MASIKINI wa Mungu mama huyu wa kijiji cha Buhundwe wilayani Rorya mkoani Mara akitambulika kwa jina la Catherine Benedicto, amepokea kichapo kikali toka kwa mwanamke mwenzie aliyetajwa kwa jina la Bi. Tatu Wambura kwa kosa la eti kupitisha ng'ombe kwenye eneo la shamba linalomilikiwa na Bi. Tatu.
Inatajwa kuwa jumatano katikati ya wiki tunayoimalizia majira ya saa sita mchana, Catherine akiwa anaswaga ng'ombe wake wapatao 30 hivi na ushee kutoka nyumbani kwake kuelekea malishoni alipitisha mifugo hiyo katika shamba la Bi Tatu Wambura, ambalo hata hivyo lilikuwa halijalimwa wala halikuwa na mazao yoyote na ndipo alipoonwa na Bi Tatu alivamiwa na kupewa kipigo kikali kilichoambatana na makofi na mangumi hata kumpelekea mwanamama huyo kupata maumivu makali sambamba na uvimbe katika baadhi ya sehemu zake za mwili hasa jichoni.
Hadi kamera yetu inaondoka eneo la tukio suala hilo lilikuwa tayari limefikishwa mbele ya uongozi wa kijiji na tayari hatua za kisheria zilikuwa zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni sambamba na taratibu za matibabu kwa Bi. Catherine.
Tukio hili linatokea ikiwa ni siku chache tu taifa la Tanzania likitoka kuungana na nchi nyingine ulimwenguni kuadhimisha siku ya Mwanamke duniani ambapo suala la unyanyasaji na ukatili limekuwa likitizamwa na kukemewa huku mtu ambaye anatajwa sana kuhusishwa na ukandamizaji pamoja na ufanyaji ukatili akitajwa kuwa ni mwanamme.
Lakini kwa taswira hii ya mwanamke kumpiga mwanamke mwenzie tena kwa kumshambulia kiasi cha kutisha inaleta taswira gani?
Ni moja kati ya baadhi ya nyumba majirani za watu wa kijiji cha Buhundwe wilayani Rorya mkoani Mara, maisha yanaendelea na hapa binti mdogo Robi akitimiza majukumu ya nyumbani kama mtoto. PICHA NA ZEPHANIA MANDIA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni