Watu 25 wamethibitika kufa mkoani Dar es Salaam nchini Tanzania
kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo kuanzia Ijumaa hadi
Jumapili iliyopita.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amethibitisha
kutokea kwa vifo hivyo akisema watu wengine 14 wanadaiwa kufa, lakini
hawajathibitishwa na polisi.
Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam wenye wilaya tatu, amesema watu 11
wamekufa katika wilaya ya Ilala, huku wengine wawili hawajaonekana mpaka
sasa.
Taarifa kutoka wilaya ya Temeke imesema watu saba wamethibitishwa kufa
kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha.
Pia kuna taarifa za watu 21 kufariki dunia katika wilaya ya Kinondoni, japo
hawajathibitishwa.
Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam Bwana Sadik amesema miundombinu ya
barabara na madaraja imeanza kurejeshwa baada ya kuharibiwa na mafuriko na
kusababisha mkoa wa Dar es Salaam kukosa mawasiliano ya ndani na pia kukosa
mawasiliano na mikoa jirani. (TK)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni