HOTUBA YA MKUU WA NCHI DK JAKAYA KIKWETE YA KUFUNGIA MWAKA 2013 NA KUUKARIBISHA 2014 NDIYO HII. AFAFANUA UTENDAJI MZURI WA SERIKA KWA MWAKA 2013
SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT.
JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA, TAREHE 31 DESEMBA, 2013.
Utangulizi Ndugu zangu; Watanzania
Wenzangu; Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema,
kwa kutujalia uzima mpaka kufika na kuiona siku hii ya leo ya kuuaga mwaka 2013
na kuukaribisha mwaka 2014. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao
hawakupata bahati tuliyoipata sisi kwa vile wametangulia mbele ya haki.
Tuendelee kumwomba Mola wetu awape mapumziko mema na azilaze roho zao mahali
pema peponi. Ameen. Hali ya
Usalama Ndugu Wananchi; Tunaumaliza mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama na
tulivu. Mipaka iko salama na ile hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati
fulani mwaka huu sasa haipo tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na
tutaendelea kufanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au
hata kuwa bora zaidi mwaka 2014 na daima dumu. Hali ya usalama wa ndani ya
nchi nayo ni nzuri. Hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo mwaka wa jana na mwanzoni
mwa mwaka huu kuhusu uhusiano baina ya Wakristo na Waislamu haipo. Ni matumaini
yangu kuwa haitajirudia tena. Pepo mbaya amepita tuombe atokomee
kabisa. Ndugu zangu; Watanzania wenzangu; Napenda kurudia kuwasihi kuwa
tuchague kuendelea kuishi pamoja kwa upendo, umoja, kuvumiliana na kushirikiana.
Tuepuke kugeuza tofauti zetu za kisiasa, kidini, rangi, kabila au maeneo
tutokayo kuwa chanzo cha uadui na mifarakano. Kwa sasa tuna mwelekeo mzuri
nawaomba tuudumishe. "Mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi".
Tuchague kuijenga nchi yetu badala ya kuibomoa. Tusiwasikilize watu hasidi
wanaochochea uadui na mifarakano miongoni mwetu. Watatuvurugia nchi yetu
nzuri.(P.T) Uhalifu Ndugu Wananchi; Katika mwaka 2013 vyombo vya dola
vikishirikiana na wananchi viliendelea kupambana na vitendo vya uhalifu.
Mafanikio ya kutia moyo yameendelea kupatikana ingawaje bado kuna kazi kubwa ya
kuendelea kufanya mwaka 2014 na miaka ijayo. Dawa za Kulevya Ndugu
Wananchi; Kati ya Januari na Desemba 2013, kilo 1,261 za heroin, kilo 3 za
cocaine na kilo 89,293 za bangi zimekamatwa na watuhumiwa 1,631 wametiwa
mbaroni. Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na mapambano
yanazidi kuwa makali. Mafanikio yanaendelea kupatikana ingawaje bado tuna kazi
kubwa na ngumu ya kufanya mbele yetu. Ni makusudio yetu kuongeza maradufu nguvu
ya kupambana dhidi ya uhalifu huu. Tupo hatua nzuri katika matayarisho ya
kuanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha
2014/15. Pia tutaitazama upya sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya
dawa za kulevya ili kuifanya iwe na meno makali zaidi. Vilevile, tutaongeza
uwekezaji katika vituo vya tiba na kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za
kulevya. Mafanikio yanayopatikana Muhimbili na Mwananyamala yanatupa moyo wa
kufanya zaidi. Ujambazi Ndugu wananchi; Jeshi la Polisi limeendelea
kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio yameendelea kupatikana.
Matukio ya ujambazi yemepungua mwaka 2013 ukilinganisha na mwaka 2012. Takwimu
zifuatazo zinathibitisha ukweli huo. Mwaka 2012 matukio ya ujambazi
yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409.
Mwezi Julai mwaka huu, niliamua kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania katika kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa magari
katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma. Katika Mikoa hiyo tatizo la ujambazi
lilikuwa limefikia kiasi cha kulazimisha watu kusindikizwa na Polisi kutoka
Ngara kwenda Karagwe, Biharamulo kwenda Muleba na kutoka Nyakanazi hadi Kakonko.
Hali hii haikubaliki na hatuwezi kuiacha iendelee. Ndugu Wananchi; Uamuzi
wangu huo ndiyo ulioanzisha Operesheni Kimbunga ambayo imekuwa na mafanikio ya
kutia moyo. Hali ya usalama katika Mikoa hiyo inaelekea kuimarika ingawaje ni
mapema mno kusema tatizo limedhibitiwa. Silaha nyepesi na nzito zipatazo 650
zikiwemo za kijeshi na za kiraia pamoja na mabomu ya kutupwa kwa mkono 11
zilikamatwa kwenye operesheni hiyo. Aidha, watu 31,203 waliokuwa wanaishi nchini
kinyume cha sheria walirudi makwao. Kati yao, watu 21,758 walirudi kwa hiari na
9,445 walirudishwa wakati wa Operesheni. Ndugu Wananchi; Nimepata
minong'ono kuwa baadhi ya watu walioondoka wanarudi kinyemela. Napenda
kuwatahadharisha kuwa wasifanye hivyo. Wanajisumbua bure. Hawatadumu. Ushauri
wangu kwao ni kuwa kama wanapenda kuishi Tanzania wafuate njia halali za kufanya
hivyo. Ujangili wa Wanyamapori Ndugu Wananchi; Mwaka huu tuliongeza
nguvu katika kupambana na ujangili wa wanyamapori na uvunaji haramu wa
rasilimali za misitu. Hili ni tatizo la siku nyingi lakini katika miaka ya hivi
karibuni limekuwa kubwa mno na kuwazidi nguvu Askari wa Wanyamapori na Maafisa
Misitu. Kwa nia ya kuwaongezea nguvu, mwaka 2010 niliagiza Jeshi la Polisi
lisaidie Idara ya Wanyamapori na Idara ya Misitu katika kupambana na uhalifu
huo. Operesheni kadhaa ziliendeshwa maeneo mbalimbali nchini na mafanikio ya
kutia moyo yalipatikana. Lakini, kwa kutambua ukubwa wa tatizo na hasa kwa
upande wa aina ya silaha na mbinu zinazotumiwa na majangili niliamua kuhusisha
vyombo vingine vya usalama likiwemo Jeshi la Ulinzi. Nia ni kuongeza nguvu ya
mapambano. Ndipo ilipoanzishwa "OPERESHENI TOKOMEZA". Ndugu Wananchi; Kazi
nzuri imefanyika chini ya Operesheni hiyo. Mafanikio ya kuleta matumaini
yameweza kupatikana. Mitandao ya ujangili imeweza kutambulika na wahusika wake
kadhaa wametiwa nguvuni. Mitandao hiyo inahusisha watu wa aina mbalimbali. Wamo
raia wa kawaida, wapo watu maarufu, wapo watumishi wa idara mbalimbali za
Serikali wakiwamo wa Idara za Wanyamapori na Misitu. Watu 1,030 walikamatwa
pamoja na silaha za kijeshi 18, za kiraia1,579 na shehena kubwa za meno ya ndovu
na nyara nyingine navyo vilikamatwa.Watu kadhaa tayari wameshafikishwa
mahakamani. Ndugu Wananchi; Wahenga wamesema "kwenye wengi pana mengi".
Katika utekelezaji wa Operesheni hii kumekuwepo na taarifa za kufanyika makosa
kinyume na malengo na madhumuni ya Operesheni. Niliagiza baada ya kumalizika kwa
awamu ya kwanza, zoezi lisitishwe kwa muda ili uchunguzi ufanyike, kasoro
zitambuliwe na waliofanya makosa wachukuliwe hatua zipasazo. Wakati kazi hiyo
inafanyika suala hilo lilijadiliwa Bungeni na Kamati Teule kuundwa. Matokeo yake
sote tunayajua. Mawaziri wanne wamewajibika kisiasa. Ndugu
Wananchi; Napenda kutumia nafasi hii kuwapa pole Mawaziri wetu hao kwa
matatizo yaliyowakuta. Nawapongeza kwa uamuzi wa kukubali kuwajibika kwa makosa
yaliyofanywa na maofisa wa chini yao. Wameonesha ukomavu wa kisiasa na kiuongozi
wa hali ya juu na moyo wa uzalendo. Kama mlivyosikia nitaunda Kamisheni ya
Uchunguzi itakayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu. Uchunguzi wa kina utafanywa
kuhusu kadhia yote hiyo. Makosa yaliyofanyika yataainishwa na waliofanya
kutambuliwa ili wachukuliwe hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa
kanuni za utumishi wa umma. Ndugu Wananchi; Ni muhimu kufanya hivi ili
haki itendeke ipasavyo. Mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa
na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo
sahihi. Lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili. Ni matumaini yangu pia
kwamba katika siku za usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa
kina ili wale hasa waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe. Uwajibikaji wa
wana-siasa peke yao hautoshi, kwani huwaacha waharibifu waendelee na kazi
isivyostahili. Mtindo huu utawafanya watumishi wasione umuhimu wa kutokurudia
makosa. Hata hivyo, pale kwenye ushahidi wa wazi kwamba kiongozi wa kisiasa
angeweza kuchukua hatua za kuzuia madhara lakini hakufanya hivyo lazima kiongozi
huyo awajibike. Ndugu Wananchi; Tunakamilisha matayarisho ya kuanza awamu
ya pili ya Operesheni Tokomeza. Ni muhimu kuendelea nayo kwani tusipofanya hivyo
majangili wataendelea na vitendo vyao viovu. Hali ni mbaya sana kwa upande wa
uwindaji wa ndovu. Nilipolihutubia Bunge tarehe 7 Novemba, 2013, nilieleza kuwa
tutafanya sensa ya ndovu katika Pori la Hifadhi la Selous. Sensa hiyo
imekamilika lakini taarifa yake inatisha. Kuna ndovu 13,084 tu wakati mwaka 1976
walikuwa109,419. Tusipoendelea na Operesheni hii baada ya miaka michache ijayo
hakutakuwa na ndovu hata mmoja. Halikadhalika, zoezi la kuondoa mifugo katika
mapori ya hifadhi ya taifa litaendelea. Katika awamu ya pili ya Operesheni hii,
washiriki watasisitizwa kutokutenda maovu yaliyofanyika katika awamu ya
kwanza. Mchakato wa Kuunda Katiba Ndugu wananchi; Tumefika mahala
pazuri katika mchakato wetu wa kutayarisha Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Jana Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, alitukabidhi
Rasimu ya Pili ya Katiba, mimi na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed
Shein. Kama nilivyosema jana kinachofuata sasa ni kuitangaza Rasimu hiyo katika
Gazeti la Serikali kwa kila mtu na hasa Wajumbe wa Bunge la Katiba, kuiona na
kuisoma. Baada ya hapo kitafuata kitendo cha kuifikisha Rasimu kwenye Bunge
Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupatikana Rasimu ya Mwisho
itakayofikishwa kwa wananchi kupigiwa kura. Ndugu Wananchi; Mchakato wa
kupata Wajumbe 201 watakaoungana na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
kuunda Bunge Maalum la Katiba umeanza. Ni matarajio yetu kuwa katika wiki ya
tatu ya Januari, 2014, uteuzi utakamilika. Siku 21 baada ya hapo Bunge la Katiba
litaanza. Hii ni kwa nia ya kuwapa nafasi Wajumbe hao kusoma Rasimu ya Katiba.
Baada ya Bunge la Katiba kumaliza kazi yake, utaanza mchakato wa Kura ya Maoni
itakayopigwa na wananchi ndani ya siku 74 baada ya Rasimu ya Katiba kupitishwa
na Bunge Maalum na kukabidhiwa kwa Rais. Iwapo Rasimu itakubaliwa na wananchi
hapo tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Lakini, iwapo Rasimu itakataliwa ina maana
kuwa Katiba ya sasa itaendelea kutumika mpaka hapo mchakato mwingine
utakapoanzishwa na Katiba mpya kupatikana. Ni matumaini yangu na, ni maombi
yangu na rai yangu kuwa Rasimu hiyo itakubalika ili nchi yetu isonge
mbele. Pongezi Ndugu Wananchi; Niruhusuni nitoe pongezi zangu za dhati
kwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Tume kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.
Najua haikuwa kazi rahisi hata kidogo lakini wameweza. Kwa namna ya pekee
nawashukuru wananchi kwa ushiriki wao mzuri uliowezesha zoezi la mabadiliko ya
Katiba kufikia hatua tuliyofikia sasa. Ndugu Wananchi; Ni matumaini yangu
na ndiyo matumaini ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
wataijadili Rasimu ya Katiba kwa makini na kufanya kila wawezalo kuiwezesha nchi
yetu kupata Katiba nzuri itakayoimarisha na kudumisha Muungano wetu. Katiba
itakayoendeleza umoja, upendo, udugu, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa
wananchi wa Tanzania. Katiba itakayoihakikishia nchi yetu amani, utulivu na
ustawi wa kiuchumi na kijamii. Ni imani yangu na ya Watanzania wote kuwa
Wajumbe wa Bunge la Katiba wataweka mbele maslahi mapana ya taifa na watu wake.
Wasiweke mbele maslahi yao binafsi au ya vikundi vyao vya kisiasa au kijamii.
Wakifanya vinginevyo kuna hatari ya kupata Katiba isiyokidhi haja na itakuwa
hasara kubwa kwa taifa letu na kwao pia. Uchumi Ndugu wananchi; Katika
mwaka tunaoumaliza leo, Tanzania iliendelea kupata mafanikio katika nyanja
mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jambo la kufurahisha ni kuwa
mafanikio hayo yamepatikana licha ya kuwepo changamoto kadhaa hapa nchini na
hali ya uchumi wa dunia kuwa bado haijatengemaa vya kutosha. Pato la taifa
limekua kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 6.9 mwaka jana. Tunategemea
kuwa mwaka 2014 pato la taifa litakua kwa asilimia 7.3. Mfumuko wa bei umeshuka
kutokaasilimia 12.1, Desemba, 2012 hadi asilimia 6.2, Novemba 2013. Lengo letu
ni kufikiaasilimia 5 mwezi Juni, 2014. Ndugu Wananchi; Hadi Novemba, 2013,
Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani
milioni 7,720.8 ukilinganisha na dola milioni 7,916.6 za mwaka ulioishia Novemba
30, 2012. Kushuka kwa bei za kahawa, pamba, katani, chai, karafuu na dhahabu
ndiko kulisababisha kupungua kwa mapato yetu ya fedha za kigeni. Hali hii
inatukumbusha umuhimu na uharaka wa kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani
mazao na bidhaa zetu tunazouza nje. Jambo hili tutalipa msukumo maalum mwaka
2014 na kuendelea. Pamoja na kushuka kidogo kwa mapato ya mauzo yetu ya nje
akiba yetu ya fedha za kigeni iliendelea kuwa nzuri. Hadi Novemba 30, 2013 akiba
yetu ilikuwa dola za Marekani 4,538 milioni. Hata hivyo, akiba hiyo inatuwezesha
kuagiza bidhaa toka nje wa miezi 4.4 ni chini ya lengo letu la miezi 4.5. Sina
wasiwasi kuwa mwaka 2014 tutaliziba pengo hilo. Ndugu Wananachi; Sekta
zilizochangia sana katika kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2013 ni pamoja na
mawasiliano asilimia 20.6, huduma ya fedha asilimia 13.2, uzalishaji viwandani
asilimia 8.2,madini asilimia 7.8, ujenzi asilimia 7.8, biashara asilimia 7.7 na
uchukuzi asilimia 7.1. Bado kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo ilikuwa ndogo
kwani ilikuwa asilimia 4.3. Pamoja na hayo, kilimo kinaendelea kutoa mchango
mkubwa kwa ustawi wa uchumi wa Tanzania na watu wake. Kilimo kinachangia
asilimia 24.7 ya pato la taifa na asilimia 10.7 ya mapato ya fedha za kigeni.
Kilimo kimeiwezesha nchi yetu kujitosheleza kwa chakula na kuvipatia viwanda
malighafi. Kwa upande wa mazao ya chakula, kwa mfano, mwaka huu uzalishaji
ulikuwa tani 14,383,845. Ukilinganisha na mahitaji yetu ya chakula ya
tani12,149,120 hivyo tunajitosheleza na kuwa na ziada kidogo. Ziada hii ni
kidogo mno hivyo inatulazimu mwaka ujao tuongeze maradufu juhudi na uwekezaji
katika kutekeleza shabaha na malengo ya kilimo. Ndugu Wananchi; Kwa ajili
ya uzalishaji wa chakula kuwa mzuri, mwaka huu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula wameweza kununua tani 233,689.8 za nafaka hadi kufikia Desemba 27, 2013
kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa miaka ya nyuma. Mwaka 2012 wakati kama huu
Wakala ilikuwa na kiasi cha tani 93,047.8 tu na kutulazimisha kutafuta chakula
nje ya nchi. Kwa ajili hiyo tulilazimika kuruhusu wafanyabiashara kuagiza
mahindi, mchele na sukari kutoka nje kwa nafuu ya kodi. Uamuzi huo umesaidia
nchi kuwa na chakula cha kutosha na kuuzwa kwa bei nafuu kwa walaji. Ndugu
Wananchi; Ni matarajio yangu, na ndiyo hasa dhamira yetu, kwamba mwaka 2014
tutapata mafanikio makubwa zaidi kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Naamini tutaweza kwa vile tumejipanga vizuri. Tunayo miradi ya kimkakati
iliyoainishwa vizuri katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na chini ya
Utaratibu wa Matokeo Makubwa Sasa. Miradi hiyo kama itatekelezwa kama
ilivyopangwa uchumi utakua kwa kasi kubwa zaidi, ajira nyingi zitapatikana na
huduma za kiuchumi na kijamii zitaboreka sana. Bahati nzuri tumeweka
utaratibu mpya na mzuri wa kufuatilia utekelezaji wa mipango, miradi na shughuli
za Serikali. Katika Ofisi ya Rais kumeanzishwa Ofisi maalum ya ufuatiliaji
ijulikanayo kama Presidential Delivery Bureau. Na, kila Wizara ina kitengo cha
namna hiyo kijulikanacho kama Ministerial Delivery Unit. Kwa ajili hiyo
utekelezaji wa miradi ya kimkakati na shughuli za Serikali utakuwa mzuri
zaidi. Mazingira ya Uwekezaji Ndugu Wananchi; Ni makusudio yetu kuwa
kuanzia sasa tutaihusisha sekta binafsi kwa nguvu zaidi katika utekelezaji wa
miradi na shughuli za maendeleo. Nimeagiza Presidential Delivery
Bureauishughulikie suala la uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji nchini. Sifa ya
nchi yetu kuhusu mazingira ya uwekezaji siyo nzuri. Kwa mujibu wa tathmini
inayofanywa kila mwaka na Benki ya Dunia, mwaka 2007 nchi yetu ilikuwa kati ya
nchi 10 bora duniani kwa kufanya mageuzi makubwa ya kupunguza gharama za kufanya
biashara. Mwaka huo tulikuwa nchi ya 142 kati ya nchi 175. Mwaka 2008 tukapanda
na kuwa wa 130 kati ya nchi 176, mwaka 2012 tulikuwa wa 134 kati ya nchi 185 na
sasa ni wa 145 kati ya nchi 185. Hali hii si nzuri hata kidogo kwa uchumi
unaokusudiwa kujengwa kwa kutegemea uwekezaji wa sekta binafsi. Tunategemea PDB
itatupa ushauri mzuri wa nini kifanyike kurekebisha mambo. Ndugu
Wananchi; Utekelezaji wa miradi ya Big Result Now (BRN) katika kilimo, umeme,
reli, barabara, bandari, maji, elimu na kuongeza mapato ya Serikali umeanza kwa
kasi inayoleta matumaini. Kama upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali
utakwenda inavyotarajiwa tutegemee mambo mengi mazuri kufanyika kuanzia mwaka
2014 mpaka 2016. Mpaka sasa hali ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali si
mbaya. Wastani kwa mwezi unakaribia shilingi bilioni 700 kuelekea shilingi
bilioni 800. Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa miezi ya Julai hadi Novemba
yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,008.1 kipindi kama hicho mwaka 2012 hadi
shilingi bilioni 3,555.5 mwaka 2013. Hata hivyo makusanyo ya Julai hadi Novemba,
2013 ni asilimia 88.1 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 4,036.8. Lengo
halijafikiwa kwa sababu ya kuchelewa kutekelezwa kwa baadhi ya marekebisho ya
mfumo wa kodi, hususan tozo ya simcard, kodi za mishahara kutokana na
kutokupandishwa kwa kima cha chini katika sekta binafsi na ya uhawilisho wa
fedha (money transfer). Pia kuendelea kwa mvutano baina ya TRA na
wafanyabiashara kuhusu bei za mashine za kodi. Ni matumaini yangu matatizo hayo
yatashughulikiwa na kumalizwa mapema iwezekanavyo ili tuweze kupata mafanikio
makubwa zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali mwaka
2014. Elimu Ndugu Wananchi; Kwa upande wa elimu tumeendelea kupata
mafanikio katika kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi na
sekondari. Mwaka huu tuliajiri walimu 28,666. Kwa ajili hiyo upungufu wa walimu
ni 57,755 kati yao 20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule za Sekondari.
Mapema mwaka ujao tutaajiri walimu wapya 36,100 kati yao 18,100 wa shule za
msingi na 18,000 wa sekondari. Kufanya hivyo kutafanya pengo lililopo liwe dogo
zaidi. Kwa upande wa shule za sekondari, tatizo la walimu wa masomo ya sanaa
tunakaribia kulimaliza. Changamoto yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya
sayansi. Upungufu ni walimu 26,998 na uwezo wa vyuo vyetu ni kutoa walimu wa
sayansi 2,300 kwa mwaka. Mapema mwaka 2014 tutakutana na wadau wa elimu nchini
kujadiliana juu ya mkakati wa haraka wa kulikabili tatizo hili. Nilipanga
tufanye hivyo mwaka huu lakini mambo yaliingiliana sana hatukuweza. Ndugu
Wananchi, Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya
kujifunzia na kufundishia. Tuliongeza fedha katika bajeti ya elimu kwa ajili ya
vitabu. Hivi sasa usambazaji wa vitabu vyenye thamani ya shilingi bilioni 76 za
bajeti ya mwaka 2012/13 unaendelea. Kwa sababu hiyo hivi sasa upungufu wa vitabu
umeshuka na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi 3. Naamini shilingi bilioni 49
zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya vitabu itafanya
mambo kuwa nafuu zaidi. Tukiendelea kuwekeza kama tufanyavyo sasa shabaha yetu
ya kila mwanafunzi wa msingi na sekondari kuwa na kitabu chake kwa masomo yote
ifikapo 2016 itatimia. Ndugu Wananchi; Mwaka huu tumeanza utekelezaji wa
mpango mkubwa wa kujenga nyumba za walimu. Kwa kuanzia tumetenga shilingi
milioni 500 kwa kila Halmashauri. Tumeanza na Halmashauri 40,mwaka ujao na miaka
inayofuata tutaongeza fedha zinazotengwa na kuzifikia Halmashauri zote. Kwa
upande wa ujenzi wa maabara katika sekondari za kata napenda kuwakumbusha Wakuu
wa Mikoa na Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji, kuwa kila
mmoja ahakikishe kuwa ifikapo Novemba, 2014 malengo yanatimia. Wasisubiri
kuulizwa. Maji Ndugu Wananchi; Kwa kutambua umuhimu wa maji kwa maisha
ya wanadamu na uchumi katika bajeti ya mwaka huu wa fedha sekta ya maji imepewa
upendeleo katika mgao wa fedha. Tutaendelea kuongeza fedha katika bajeti mbili
zinazofuata ili watu wengi zaidi mijini na vijijini wapate maji safi na salama.
Kama fedha zitapatikana kama ilivyopangwa na utekelezaji ukasimamiwa vizuri
tunatarajia kuwa katika mwaka 2013/14 watu milioni 7.1 watapata maji. Katika
mwaka ujao wa fedha 2014/15 tumepanga kuwapatia maji watu wengine milioni 7 na
mwaka utaofuata (2015/16) tutaongeza tena huduma hiyo kwa watu milioni 1.3 na
kufanya tufikie asilimia 74 ya Watanzania wanaopata maji safi na salama ifikapo
2015/2016. Afya Ndugu wananchi; Tumeendelea kupata mafanikio katika
kuendeleza upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa Tanzania. Zahanati,
vituo vya afya na hospitali zimeendelea kujengwa kote nchini. Aidha, hospitali
za wilaya, mikoa, kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuboreshwa.
Kwa ajili hiyo idadi ya Watanzania wanaoweza kupata huduma ya afya iliyo bora
inazidi kuongezeka. Hali kadhalika, wataalamu wa afya wa fani mbalimbali
wameongezeka na hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba imezidi kuboreshwa.
Pamoja na yote hayo bado kuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu. Kufanya hayo
ndiyo dhamira yetu kuu kwa mwaka 2014. Ndugu wananchi; Tumeendelea kupata
ushindi katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayoua watu wengi nchini. Kwa
upande wa malaria, kwa mfano, maambukizi ya ugonjwa huo kwa watoto na mama
wajawazito yamepungua kutoka asilimia 18 hadi 9.5. Tutaendelea kugawa vyandarua
kwa wajawazito na watoto kwa kutumia hati punguzo pamoja na kusisitiza matumizi
ya dawa mseto na kupulizia dawa ya kuua mbu majumbani. Aidha, tunatarajia kupata
mafanikio zaidi miaka ijayo kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluilui vya
mbu wanaoeneza malaria kitapoanza kazi. Ndugu Wananchi; Mambukizi ya
UKIMWI yameshuka hadi asilimia 5.1. Inaleta faraja kuona watu wengi wamejitokeza
kupima afya zao kwa hiari. Mpaka sasa watu milioni 18 wamepima. Tunao watu
1,298,402 walioorodheshwa kwa ajili ya kupata huduma ya tiba na kati yao
485,715wanapata dawa. Waliosalia watapata wakati wao ukifika. Mpaka sasa
vituo 4,603 vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto vimeanzishwa nchini kote tangu mpango huo uzinduliwe tarehe 1
Desemba, 2012. Idadi yake inaendelea kuongezeka. Ni dhamira yetu kuendeleza
jitihada za kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa Watanzania. Mafanikio
ya kampeni hii pamoja na ile dhidi ya malaria ndiyo chachu ya mafanikio
tuliyopata katika kupunguza vifo vya watoto nchini na kufikia lengo la Milenia
mwaka huu. Magonjwa ya Moyo Ndugu Wananchi; Katika mwaka 2013
tunaoumaliza leo, tumeshuhudia mambo kadhaa mazuri yakifanyika yanayoelezea
mafanikio tunayoendelea kuyapata katika jitihada zetu za kujenga uwezo wa tiba
kwa maradhi tunayopeleka wagonjwa nje ya nchi. Niruhusuni niyataje baadhi yake.
La kwanza, ni kuanza kazi kwa Kituo cha Tiba na Mafunzo ya Magonjwa ya Moyo
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Hiki ni kituo kikubwa na cha aina yake
cha matibabu ya maradhi ya moyo hapa nchini. Huduma za kisasa za uchunguzi na
matibabu ya maradhi ya moyo ambazo zamani zilikuwa zinapatikana nje ya nchi sasa
zinaweza kupatikana hapa hapa nchini. Kwa kuwa na vitanda 100 vya kulaza
wagonjwa, Watanzania wengi wataweza kuhudumiwa na maisha yao kuokolewa. Ndugu
Wananchi; Katika kituo hiki watu wanaweza kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo
(open heart surgery), uwekaji wa mashine ya kuongezea nguvu kwenye moyo
(pacemaker), uwekaji wa vyuma vidogo katika mishipa ya damu ya moyo ambayo
imebanana (stent). Tangu kituo kianze kazi rasmi tarehe 30 Aprili, 2013 mpaka
sasa watu 347 wamefanyiwa upasuaji wa moyo na watuwatatu wamewekewa pacemaker
tangu huduma hiyo ianze Novemba, 2013. Mapema mwakani kituo kinatarajiwa kuanza
huduma ya kuweka stent. Kituo hiki ni kipya hivyo katika mwaka 2014
tutaendelea kukijengea uwezo wa vifaa tiba, wataalamu na mahitaji mengine muhimu
ili kulipunguzia taifa mzigo wa kupeleka wagonjwa nchi za nje. Serikali, pia
itaendeleza ushirikiano wake na uongozi wa Hospitali ya Kanda ya Bugando
kuboresha huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo katika hospitali hiyo. Huduma hiyo
ilizinduliwa tarehe 26 Oktoba, 2013 na Makamu wa Rais Mheshimiwa Daktari Mohamed
Ghalib Bilal.
Saratani Ndugu Wananchi: Kwa upande wa
maradhi ya saratani, Februari, 2013 jengo jipya la kulaza wagonjwa
170lilifunguliwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Kufunguliwa kwa jengo
hilo kumeongeza uwezo wa taasisi yetu hiyo kulaza wagonjwa 290 badala ya 120 tu
kabla ya hapo. Ujenzi wa jengo hili jipya umesaidia sana watu wengi zaidi
kuhudumiwa na kupunguza msongamano mkubwa wa wagonjwa
uliokuwepo.
Figo Ndugu Wananchi: Kuhusu maradhi ya
figo mwaka huu pia tumeshuhudia huduma ya usafishaji wa figo zenye matatizo
ikipanuliwa. Huduma hiyo imeanzishwa tena katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya na
imeanzishwa kwa mara ya kwanza katika Chuo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha
Dodoma. Pale Mbeya tayari wagonjwa 93 wamehudumiwa mwaka huu na kuwapa matumaini
mapya ya maisha yao. Kwa pale Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa kituo kikubwa
kitakachobobea kwa magonjwa ya figo unaendelea na unategemewa kukamilika mapema
mwaka 2014.
Mafunzo Ndugu Wananchi: Katika mwaka
2013 tumefungua ukurasa mpya katika jitihada zetu za kuongeza wataalamu wa afya
nchini. Chuo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma kimefanya mahafali
yake ya kwanza ambapo wanafunzi 50 wa Shahada ya Uuguzi walihitimu. Tunatarajia
kuanza kupata madaktari kuanzia mwaka 2014.
Kwa
upande wa mchakato wa kujenga makazi mapya ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi
Shirikishi cha Muhimbili kule Mloganzila mchakato umeanza. Ujenzi wa miundombinu
ya barabara, maji na umeme unaendelea hivi sasa. Mwaka 2014 ujenzi wa Hospitali
ya kisasa ya kufundishia yenye vitanda 650 utaanza.
Ujenzi wa Mlonganzila ukikamilika Chuo Kikuu cha
Muhimbili kitaweza kuchukua wanafunzi 15,000 wa fani zote ukilinganisha na 3,060
wa sasa. Hatua hiyo itaongeza sana uwezo na kasi yetu ya kupunguza uhaba wa
Madaktari, Wauguzi na wataalam wengine wa afya.
Nyumba Ndugu Wananchi: Katika mwaka
2013 ujenzi wa nyumba 35 za kuishi watumishi wa afya katika mikoa ya Mtwara (5),
Rukwa (20) na Singida (10) umekamilika. Ujenzi wa nyumba 100 unaendelea. Nyumba
hizo ni sehemu ya mpango wa ujenzi wa nyumba 580 zinazojengwa kwa ushirikiano
kati ya Serikali na Global Fund kwa awamu mbili.
Awamu ya kwanza zinajengwa nyumba 310ambapo taasisi ya
Benjamin William Mkapa Foundation ndiyo mtekelezaji wa ujenzi huo. Napenda
kutumia nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin
Mkapa kwa mchango wake mkubwa alioutoa na anaoendelea kutoa kwa maendeleo ya
nchi yetu na watu wake.
Ujenzi
wa Miundombinu Ndugu wananchi: Katika mwaka 2013, tumeendelea kupata
mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na
angani. Kasi ya ujenzi wa barabara imeendelea kufanyika kote nchini. Kazi ya
ujenzi ingekuwa nzuri zaidi kama mtiririko wa malipo kwa Wakandarasi ungekuwa
mzuri. Tatizo hili tutalitafutia ufumbuzi mwaka 2014 ili kasi ya ujenzi wa
barabara za lami nchini iwe nzuri zaidi.
Pamoja na
hayo mwaka huu kilomita 877 za barabara zimekamilika. Ujenzi wa daraja la
Malagarasi nao umekamilika kinachosubiriwa ni sherehe za uzinduzi. Ujenzi wa
daraja la Kilombero umeanza na ule wa daraja la Kigamboni unaendelea
vizuri.
Tunatarajia kuwa
mwakani tutaongeza zaidi kasi ya ujenzi wa barabara zilizosalia ikiwa ni pamoja
na kujenga baadhi ya barabara kwa ubia na sekta binafsi. Kwa kasi na mwenendo
tunaoendelea nao sasa naamini ifikapo mwaka 2015 tutakuwa tumefikia hatua ya juu
sana katika shabaha yetu ya kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za
lami. Ndugu
Wananchi: Jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar
es Salaam zimeendelea kutekelezwa. Barabara kadhaa zilipanuliwa na kazi
inaendelea. Ujenzi wa njia ya kupita mabasi yaendayo haraka umeendelea kwa kasi
ya kuridhisha. Mchakato wa ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika njia
panda za TAZARA na Ubungo umeshaanza. Mwaka ujao huduma ya usafiri wa treni
kusafirisha abiria Dar es Salaam itaongezwa ili watu wengi zaidi
wanufaike.
Ndugu wananchi: Mwaka huu, kwa upande wa
reli ya kati, kazi ya kuboresha njia ya reli imeendelea kufanyika na itaendelea
mwaka 2014. Mwakani (2014) Shirika la Reli litapokea injini mpya 13, mabehewa ya
mizigo 274 na breki 34 hivyo kuboresha sana huduma katika reli ya kati. Kuhusu
ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa ni matarajio yetu kuwa kama kila kitu
kitaenda sawa mchakato wa ujenzi utaanza katika nusu ya pili ya mwaka
2014.
Ndugu Wananchi: Tumetoa kipaumbele cha
juu katika kuboresha huduma ya usafiri wa anga nchini. Mwaka huu, tumeendelea na
ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mikoa ya Kilimanjaro,
Kigoma, Tabora, Mwanza, Arusha, Mtwara na Kagera. Ni jambo la kufurahisha kuona
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe ukianza kutumika. Hatimaye ndoto
imetimia. Mwaka wa 2014 ujenzi wa majengo mengine ya kuhudumia abiria, mizigo na
ndege utaendelea katika uwanja huo.
Pia ni
furaha iliyoje kwamba upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na ujenzi wa gati la
Kilindoni vimekamilika. Kero ya miaka mingi imepatiwa ufumbuzi. Kazi ya ujenzi
wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
itaanza rasmi mwaka 2014.
Nishati Ndugu wananchi: Dhamira yetu
ya kutaka Tanzania iwe na umeme wa uhakika na unaonufaisha watu wengi imepata
sura na mwelekeo mzuri mwaka huu 2013. Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na
Songosongo kuja Dar es Salaam umeanza na utekelezaji unakwenda vizuri. Kama
ujenzi wa bomba utakamilika kama inavyotarajiwa na ujenzi wa mitambo ya
kuzalisha umeme Kinyerezi utaenda kama ilivyopangwa, ifikapo mwaka 2015 Tanzania
itafikia lengo la kuzalishamegawati 3,000 za umeme.
Ndugu
Wananchi: Bahati nzuri mwaka huu, kufuatia kuongezewa fedha za bajeti,
kasi ya usambazaji umeme imekuwa nzuri. Tunaumaliza mwaka huku idadi ya
Watanzania waliounganishiwa umeme ikiwa imefikia asilimia 24 ukilinganisha na
asilimia 21 mwaka 2012 na asilimia 10 mwaka 2005. Haya si mafanikio madogo. Kwa
mwelekeo huu, kufikia lengo la asilimia 30 ya Watanzania kupata umeme mwaka 2015
ni jambo la uhakika kabisa sasa. Tena kuna uwezekano mkubwa wa kulivuka lengo
hilo.
Ushirikiano wa Kanda Watanzania
Wenzangu: Katika mwaka 2013, nchi yetu imeendelea kushiriki vizuri katika
shughuli za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo sisi ni wanachama. Mwezi wa Agosti, 2013
tulikabidhi Uenyekiti wa chombo cha SADC kinachoshughulikia Siasa, Ulinzi na
Usalama kwa Namibia. Tulikuwa tumemaliza kipindi chetu cha mwaka
mmoja.
Katika kipindi chetu cha uongozi tulishiriki kwa
ukamilifu kutafuta suluhu kwa mizozo na migogoro ya kisiasa na kiusalama nchini
Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Madagascar. Tunafurahi kuona
kwamba mambo katika nchi zote hizo sasa yanakwenda
vizuri.
Nchini Zimbabwe
utulivu umerejea baada ya kufanyika kwa uchaguzi mwezi Julai, 2013. Nchi ya
Madagascar nayo imemaliza duru ya pili ya uchaguzi wa Rais kwa usalama. Matokeo
yanatarajiwa kutangazwa tarehe 7 Januari, 2014. Ni matumaini yetu kuwa watu wa
nchi hiyo watayapokea matokeo hayo na wataelekeza nguvu zao katika kujenga umoja
na maridhiano ili wajenge upya uchumi wa nchi yao.
Kwa
upande wa Mashariki ya Kongo, tishio kubwa la usalama kutokana na vitendo vya
kundi la waasi la M23 limezimwa na Jeshi la Kongo kwa kushirikiana na Jeshi la
Umoja wa Mataifa. Kama mjuavyo Tanzania ni moja ya nchi zinazochangia maafisa na
askari wa Jeshi hilo.
Ndugu
Wananchi: Napenda kutumia nafasi hii, kwa mara nyingine tena kutoa
pongezi zangu za dhati kwa wanajeshi wetu kwa kazi yao nzuri na iliyotukuka
waliyoifanya huko Mashariki ya Kongo. Pia nawapongeza wanajeshi wetu walioko
Darfur na Lebanon kwa kazi yao njema waifanyayo. Wote nawaomba waendelee
kudumisha nidhamu na weledi, mambo yaliyowafanya wapewe sifa nyingi na
kuheshimiwa.
Wameiletea
nchi yetu heshima kubwa. Bahati mbaya, katika kutimiza wajibu wao huo wa
kimataifa tumepoteza vijana wetu 10, sabaDarfur na watatu Kongo. Narudia kutoa
pole kwa Jeshi letu na familia za marehemu kwa msiba mkubwa uliowakuta. Napenda
kuwahakikishia kuwa daima tutauthamini na kuuenzi mchango wao. Wanajeshi wote
tunawatakia heri na fanaka tele katika mwaka 2014.
Jumuiya ya Afrika Mashariki Ndugu
Wananchi: Mwaka huu, ushiriki wetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
umepita katika mtihani kidogo kufuatia ndugu zetu wa Uganda, Rwanda na Kenya
kufanya mambo ambayo yalijenga hisia ya kuwepo mifarakano. Pia yalileta hofu
kuwa hata uhai wa Jumuiya yenyewe ulikuwa mashakani. Katika mkutano uliopita wa
Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 mambo
hayo tuliyazungumza kwa uwazi na kidugu. Tumeelewana kuwa yaliyopita si ndwele
tugange yajayo.
Ndugu Wananchi: Katika mkutano wa Kampala
tuliamua mambo matatu makubwa na muhimu katika kuendeleza agenda ya utangamano
wa Afrika Mashariki. La kwanza, tulikubaliana kuhusu Itifaki ya kuanzisha Umoja
wa Fedha wa Afrika Mashariki na kutia saini. Hii ndiyo hatua ya juu ya
utangamano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Tumekuwa
tunashirikiana katika kuwianisha sera za uchumi, fedha na bajeti, kwa uamuzi huu
sasa tunaelekea kwenye kuwa na sera moja ya fedha na bajeti kwa mambo hayo na
hatimaye sarafu moja. Baada ya hatua hii, inayofuata ni ile ya utangamano wa
kisiasa, yaani Shirikisho la Kisiasa. Katika mkutano wetu wa Kampala
tulikubaliana kuwa nchi wanachama ambazo hazijakamilisha kutoa maoni yao,
zifanye hivyo kisha baada ya hapo tuzungumzie jambo hilo na kulipa
mwelekeo.
Ndugu
Wananchi: Vilevile katika kikao chetu cha Kampala, tuliridhia mpango wa
utekelezaji wa uamuzi wetu wa awali wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la mfumo au utaratibu huu ni kufanikisha
utekelezaji wa malengo na madhumuni ya Umoja wa Forodha wa Afrika
Mashariki.
Utaratibu huu
utarahisisha na kuharakisha uingizaji na utoaji wa bidhaa katika bandari na
mipaka ya nchi za Afrika Mashariki. Pia, utaondoa vikwazo visivyokuwa vya kodi
katika uingizaji na usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi wanachama kwenda nchi
nyingine. Kwa jumla, Himaya Moja ya Forodha itasaidia biashara kukua na hivyo
uchumi wa nchi wanachama kukua na kuboresha ustawi wa wananchi wa Afrika
Mashariki.
Narudia kuwakumbusha wenzetu wa Wizara ya Afrika
Mashariki na Wizara ya Fedha kutengeneza utaratibu mzuri wa kuelimisha jamii
kuhusu Umoja wa Fedha na Himaya Moja ya Forodha. Nawataka Wizara ya Fedha,
Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya
Ndani, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya
Mapato na Jeshi la Polisi, kuhakikisha kuwa taratibu zote husika kuhusu Himaya
Moja ya Forodha zinakamilishwa mapema. Nia yangu na yetu sote ni kuona
utekelezaji unaanza mara moja. Hili ni jambo lenye maslahi makubwa kwa nchi
yetu.
Medani
za Kimataifa Ndugu
Wananchi: Katika medani za kimataifa, mwaka 2013 ulikuwa mzuri kwa
Tanzania. Nyota ya nchi yetu iliendelea kuangaza vizuri. Tumeendelea kuwa na
uhusiano mwema na mataifa yote duniani na hakuna nchi ambayo tuna uadui nayo.
Pia tuna uhusiano mzuri na mashirika ya kimataifa na kikanda yanayoshughulikia
masula ya siasa, fedha na maendeleo.
Vile vile, tuna uhusiano mzuri na watu mashuhuri na
mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulikia masuala ya maendeleo na ya
kibinadamu. Kwa sababu hiyo tumepata misaada mingi ya maendeleo na ya
kibinadamu iliyochangia katika mafanikio tuliyoyapata katika maendeleo ya
kiuchumi na kijamii mwaka 2013.
Napenda kwa niaba yenu nitumie nafasi hii kutoa
shukrani zangu za dhati kwa nchi, mashirika na watu waliochangia katika
maendeleo ya nchi yetu mwaka huu. Wakati tukiwashukuru, napenda kuwakumbusha
kuwa misaada yao bado tunaihitaji mwaka ujao (2014) na miaka
inayofuatia.
Ndugu Wananchi: Kwa upande wa wageni,
mwaka huu ulikuwa wa baraka sana kwa Tanzania. Tumepata heshima ya aina yake ya
kutembelewa na Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jiping tarehe 24 – 25 Machi, 2013 na
Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Obama tarehe 01 - 02 Julai,
2013.
Pia tulitembelewa na
Rais wa Sri Lanka Mheshimiwa Mahinda Rajapaksa tarehe 26 – 27 Juni, 2013. Waziri
Mkuu wa Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra tarehe 30 Julai mpaka Agosti 1,
2013 Pamoja na hao, tulipokea Wakuu wa Nchi na Serikali 19 waliokuja kushiriki
mkutano wa Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni,
2013.
Ndugu Wananchi: Vilevile, tulitembelewa
na Marais Wastaafu wa Marekani, Mheshimiwa Bill Clinton na Mheshimiwa George W.
Bush. Nchi yetu inanufaika na misaada inayotolewa na mashirika yao katika nyanja
za afya na kilimo.
Napenda
kutumia nafasi hii kuwashukuru wageni wetu wote hao kwa uamuzi wao wa kuja
kututembelea. Wameipa nchi yetu heshima kubwa. Ni matumaini yetu kuwa mwaka 2014
utaendelea kuwa wa baraka kama huu tunaoumaliza leo. Pia nawashukuru sana
Watanzania wenzangu kwa kuwapokea vizuri wageni wetu. Wameondoka nchini wakiwa
na furaha kubwa na kumbukumbu nzuri kuhusu nchi yetu.
Licha ya
kutembelewa, mimi na viongozi wenzangu Wakuu wa Nchi yetu tulialikwa na kufanya
ziara katika nchi mbalimbali duniani. Pia tumeshirikishwa katika mikutano
mbalimbali ya kimataifa. Ziara hizo zimekuwa na manufaa makubwa kwa nchi
yetu.
Ndugu Wananchi: Katika kikao cha Wakuu wa
Nchi wa Umoja wa Afrika kilichofanyia mwezi Januari, 2013 nilichaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika ya kushughulikia masuala ya
mabadiliko ya tabia nchi. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndiye huwa mwakilishi na
msemaji wa Bara la Afrika katika majukwaa ya kimataifa ambapo masuala hayo
yanazungumzwa au kushughulikiwa.
Kwa ajili
hiyo nilikwenda Warsaw, Poland kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 19 wa Mabadiliko ya
Tabia Nchi uliofanyika tarehe 11 – 22 Novemba, 2013. Katika mkutano huo
hatukufanikiwa vya kutosha. Hivi sasa matumaini yetu yapo katika mkutano wa
mwakani (2014) nchini Peru.
Iwapo tutafanikiwa tutakuwa tumejenga msingi mzuri
utakaowezesha Mkutano wa Paris mwaka 2015 kufanikiwa kupatikana Mkataba wa
Kimataifa unaozifanya nchi ziwajibike kisheria kwa masuala yahusuyo kupunguza
athari za mabadiliko ya tabia nchi. Ikishindikana Peru na kama mataifa
yataendelea kukaidi katika mkutano wa Paris, hatma ya dunia yetu itakuwa
mashakani kwani hali si nzuri hata kidogo.
Ndugu
Wananchi: Mwaka huu tunaoumaliza nchi za SADC tumepoteza mmoja wa
viongozi wetu mashuhuri, shujaa Nelson Mandela. Nilipata nafasi ya kuwawakilisha
katika sala ya kitaifa, kutoa heshima za mwisho na mazishi yake. Kule Qunu,
nilipewa nafasi ya kuzungumza ambayo niliitumia kuelezea uhusiano wetu na shujaa
Mandela, ANC na mchango wa Tanzania kwa ukombozi wa kusini mwa
Afrika.
Hotuba yetu
ilipokelewa vizuri sana na wenyeji kwani niliwaelezea baadhi ya mambo ambayo
walikuwa hawayajui. Watu wengi wa Afrika Kusini na duniani kwa jumla sasa
wanaufahamu vizuri mchango mkubwa wa nchi yetu kwa ukombozi wa Afrika Kusini.
Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema, peponi roho ya shujaa
Nelson Mandela. Miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano
Ndugu
Wananchi: Mwaka ujao (2014) ni wa aina yake katika historia ya nchi yetu.
Ni mwaka ambao tunatimiza miaka 50 tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya
Januari 12,1964 na miaka 50 ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Tanganyika ziungane na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 26,
1964. Ni mwaka wa kutambua na kusheherekea mafanikio tuliyoyapata. Lakini, ni
mwaka wa kuweka nadhiri ya kupata mafanikio makubwa zaidi miaka 50 ijayo na
kuendelea. Tutakiane heri katika kusheherekea siku hizo adhimu. Shukurani Ndugu Wananchi: Napenda
kuchukua nafasi hii adhimu kuwashukuru kwa dhati Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali
Idd.
Viongozi Wakuu wenzangu
hao nawashukuru kwa msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa katika
kuiongoza nchi yetu mwaka 2013. Naomba tuendelee hivyo mwaka 2014 kwa maslahi ya
nchi yetu na watu wake.
Nawashukuru pia Mawaziri na viongozi wengine wa
Serikali zetu mbili kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuongoza na kusimamia
utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za Serikali. Kazi yao nzuri ndiyo
iliyotupatia mafanikio tunaojivunia leo. Naomba sote tutambue kuwa bado zipo
mbele yetu kazi nyingi na changamoto kubwa na nzito za kushughulikia katika
jitihada zetu za kuwaletea wananchi na nchi yetu
maendeleo.
Tunao wajibu wa
kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu wa nchi yetu. Hatuna budi
kuendelea kushirikiana na kusaidiana pamoja na kufanya kazi kwa bidii zaidi
mwaka ujao 2014 kwa niaba na kwa maslahi ya watu waliotuchagua.
Ndugu
Wananchi: Kwa namna ya pekee nawashukuru sana Watanzania wote po pote
pale walipo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kufanya kazi kwa bidii na
maarifa kujiletea maendeleo. Hali kadhalika nawapongeza kwa uelewa wenu
ulioiwezesha nchi yetu kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Nawaomba tuendelee na
moyo huo wa kuipenda nchi yetu na kujitolea kwa ajili ya utulivu wake na
maendeleo yake na yetu sote.
Naomba
pia nimalize kwa kuwashukuru viongozi wetu wa dini wa madhehebu mbalimbali
pamoja na waumini wao kwa sala na maombi katika kipindi chote cha mwaka unaoisha
leo.
Sala zao na maombi yao
yametupa nguvu na faraja katika vipindi vigumu ambavyo tumevipitia. Naomba
muendelee kuliombea taifa letu ili lipate baraka na neema ya Mwenyezi
Mungu. MWISHO. Ndugu
Wananchi; Naomba tuzidi kuombeana heri ili mwaka ujao uwe wa baraka na
mafanikio makubwa zaidi. Twendeni tukasherehekee mwaka mpya kwa amani na
utulivu. Nawatakia heri na fanaka tele katika mwaka mpya wa
2014. Mungu Ibariki
Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni