Jumatatu, 24 Machi 2014

RISASI ZA MOTO NA MABOMU ZATUMIKA NZEGA, DKT KIGWANGALA ALIPOKAMATWA NA WACHIMBAJI WADOGO WA NZEGA WALIVYOTAWANYWA NA POLISI

Jeshi la polisi wilayani Nzega mkoani Tabora jana limemkamata mbunge wa jimbo la Nzega Dkt. Hamis Kigwangalla aliyekuwa kwenye maandamano ya wachimbaji wadogo wa dhahabu ya kupinga kufungwa kwa machimbo yao ya Mwashina yaliyo jirani na mgodi wa Resolute Tanzania Limited.
Kabla ya hapo mbunge huyo alifanya mkutano mkubwa wa hadhara na wachimbaji hao katika kijiji cha Nzega Ndogo wilayani humo ambapo alielezwa matatizo ya kufungwa kwa machimbo hayo na kamishna wa madini nchini Bw. Paulo Masanja bila kujali gharama walizoingia wachimbaji hao wadogo kwenye eneo hilo.
Katika mkutano huo wachimbaji hao walidai ni vema serikali iangalie haki zao zilizotumika kwenye uendeshaji na uchimbaji wa mashimo hayo kuliko kuwafungia bila kujali ingawa eneo hilo liko ndani ya leseni ya mgodi wa Resolute lakini wao ndiyo wamiliki wa ardhi hiyo.
Hata hivyo katika hoja hiyo mbunge huyo aliwataka wachimbaji hao kudai haki yao kwa kufuata taratibu zinazostahili bila kujali tofauti zao kisiasa, kikabila na kidini na badala yake wawe kitu kimoja.
Baada ya kauli hiyo mbunge huyo aliwaambia wachimbaji hao wadogo kuwa haki yao iko mikononi mwao hivyo ni uamuzi wao wa kudai haki yao na yeye kama mwakilishi wao yuko nyuma yao mpaka pale haki yao itakapopatikana.
Wachimbaji hao walimwomba mbunge huyo kuambatana nao kwenye maandamano ya amani kutoka kijiji cha Nzega Ndogo kwenda Mwashina yalipo machimbo yaliyofukiwa umbali wa zaidi ya kilomita tatu kujionea hali halisi ya kufukiwa kwa eneo hilo na ikiwezekana kufanya mkutano mwingine wa hadhara kijijini hapo.
Kufuata hali hiyo wachimbaji hao walianza maandamano ambayo yaliungwa mkono na mbunge huyo hadi kijiji cha Mkwajuni kabla ya kufika Mwashina ambapo polisi waliibuka na kuyasambaratisha maandamano hayo kwa mabomu ya machozi na risasi za moto.
Katika na purukushani hizo polisi walifanikiwa kumkamata mbunge huyo na kumjeruhi mtu mmoja kwa risasi ya moto kwenye paji la uso ambapo waliondoka nae kwenye gari pamoja na mbunge huyo.
Awali askari wa jeshi hilo waliziba njia na kuwazuia waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa vitisho mbalimbali ingawa hali hiyo ilitulia baada ya maandamano ya wachimbaji kujitokeza.
Pichani ni mmoja kati ya waandamanaji hao aliyekuwa karibu na Dkt Kigwangalla akiwa chini baada ya kujeruhiwa na polisi
Mlipuko wa mabomu kwa mbali


Awali mbunge wa Nzega Dkt Hamis Kigwangalla akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini hao katika kijiji cha Nzega Ndogo kabla ya maandamano
Maandamano baada ya mkutano wa Dkt Kigwangalla kuelekea eneo la machimbo ya Mwashina wilayani Nzega.
 
Kamanda wa polisi mkoani Tabora Suzan Kaganda alipopigiwa simu na waandishi wa habari alisema hana taarifa yoyote kuhusiana na maandamano hayo, kukamatwa kwa mbunge huyo wa jimbo la Nzega na kutumika kwa risasi za moto na mabomu ya machozi kuzuia maandamano hayo.
Tayari Dkt Kigwangala ametoka polisi usiku wa kumkia leo
Na Kadama Malunde-Nzega,Tabora
NA JIACHIE BLOG

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni