Jumatano, 18 Desemba 2013

ABIRIA 213 WA NDEGE YA ETHIOPIA AIRNES WANUSURIKA KIFO, NI BAADA YA KULAZIMIKA KUTUA KWA DHARURA KATIKA UWANJA MDOGO WA NDEGE WA ARUSHA.





Ndege ya Ethiopia ililazimika kuelekea Arusha na kutua kwenye uwanja huo mdogo kuweza kupokea ndege kubwa kutokana na kuishiwa mafuta.
ARUSHA. 
ABIRIA 213 waliokuwa wakisafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia jana walinusurika kifo baada ya ndege hiyo kutua kwa dharura katika uwanja mdogo wa Arusha.



Ndege hiyo aina ya Boeing 767, ilitua saa 6.45 mchana katika uwanja huo baada ya kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kutokana na kupata pancha kwa ndege nyingine inayomilikiwa Shirika la Ndege la Tanganyika (TFC), kwenye njia ya uwanja huo.



Ndege ya Ethiopia ililazimika kuelekea Arusha na kutua kwenye uwanja huo mdogo kuweza kupokea ndege kubwa kutokana na kuishiwa mafuta.


Ndege hiyo iliyokuwa inatokea Addis Ababa, Ethiopia ikiwa pia na wahudumu 23, baada ya kutua kwenye Uwanja wa Arusha, ilinasa kwenye tope baada ya tairi lake la mbele kuvuka sehemu ambayo lami inaishia kutokana na ufupi wa njia zinazotumiwa na ndege zinapotua kwenye uwanja huo.


Jitihada za kuiondoa ndege hiyo zilishindikana jana. Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Johannesburg, Afrika Kusini kwa kupitia Kia na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema: “Rubani amejitahidi kutua katika uwanja huu japo ni mdogo ili kuokoa maisha ya abiria kwani walikuwa hawana mafuta ya kutosha kwenda uwanja mwingine.”


Tukio la ndege hiyo kutua kwa dharura limekuja siku chache tangu ndege ya Shirika la Ndege la Precision iliyokuwa na abiria 37 kupasuka matairi manne ilipokuwa ikitua kwenye Uwanja wa KIA Jumamosi iliyopita. MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni