Jumanne, 18 Machi 2014

MATESO ANAYOPATA HUYU MAMA, MSAADA WAKO UNAHITAJIKA


hatar

HUJAFA hujaumbika. Hicho ndicho unachoweza kusema ukimuona na baadaye kumsikiliza Disnia Rajabu,32, mkazi wa mtaa wa Geza Ulole mkoani Tanga ambaye anaumwa uvimbe wa mguu kwa muda wa miaka 10 sasa bila kupata nafuu.Disnia hakuzaliwa na tatizo hilo, bali alilipata ukubwani, tena akiwa tayari ameshaolewa, lakini katika hali ya masikitiko makubwa, anadai mumewe alimkimbia mara baada ya kugundua kuwa yupo katika majaribu makubwa kabisa katika maisha yake.Na kutokana na kukimbiwa na mumewe, mwanamke huyo sasa anaishi na wazazi wake, ambao nao wana uwezo mdogo kiuchumi, hivyo licha ya kutopata matibabu ya uhakika, pia maisha yake yeye na watoto wake watatu ni ya kubahatisha, kwani mara kadhaa hukosa kula.

“Ni bora nisingezaliwa kwa mateso niliyonayo, sina raha kabisa duniani kwani nina miaka kumi nipo kitandani, huwa nalia wanangu wanaponijia na kunililia kuwa wana njaa hawajui kuwa sina uwezo wa kuwatunza,” anasema mama huyo.

Akisimulia kuhusu mume wake, anadai walioana mwaka 2002 kwa ahadi ya maisha ya raha na shida, licha ya ukweli kwamba maisha yao yalikuwa ya chini, lakini alipopata ugonjwa huo, mwenzake alimkimbia bila kuaga na simu zake hazipatikani kila anapompigia.
“Nilizaliwa nikiwa mzima wa afya njema, mwaka 2004, usiku nikiwa nimelala, kichwa kiliniuma ghafla huku mwili wote ukitokwa na jasho, asubuhi kulipokucha, mwili ulikuwa umevimba.
“Nilichukuliwa hadi Hospitali ya Bombo, nililazwa siku saba, presha ilikuwa juu, niliwekewa dripu, nilichomwa sindano, presha ikashuka, uvimbe ulipungua isipokuwa mguu, madaktari waliniruhusu kwenda nyumbani ili nianze kliniki.
“Walinipima damu wakifikiri ni ugonjwa wa matende, walipogundua haukuwa huo, walinipa vidonge vya kutumia nyumbani lakini haikusaidia kwani nilikuwa napata maumivu makali sana huku mguu ukiendelea kuvimba,” anasimulia mama huyo kwa uchungu mkubwa.
Alisema hakuwa akipumua vizuri na mguu wake uliendelea kuvimba hadi alipojikuta akishindwa kutembea. Kuanzia wakati huo, akawa ni mtu wa kitandani, akila na kujisaidia hapo hapo. Ni wakati huo ndipo mumewe, ambaye hakumtaja jina alipoamua kumtoroka na kuwafanya wazazi wake kwenda kumchukua alipokuwa akiishi naye.
“Hali ilizidi kwa mbaya, wazazi wangu wakawa ni watu wa kulia tu, hawakuwa na uwezo, wakajiuliza jinsi ya kunileta Hospitali ya Muhimbili kwani baba ni kuli na mama yangu anapika na kuuza maandazi.”

Lakini anasema baadaye wazazi wake walipata wazo la kuomba msaada kwa watu na kufanikiwa kupata fedha zilizowatosha kumfikisha katika Hospitali ya Muhimbili, Februari mwaka jana.
“Nililazwa kwa muda wa wiki mbili, wazazi wakaambiwa wanichukue na kunipeleka hospitali moja ya binafsi ili nikapate kipimo ambacho pale Muhimbili hakipatikani kinachogharimu shilingi 470,000, walipigwa na butwaa, ilibidi wachukue picha yangu na kuanza kutembeza bakuli mtaani, Mungu akawasaidia wakapata hizo fedha.
“Walinichukua hadi hospitali hiyo, hata hivyo, haikugundulika kinachonisumbua, nilirejeshwa Muhimbili, daktari akanishauri nitafute pa kukaa ili niwe nahudhuria kliniki, sikuwa na ndugu Dar es Salaam, wazazi wakanirudisha nyumbani Tanga tukisubiri muda wa kwenda kliniki.
“Nililetwa Muhimbili mara mbili ndani ya wiki mbili, baadaye daktari alinieleza niendelee kukaa nyumbani nikisubiri muda wa kwenda India ambapo ugonjwa wangu ungeweza kujulikana na kupatiwa matibabu, sasa ni muda mrefu napata maumivu, nakaa nyumbani bila matibabu yoyote na haijulikani lini nitapelekwa nje kutibiwa.
“Baada ya kuona kimya muda mrefu, tulimpigia simu daktari wangu wa Muhimbili ili kujua siku ya kwenda India, akajibu haijulikani kwani serikali haina bajeti, tulipouliza ni kiasi gani, wakasema zinatakiwa shilingi milioni 20.
“Nilipowaeleza wazazi waliinamisha vichwa chini na kuniambia nisubiri kufa, hakuna jinsi, nilitokwa na machozi nikatamani kujiua, sasa naleta ombi kwenu wananchi, naomba muokoe maisha yangu.
“Licha ya matatizo ya matibabu lakini hata njaa inanikabili, wazazi hawana uwezo, kuna wakati tunakosa hata chakula, nina watoto watatu nimetelekezewa na baba yao, naishi kwa kutegemea msaada wa kila kitu, nyumba ninaishi na wazazi wangu nusu ya paa imeezekwa kwa makuti na bati, imekuwa ikivuja wakati wa mvua,” alisema Disnia.
Kwa yeyote aliyeguswa na mateso ya mama huyu na ana nia ya kumsaidia awasiliane kwa namba 0755 033718, 0685 836159 au 0719 546505.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni