NA FRANCIS GODWIN:
MAELFU ya wakazi wa mkoa wa Iringa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na Serikali wakiongozwa na Rais Dr Jakaya Kikwete wameshiriki katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kalenga na waziri wa fedha Dr Wiliam Mgimwa.
Huku waziri mkuu Mizengo pinda katika salam zake za serikali akielezea jinsi ambavyo Taifa lilivyopata pigo kubwa kufuatia kifo cha Dr Mgimwa kutokana na mchango wake katika baraza la mawaziri.
Katika mazishi hayo yaliyofanyika leo kijiji kwake Magunga jimbo la Kalenga wananchi mbali mbali walionyesha kujipanga barabarani kutoka Manispaa ya Iringa hadi kijijini kwake huku wakiupungia mkono msafara wa rais Kikwete na baadhi yao wakilazimika kutumia usafiri wa baiskeli na pikipiki kwenda katika mazishi hayo.
Akitoa shukrani za familia kwa niaba ya familia mtoto wa marehemu Dr Mgimwa Godfrey Mgimwa aliishukuru serikali kwa jinsi ambavyo ilivyohangaika kumuuguza baba yake na kutoa wosia mzito wa marehemu Dr Mgimwa ambao alimtaka kuufikisha kwa Rais Kikwete..
Alisema katika uhai wake kabla ya kifo chake ikiwa ni siku tano kabla Dr Mgimwa alimwita na kumtaka kufikisha shukrani zake kwa Rais Kikwete kwa kumtembelea mara mbili Hospital alipokuwa amelazwa pamoja na spika wa bunge Anne makinda .
Pia alisema kuwa alieleza dhamira yake ya kuwatumikia wana Kalenga na kusema zawadi kubwa ni msaada wa bati zaidi ya 2000 kwa wananchi hao ili kuendeleza ujenzi wa shule na vituo vya afya jimboni.
"Baba kabla ya kufa aliniachia wosia huo juu ya wana Kalenga kwa kuwashukuru kwa ushirikiano wao na kutoa bati ila alipenda kuona Kalenga inakuwa na maendeleo zaidi"
Kwa upande wake waziri Mkuu Pinda alisema kuwa serikali imepata pigo kubwa juu ya kifo hicho na kuwa bado serikali itaendelea kuwa karibu na familia ya Dr Mgimwa na pale penye tatizo isisite kuwasiliana .
Hata hivyo Rais Kikwete hakupata kuzungumza chochote katika msiba huo zaidi ya kuweka mchanga na shada la maua pamoja na kuwapa mkono ndugu wa Dr Mgimwa .
Spika wa bunge Anne Makinda alisema kuwa bunge limempoteza kiongozi na mbunge aliyependa kutumia nafasi yake kwa ajili ya Taifa na kuwa kamwe mchango wake hawataacha kuukumbuka
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni