Jumanne, 22 Novemba 2016

Ajali ya treni yaua watu 140 India

Watu 140 wameuawa na wengine zaidi 150 wamejeruhiwa wakati treni ilipoacha reli katika jimbo la Uttar Pradesh kaskazinii mwa India Jumapili (20.11.2016).
Maafisa wa polisi wamesema takriban watu 20 bado hawajulikani walipo wakati mamlaka zikijaribu kutafuta chanzo kilichosababisha kuanguka kwa ghafla kwa mabehewa 14 kutoka kwenye reli huko Pukhran kiasi cha kilomita 65 kusini mwa mji wa Kanpur wakati treni hiyo ilipokuwa ikisafiri kati ya mji wa kaskazini mashariki wa Patna na mji wa kati wa Indore.
Huku kukiwa na hali ya taharuki na kuchanganyikiwa manusura wamekuwa wakihangaika kuwatafuta ndugu zao na wengine wamekuwa wakijaribu kuingia kwenye mabehewa yalioharibiwa kuwaokoa jamaa zao na kukusanya vitu vyao.

Pratap Rai afisa mwandamizi wa reli amesema wanatumia kila mbinu kunusuru maisha lakini ni vigumu sana kukata mabehewa ya chuma.

Indien Zugunglück (Reuters/J.Prakash) Hali katika eneo la ajali.
Ajali hiyo inaweza kuwa ajali mbaya kabisa ya reli kutokea nchini India tokea mwaka 2005 wakati treni ilipobamizwa na jabali na nyingine kutumbukia mtoni kila moja ikiua watu zaidi ya 100.
Mfumo wa reli wa India ulioelemewa unashika nafasi ya nne kwa ukubwa duniani ukisafirisha watu zaidi ya milioni 20 kwa siku lakini una rekodi mbaya ya usalama ambapo maelfu ya watu wanakufa katika ajali kila mwaka zikiwemo ajali za mara kwa mara za treni kuacha reli.
Suresh Prabhu waziri wa reli nchini India amesema katika mtandao wa Twitter kwamba serikali itachunguza kwa haraka sababu za treni hiyo kuacha reli na kuahidi uwajibikaji na kuchukuliwa kwa hatua kali.

Indien Zugunglück (Reuters/J.Prakash) Hali katika eneo la ajali.
Mabehewa yaharibiwa vibaya
Mikanda ya video imeonyesha mabebewa yaliyoharibiwa vibaya huku polisi na watu wakiwa juu ya mabehewa hayo wakitafuta manusura. Maafisa wa uokozi wameonekana wakijipenyeza kwenye umma wa watu huku wengine wakiyaondoa mabehewa yaliyoinduka kutoka kwenye reli mojawapo ya njia kuu za usafiri wa mizigo na abiria kaskazini mwa India.
Treni hiyo iliyokuwa imefurika abiria ambayo inamilikiwa na serikali imeacha reli alfajiri ya Jumapili wakati abiria zaidi ya 500 walipokuwa wamelala. Treni kuacha reli na ajali nyingine za treni zimekuwa zikitokea mara kwa mara ikiwemo ajali iliyotokea Uttar Pradesh jimbo lenye idadi kubwa ya watu nchini India hapo mwezi wa Machi mwaka jana na kuua watu 39.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi aliyeanza maisha kwa kuuza chai nje ya vituo vya treni ameahidi kufanya mfumo wa  safari za reli nchini India kuwa wa kisasa.
Mwandishi: Mohamed Dahman /Reuters
Mhariri: Zainab Aziz

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni