kuondokewa na
mwenzao.
Dk. Magufuli aliongezea “Nakuomba
pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa wananchi wa Jimbo na Wilaya ya
Ludewa ambao wamepoteza Mbunge wao aliyewatumikia kwa ustadi mkubwa kwa kipindi
chote kwa kujali maslahi ya wananchi wake,”
LOWASSA ASHTUSHWA
Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ameelezea kustushwa kwake na taarifa za
kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe, aliyefariki
dunia juzi jioni baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria kuanguka kabla ya
kushika moto katika maeneo ya Mbuga ya Selous mkoani Morogoro.
Katika taarifa yake alaiyoituma kwa
vyombo vya habari jana, Lowassa anayewakilisha pia muungano wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Wananchi (CUF),
NCCR-Mageuzi na NLD, alisema kifo cha mgombea huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
aliyekuwa mahiri na imara katika kutetea jimbo lake na Watanzania, ni pigo
jingine kubwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Oktoba 25.
"Ni pigo lingine kubwa ambalo
katika kipindi kifupi taifa limepata, huku bado tukiwa na kidonda cha
kuondokewa na wanasiasa wengine mahiri, marehemu Celina Kombani, Dk. Abdallah
Kigoda na Dk. Emmanuel Makaidi aliyefariki jana (juzi)," inasema sehemu ya
taarifa ya Lowassa kwenda kwa vyombo vya habari jana.
Kombani aliyekuwa akigombea ubunge
Jimbo la Ulanga Mashariki (CCM) na Dk. Kigoda wa Handeni (CCM) walifariki dunia
wakati wakitibiwa nchini India huku Dk. Makaidi wa NLD aliyekuwa akiwakilisha
Ukawa Jimbo la Masasi akifariki dunia juzi mchana wakati akitibiwa katika
Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi.
Wagombea ubunge wengine waliofariki
dunia katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu ni Mohamed Mtoi wa
Chadema aliyekuwa akiwakilisha Ukawa katika Jimbo la Lushoto na Estomiah
Mallah, aliyekuwa akiwania ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya ACT -
Wazalendo.
"Filikonjombe alikuwa ni mbunge
mahiri, aliyesimama imara kutetea maslahi ya wananchi wa jimbo lake la Ludewa
na pia Watanzania kwa ujumla. Ni taarifa ya kushtusha sana ya msiba wa mwanasiasa
chipukizi na jasiri, Deo Filikonjombe," iliongeza taarifa hiyo.
Kadhalika, Lowassa alimuelezea
Filikunjombe kuwa ni mbunge aliyekuwa mwiba kwa serikali ya chama chake (CCM)
wakati akitetea maslahi ya nchi, akitolea mfano katika kashfa ya Escrow ambayo
alikuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati iliyochunguza kashfa hiyo na kufanya kazi
nzuri kwa manufaa ya taifa.
"Mwenyezi Mungu awape moyo wa
subira familia, jamaa, marafiki na wananchi wa Ludewa katika kipindi hiki
kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao," alisema Lowassa.
Mbali na Filikunjombe, wengine
waliokuwamo na kufariki dunia katika helikopta hiyo aliyokuwa akienda kwenye
shughuli za kampeni za chama chake kwenye Jimbo la Ludewa kwa ajili ya uchaguzi
mkuu ni pamoja na rubani wa chopa hiyo, Kapteni William Silaa, ambaye ni baba
wa mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Jerry
Silaa.
KATIBU WA BUNGE
Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila
alisema kifo cha kiongozi huyo kimewashtua na kimewapa majonzi kwa kumpoteza
mtu ambaye alikuwa ni mahiri na mwadilifu katika kutekeleza majukumu
yake.
“Filikunjombe ni kiongozi ambaye ana
misimamo yake. Tumempoteza mtu muhimu sana. Mara zote alikuwa anasimamia kitu
anachokiamini,” alisema Dk. Kashilila, akiongeza kuwa Filikunjombe ni kiongozi
mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kutoa maamuzi sahihi na kwa wakati.
Kuhusiana na msiba huo, alisema
ofisi yake itatoa taarifa zaidi baadaye.
SIMANZI LUDEWA
Habari kutoka Ludewa hadi jana jioni
zilieleza kuwa, mamia ya wananchi walifurika nyumbani kwa marehemu Filikunjombe
huku wengine wakizimia huku vilio vikitanda eneo hilo.
Taarifa hizo zilieleza kuwa,
wananchi walianza kufurika nyumbani hapo majira ya saa 7:30 mchana, baada ya
kupata taarifa za Filikunjombe kufariki kutoka kwa ndugu walioko jijini Dar es
Salaam na vyombo vya habari.
Aidha taarifa zilieleza kuwa,
nyumbani hapo walikuwapo mama mzazi wa Filikunjombe na mjomba wake.
Pia watu walifurika nyumbani
kwake na kusababisha kukosekana wa eneo la kukaa na wengine kukaa kwenye nyumba
yake mpya aliyokuwa akijenga jirani na hapo.
Umati huo uliwalazimu baadhi ya
askari wa Jeshi la Polisi kufika nyumbani hapo kwa nia ya kuhakikisha kuwa
usalama unadumishwa.
DC: HAKUNA KAMA FILIKUNJOMBE
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Anatory
Choya, akizungumza na Nipashe jana, alisema hakuwahi kumuona mbunge shupavu
kama Filikunjombe katika kipindi cha maisha yake ya uongozi serikalini.
“Kifo hiki tumekipokea kwa mshituko
mkubwa, majonzi, vilio na sintofahamu zimetawala kwa wananchi wa Ludewa.
Nimefanya kazi serikalini miaka mingi, nimekuwa mkuu wa wilaya niliyeishi
na
wabunge wengi, lakini ukweli ni
kwamba Filikunjombe ni wa tofauti sana... sijawahi kuona kama yeye,”
alisema
CCM, LUDEWA WAOMBOLEZA
Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo,
Stanley Kolimba, alisema Filikunjombe ndiye mtu aliyepeleka maendeleo Ludewa na
alikuwa mbunge wa watu wote.
Alisema Filikunjombe alijitahidi
kufika kila kona ya wilaya hiyo kushughulikia matatizo ya wananchi bila kujali
jambo lolote.
“Mpaka sasa napokea simu kutoka kila
kona ya Ludewa, wengi wakimlilia... tumepoteza mwakilishi wetu shupavu,
mpambanaji, hodari mpenda haki na msaada mkubwa kwa wana Ludewa,” alisema
Kolimba.
MAMLAKA YA ANGA
Msemaji wa Mamlaka ya Anga Tanzania,
Bestina Magutu, alisema jana asubuhi walituma timu maalum ili mwishowe watoe
taarifa kamili ya kitaalam kuhusiana na tukio hilo.
“Ni kweli hiyo helkopta jana ilipata
ajali na tayari tumeshatuma wataalamu wetu kwenda eneo la tukio ...mara baada
ya kuchukua taarifa hizo watatutaarifu nasi tutawapatia taarifa kamili,”
alisema Magutu.
RUBANI SILAA
Kabla ya ajali hiyo ya juzi,
inaelezwa kuwa marehemu Kapteni Silaa, aliwahi kukumbana pia na ajali nyingine
ya chopa Julai 8 mwaka huu wakati akiwa Arumeru na Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na abiria wengine
wawili.
Katika tukio hilo lililotokea
Arumeru wakati wakiwa njiani kuelekea kwenye mkutano wa hadhara katika maeneo
ya Ndoombo na Ngureserosambu.
Wakati akisimulia tukio hilo na
namna walivyonusurika, Nassari alisema hali ya hewa ilikuwa mbaya, kulitokea
wingu zito lakini mwishowe walipona kutokana na ustadi mkubwa ulioonyeshwa na
Kapteni Silaa.
CHOPA 5Y-DKK
Kwa mujibu wa mtandao wa Rotorspot,
chopa 5Y-DKK inayotajwa kupata ajali iliyowaua Filikunjombe na Kapteni
Silaa ni miongoni mwa 58 zilizopo katika orodha ya usajili nchini Kenya baada
ya kuziondoa kwenye orodha zile zisizofanya kazi. Hata hivyo, Nipashe haikuweza
kuthibitisha moja kwa moja juu ya uhakika wa taarifa kwenye mtandao huo.
Kadhalika, inaonekana kuwa chopa
hiyo ni aina ya Aerospatiale 350B3 Ecureuil (AS350 B3E) na aina hiyo ya chopa
ilianza kutengenezwa nchini Ufaransa. Hivi sasa zinatengenezwa kwingineko pia
ikiwamo Marekani.
Toleo la chopa hizo linaelezewa kuwa
ni madhubuti na imara na kwamba, ndiyo chopa ya kwanza kuwahi kutua kwenye
kilele cha mlima mrefu kuliko yote duniani wa Everest. Baadhi ya rejea
zinaeleza kuwa chopa za toleo hili zilianza kutengenezwa mwishoni mwa mwaka
2011 na zina uwezo wa kuruka hewani na uzito wa hadi Kilogram 2,370.
CHOPA KAMA HII ILIMUUA SAITOTI
Katika mitandao mbalimbali ya
masuala ya usafiri anga, yanaonekena kuwa chopa aina hii licha ya kusifiwa kwa
ubora na kuaminiwa na taasisi mbalimbali maarufu duniani, lakini pia zimewahi
kukumbwa na matukio mbalimbali ya ajali. Mojawapo iliyo maarufu katika ukanda
wa Afrika Mashariki ni ile iliyotokea nchini Kenya Juni 10, 2012. Chopa hiyo
AS350 B3e), iliyokuwa mali ya Jeshi la Polisi la Kenya, ilianguka katika maeneo
ya Kibiku, kwenye msitu wa Ngong, magharibi mwa Nairobi, Kenya na kusababisha
vifo vya watu sita, akiwamo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, George Saitoti
na naibu waziri wake, Orwa Ojode.
SOURCE: NIPASH
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni