Alhamisi, 2 Januari 2014

RAIS KIKWETE: BAADA YA KUKAMILIKA KWA MATAYARISHO YA AWAMU YA PILI, OPERESHENI TOKOMEZA UJANGILI KURUDI KWA KASI




DAR ES SALAAM.
RAIS Jakaya Kikwete amesema Operesheni Tokomeza Ujangili iliyositishwa kwa muda kutokana na utekelezaji wake kukumbwa na kasoro na kusababisha mawaziri wake wanne kuwajibika kisiasa, itaendelea baada ya kukamilika kwa matayarisho ya awamu yake ya pili.

Akizungumza katika salamu zake za Mwaka Mpya jana, Rais Kikwete alisema: “Tunakamilisha matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza.


Ni muhimu kuendelea nayo kwani tusipofanya hivyo majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.

“Wakati nikilihutubia Bunge Novemba 7, mwaka jana niliagiza ifanyike sensa katika Pori la Hifadhi la Selous. Hali ni mbaya, sensa imekamilika lakini taarifa yake inatisha. Kuna tembo 13,084 tu wakati mwaka 1976 walikuwa na tembo 109,419.”

Rais Kikwete ametoa kauli hiyo ikiwa zimepita siku 12 tangu Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilipotoa ripoti yake iliyoeleza athari mbalimbali za operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji, uharibifu wa mali na mauaji ya binadamu na mifugo.

Ripoti hiyo ilisababisha, Rais kutengua uwaziri wa Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi), Dk David Mathayo (Mifugo na Uvuvi) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), baada ya wizara zao kutajwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa operesheni hiyo.

Hata hivyo, Rais alisema mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo sahihi. “Lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili. Ni matumaini yangu pia kwamba katika siku za usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe.

“Uwajibikaji wa wana-siasa peke yao hautoshi, kwani huwaacha waharibifu waendelee na kazi isivyostahili. Mtindo huu utawafanya watumishi wasione umuhimu wa kutokurudia makosa. Hata hivyo, pale kwenye ushahidi wa wazi kwamba kiongozi wa kisiasa angeweza kuchukua hatua za kuzuia madhara lakini hakufanya hivyo lazima kiongozi huyo awajibike.”

Kuhusu umuhimu wa kuendelea na operesheni hiyo alisema: “Tusipoendelea na operesheni hii, baada ya miaka michache ijayo hakutakuwa na tembo hata mmoja.


Zoezi la kuondoa mifugo katika mapori ya hifadhi ya taifa litaendelea na katika awamu ya pili ya operesheni hii, washiriki watasisitizwa kutokutenda maovu yaliyofanyika katika awamu ya kwanza.”

Alisema tangu mwaka 2010 Serikali ilianzisha operesheni mbalimbali kupambana na ujangili wa wanyamapori na uvunaji haramu wa rasilimali za misitu, lakini kutokana na majangili kutumia silaha na mbinu, aliamua kuhusisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama na hapo ndipo ilipoanza Operesheni Tokomeza.

“Pamoja na matatizo yake, katika Operesheni Tokomeza tumebaini mitandao ya ujangili na wahusika kadhaa wametiwa nguvuni.


Mitandao hiyo inahusisha watu wa aina mbalimbali, wamo raia wa kawaida, watu maarufu, watumishi wa idara mbalimbali za Serikali wakiwamo wa Idara za Wanyamapori na Misitu,” alisema.

Alisema katika operesheni hiyo watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za kijeshi 18, za kiraia 1,579 na shehena kubwa za meno ya tembo na nyara mbalimbali.

“Niliagiza operesheni hii isitishwe na uchunguzi ufanyike kubaini kasoro zake sambamba na waliofanya makosa wachukuliwe hatua. Wakati suala hilo likiendelea, Bunge likaunda kamati na matokeo yake mliyaona, mawaziri wanne wamewajibika kisiasa,” alisema Rais Kikwete. MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni