Alhamisi, 1 Desemba 2016

Mganga auawa kwa kutaka kubaka mteja


MGANGA wa kienyeji aliyejulikana kwa jina la Kashinje Kashinje (55), mkazi wa kijiji cha Singita kilichopo Kata ya Usanda wilayani hapa ameuawa kwa kupigwa na wananchi ikielezwa alijaribu kutaka kumbaka mteja wake.
Mteja huyo ambaye ni mwanamke mwenye umri wa miaka 20 (jina linahifadhiwa) aliyekwenda kutibiwa ugumba kwa lengo la kupata mtoto.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne, tukio hilo ni la Novemba 29 mwaka huu, akisema lilitokea majira ya saa tano asubuhi.
Alisema Kashinje alifariki dunia alipokuwa anakimbizwa hospitali baada ya kujeruhiwa kwa kitu chenye ncha kali katika jicho la kulia na kupigwa kwa fimbo mgongoni na watu waliojichukulia sheria mkononi.
“Watu hao walijichukulia sheria mkononi baada ya mganga huyo kujaribu kumbaka mwanamke huyo mkazi wa kijiji cha Ishinabulandi wilaya ya Shinyanga ambaye alikuwa akimtibu kwa tiba za asili ili aweze kupata mtoto”, alieleza kamanda Muliro.
Alisema tatizo lililompeleka mwanamke huyo kwa mganga ni kupata tiba ili aweze kupata mtoto.
Kamanda Muliro alibainisha kuwa chanzo cha tukio hilo ni tamaa za kimwili na uongo wa kimatibabu wa kutaka kumuingilia kimwili mgonjwa wake baada ya kumlewesha kwa dawa za kienyeji, lakini alifanikiwa kupiga kelele na ndipo wananchi walipomvamia mganga huyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni