MASIKU
Mbaraka Mwishehe ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Kinondoni, Dar es
Salaam kwa madai ya kuwashambulia kwa kisu watu wawili wa familia moja. Tukio
hili lilitokea hivi karibuni Mwananyamala Kisiwani, Dar ambapo kwa
mujibu wa taarifa ya kipolisi, mtuhumiwa huyo alikutwa ndani ya nyumba
ya Nelson Ainea Shoo, saa kumi na moja alfajiri. Akizungumza na Amani, mke wa Nelson aliyejitambulisha kwa jina la Neema Hamis Zame (32), alikuwa na haya ya kusema:
“Siku ya tukio, ilikuwa alfajiri kabla hatujaamka, ghafla nilimsikia
shemeji yangu aitwaye Goodluck (Ainea Shoo) akipiga kelele na kusema:
‘Kaka kuna mwizi.’ Mume wangu aliamka akatoka kuelekea sebuleni na mimi
nilikuwa nyuma yake. “Kufika, tulimkuta shemeji amelala sakafuni huku
utumbo ukiwa nje na damu nyingi zikimtoka, alikuwa akikoroma, kumbe
alichomwa kisu kwenye paja, mara mbili tumboni na begani. “Nilikimbilia
chumbani kuchukua khanga na kumfunga ili kuzuia damu isitoke kwa wingi,
pia utumbo usiendelee kumwagika huku mume wangu akimdhibiti yule
mtu. “Cha ajabu, muda mfupi mume wangu naye akawa chini anatokwa damu,
kumbe hata yeye alikuwa amechomwa kisu mara tatu tumboni na utumbo
ukatoka nje.
“Hali ndani ilikuwa mbaya, sakafu ilitapakaa damu. Nikamwita shemeji
yangu mwingine aitwaye Erick (Ainea Shoo), yeye akapambana na yule mtu
wakati mimi nawahudumia wale majeruhi. “Nilipata akili za haraka,
nilikwenda kumuita mlinzi akaingia na kushirikiana na shemeji
wakamdhibiti. Huwezi kuamini, eti yule mtu akaomba asamehewe kwa vile
hakujua kama alikuwa ameingia katika nyumba yetu.
“Hakuna aliyemsikiliza kwani alikuwa amefanya kosa kubwa, akaingizwa
kwenye gari hadi polisi kuchukua PF3 na likafunguliwa jalada
(OB/RB/20201/2013 Kujeruhi) kisha majeruhi tukawapeleka Hospitali ya
Muhimbili. “Kilichotokea hospitali, shemeji alitolewa bandama kwa vile
iliharibika kutokana na majeraha ya kisu,” alisema Neema.
Naye baba mzazi wa majeruhi hao, mzee Ainea Shoo ambaye alitoka
Machame Moshi, Kilimanjaro baada ya kupata taarifa hizo, alisema
mtuhumiwa huyo alikuwa na dhamira ya kuwatoa roho watoto wake hao,
akaliomba jeshi la polisi kushughulikia kesi hiyo kwa uwazi na
kuhakikisha haki inatendeka. Mlinzi wa nyumba hiyo, Boli Mtumwa
alipohojiwa na gazeti hili alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema yeye
na mdogo wa Nelson ndiyo waliomdhibiti mtuhumiwa na kumpeleka
polisi. Dada wa mtuhumiwa aliyejitambulisha kwa jina la Taji Mbaraka
alikiri kukamatwa kwa kaka yake huyo lakini hakuwa tayari kuzungumza
zaidi kwa sababu suala hilo lipo mkononi mwa dola. Kaimu Kamanda wa Mkoa
wa Polisi Kinondoni, ACP Yusuf Mrefu alikiri kutokea kwa tukio hilo na
kusema kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa huku upelelezi ukiendelea.
source: GPL
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni