Jumatatu, 31 Machi 2014

KASEBA ASHINDWA KWA POINTI


Thomas Mashali (kulia) akipambana na Japhert Kaseba.
 

Baada ya kushushiwa kipigo, bondia Japhet Kaseba amesema jambo lililompa faraja ni kutopigwa kwa Knock Out (KO) na Thomas Mashali katika pambano lao la kuwania ubingwa wa UBO Afrika lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam juzi.

 

Majaji wote watatu, Pembe Ndava, Robert Amos na Omary Yazidu walimpa ushindi Mashali wa pointi 97-94.

 

Kaseba alisema anaheshimu matokeo ya majaji kwani wao ndiyo waamuzi wa mwisho na kueleza kuwa angejutia zaidi kama angepigwa kwa KO, lakini kwa pointi bondia yoyote anaweza kupewa ushindi.

 

Alisema licha ya kupigwa, hakuna cha ajabu alichokifanya mpinzani wake kwenye pambano hilo ila raundi nne za mwanzo ndizo zilimpa ushindi Mashali.

"Nilichelewa kufungua na kushambulia raundi nne za mwanzo nikidhani namvutia muda mpinzani wangu ili achoke nami nimalize mchezo, lakini ikawa ndivyo sivyo, mahesabu tu ndiyo yalikataa hakuna kingine, najuta kwa nini nilimuachia acheze raundi za mwanzo," alisema Kaseba.

Katika pambano hilo la uzani wa light heavy, Kaseba alianza vizuri raundi ya kwanza na dakika ya pili aliachia konde la mkono wa kulia lililompata sawia Mashali na kumpeleka chini ingawa alikuwa mwepesi kunyanyuka na kuendelea na mchezo kabla ya mwamuzi wa pambano, Anthony Lutha kumhesabia.

 

Mashali alizinduka raundi ya pili hadi ya tano na alicheza kwa kushambulia hali iliyosababisha mpinzani wake kujihami kwa kukumbatia, kitendo kilichomfanya azomewe na mashabiki wa Mashali waliojitokeza kwa wingi.

 

Raundi ya saba, nane na ya tisa, Kaseba alibadilisha mchezo na kushambulia hivyo kumpa wakati mgumu mpinzani wake ambaye katika raundi hizo alitumia muda mwingi kujihami.

"Kaseba alikuwa anaongea sana. Aliahidiwa gari kama angenipiga hivyo zawadi hiyo imeota mbawa. Tangu mwanzo nilisema Kaseba hana uwezo wa kunipiga akabisha sasa naamini amekubali kiwango chake bado," alitamba Mashali dakika chache baada ya kuvikwa mkanda wa UBO Afrika.

Mashali alisema baada ya kipigo hicho hivi sasa anajipanga 'kumnyamazisha' Karama Nyilawila ambaye atapigana naye Mei Mosi jijini Dar es Salaam kuwania ubingwa wa dunia wa UBO.

Kaseba ana rekodi ya kushinda mapambano 5 (3 kwa KO) amepigwa mara 4 (3 kwa KO) hajawahi kutoka sare tangu 2000 alipoingia kwenye ngumi za kulipwa.

 

Wakati Mashali ameshinda mapambano 10 ( 5 kwa KO), amepigwa mara 2 zote kwa KO na kutoka sare mara moja tangu 2009 alipoingia kwenye ngumi za kulipwa.

Chanzo, mwananchi (TK)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni