Rais wa Brazil Michel Temer atangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia vifo vya wachezaji vilivyosababishwa na ajali ya ndege. Rais wa Brazil Michel Temer ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia vifo vya wachezaji wa timu ya soka ya Chapecoense, ambao walikuwa miongoni mwa abiria 81 waliokuwemo kwenye ndege iliyoanguka kwenye milima ya Colombia jumatatu hii, na kusababisha vifo vya abiria 76, na wengine watano kunusurika.
Ndege hiyo ndogo ya shirika la ndege la LAMIA awali ilitoa taarifa ya hali ya hatari iliyosababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa umeme, na hatimaye kuanguka muda mfupi baadaye karibu na mji wa Medelin.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba wachezaji wa timu ya Chapecoense Real ya Brazil, iliyokuwa ikielekea kucheza mechi ya fainali ya michuano ya kuwania ubingwa wa kombe la Amerika ya Kusini (Copa Sudamericana) ambayo ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Amerika ya Kusini, iliyotarajiwa kuchezwa kesho jumatano dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia.
Pamoja na Rais Temer kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, kumeendelea pia kutolewa rambirambi kutoka kona mbalimbali Barani Ulaya, ambapo Rais wa shirikisho la soka duniani, FIFA, Gianni Infatino amesema, " Hili ni tukio la kusikitisha sana kwenye anga la soka, na limetokea katika kipindi kigumu. Mawazo yetu yapo kwa wahanga wa ajali hiyo, familia na jamaa zao" amesema Infatino. FIFA inatoa pole kwa mashabiki wa Chapecoense, jumuiya ya soka na vyombo vya habari vya nchini Brazil.
Mmoja wa wajumbe wa bodi ya timu hiyo, Plinio De Nes, amesema wachezaji hao waliiaga bodi wakisema wanaenda kutimiza ndoto yao waliyoiota kwa muda mrefu.
Mshambuliaji wa timu ya Colombia Radamel Falcao, yeye ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema, "maombi yangu ni kuwa na mshikamano na manusura, familia na jamaa ya wachezaji hao katika kipindi hiki kigumu."
Timu ya Atletico Madrid, nayo imetuma salamu za pole kupitia Twitter, ikiandika, "Tumeshtushwa sana na ajali hiyo inayohusisha klabu ya mchezaji mwenzetu wa zamani, Cleber Santana ambaye kwa sasa alikuwa ni kapteni wa timu hiyo ya Chapecoense, "salamu zetu za pole ziwafikie familia zao. Pumzikeni kwa amani.
Mawazo ya kila mmoja wa Manchester United yapo kwa wahanga wa ajali ya ndege wa timu ya soka ya Chapecoense na wale wote walioathirika na janga hilo la Colombia, imeandikwa kwenye ukurasa wa Twitter wa timu ya Manchester United ya Uingereza, ambayo nayo iliwahi kupoteza wachezaji wanane mnamo mwezi Februari mwaka 1958, wakati ndege yao ilipoanguka ikiwa inaondoka kutoka uwanja wa ndege wa Munich.
Timu ya Real Madrid, kupitia tovuti yake, nayo imeeleza kusiktitishwa kwake na tukio hilo, na kutoa salamu za pole kwa ndugu na jamaa wa wahanga hao, huku pia ikiwatakia kuimarika kwa haraka afya za majeruhi wa ajali hiyo. mawazo yetu yapo pamoja na Chapecoense na kila mmoja aliyeguswa na ajali hii na familia zao, hatuna neno la kuongeza, ameandika kapteni wa Real madrid, Sergio Ramos, kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Timu za FC Barcelona, AS Roma na FC Porto nazo zimetuma salamu za pole kupitia kurasa za Twitter, kutokana na ajali hiyo.
Wachezaji tisa wa timu hiyo hawakusafiri. Ndege hiyo hiyo iliwabeba wachezaji wa timu ya Argentina wiki mbili zilizopita ikiwa na mchezaji Lionel Messi walipokuwa wakielekea san Juan Argentina kwa ajili ya mechi ya kufuzu kucheza kombe la dunia.
Mwandishi: Lilian Mtono/ http: AFPE/ APE/ //www.dw.com/en/plane-crash-kills-76-in-colombia-6-survive/a-36565336.
Mhariri: Saumu Yusu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni