Waziri
 wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango (katikati) akitoa tamko kwa 
waandishi wa habari (hawamo pichani) jijini Dar es Salaam, kuhusiana na 
kusudio la kuitoza Benki ya Stanbic faini ya shilingi bilioni 3. Kulia 
kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa 
Serikali Dkt. Servicius Likwelile na Kushoto kwake ni Naibu Gavana wa 
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bw. Lila Mkila.
Mwezi
 Julai 2013, Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa 
shughuli za mabenki iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo
 na mikopo na pia kuacha na kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa
 Stanbic Bank Tanzania Limited (Stanbic) katika muda mfupi. 
Kutokana
 na hilo, Benki Kuu iliamua kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted 
Examination) katika benki hiyo. Ukaguzi huo ni kwa mujibu wa mamlaka 
iliyopewa Benki Kuu chini ya Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka
 2006 na Kifungu 31 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 
2006.
         Matokeo ya Ukaguzi wa Benki Kuu
Katika
 ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine walibaini 
miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya kitanzania ya 
Enterprise Growth Market Advisors (EGMA). Kampuni ya EGMA ilihusika 
katika uwezeshaji wa upatikanaji wa Mkopo kwa Serikali ya Tanzania 
ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa sasa inajulikana kama ICBC Standard
 Bank) na Stanbic Bank Tanzania Limited kwa pamoja walikuwa “Mwezeshaji 
Mkuu” (Lead Arranger). 
Malipo
 hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za 
kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic. Jumla ya malipo 
yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 6, na zililipwa katika 
akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu 
(cash) ambayo ni nje ya taratibu za kibenki.
Taarifa
 ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa 
taratibu, na Benki Kuu iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo 
kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana. 
Aidha,
 benki ya Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo cha Financial 
Intelligence Unit (FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana 
na miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama Sheria ya 
Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The Anti-Money 
Laundering Act, 2006) inavyoelekeza. Benki ya Stanbic ilitekeleza 
maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala inayotiliwa shaka.
Mnamo
 29 Septemba 2015, Benki Kuu ilipokea barua kutoka Idara ya Serikali ya 
Uingereza inayohusika na Upelelezi wa Makosa ya Kugushi na Rushwa 
(Serious Fraud Office – SFO) ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya kutumia ripoti
 yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc 
ambayo ilikuwa ni mshirika wa Stanbic Bank Tanzania Limited katika 
kuwezesha mkopo wa dola za kimarekani milioni 600 kwa Serikali na kwamba
 ripoti hiyo ingekuwa wazi kwa umma. 
Benki
 Kuu iliijibu SFO kuwa kwa mujibu wa Sheria ripoti za Benki Kuu 
zinatolewa tu kwa benki au taasisi ya fedha inayohusika, hata hivyo, 
Benki Kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za ripoti hiyo 
kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.
Hatimaye,
 Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola 
za kimarekani milioni 32.20, ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni
 7 zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania (dola za kimarekani milioni 6 
zilikuwa ni fidia na dola za kimarekani milioni 1 ni riba).
Kwa
 kuzingatia mapungufu ya kufanya miamala iliyohusisha EGMA na pia 
kutokuweka taratibu madhubuti za udhibiti wa ndani, na kwa kuzingatia 
Kifungu 67 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, 
Benki Kuu imeiandikia benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini
 ya shilingi bilioni 3. Sheria inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi 
katika kipindi cha siku ishirini (20) ambacho kitaisha tarehe 30 Januari
 2016. Endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic 
italazimika kulipa faini hiyo.
Benki
 Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya Stanbic na ili iweze 
kuwa makini katika kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa 
mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia Sheria.
Aidha,
 hatua hii ni onyo kwa mabenki na taasisi za fedha zisijihusishe na 
makosa ya aina hii ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na ni 
uvunjaji wa Sheria za nchi. Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki
 au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za
 kibenki na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 20isi za Fedha ya mwaka 2006.